loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uoto wazidi kupotoea kwa ukataji miti, uchomaji misitu

UTAFITI umeonesha kuwa eneo lenye misitu katika Tao la Mashariki limepungua kutoka kilometa za mraba 18,000 eneo la asili hadi kilometa za mraba 4,750 katika miaka ya hivi karibuni.

Vile vile utafiti huo pia umeonesha kuwa takribani kiasi cha asilimia 0.1 cha uoto hupotea kila mwaka kutokana na uharibifu unaohusisha upanuzi wa mashamba kwenye maeneo ya misitu, ukataji miti ovyo, uchimbaji wa madini na uchomaji wa moto.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori) kupitia ufadhili wa Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF) ilifanya utafiti uliowezesha kupatikana mfumo wa kieletroniki kutoa taarifa za uhalifu wa misitu iliyopo kwenye milima ya Tao hilo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tafori, Dk Revocatus Mushumbusi alisema hayo juzi katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao kazi cha wadau juu ya kutoa mapendekezo ya kuboresha mfumo  huo ili kufikia lengo la kupunguza uhalifu kwenye misitu ya Tao la Mashariki.

Alisema kuwa misitu iliyopo kwenye milima ya Tao la Mashariki ni muhimu kwa taifa letu hasa katika kuendeleza uchumi wa viwanda na kuboresha maisha ya wananchi.

Dk Mushumbusi alisema zaidi ya asilimia 25 ya Watanzania wanatengemea misitu ya milima ya Tao la Mashariki kwenye upatikanaji wa maji katika shughuli mbalimbali za kujikumu na kipato.

Alisema pamoja na hilo uchumi wa viwanda unatengemea sana maji na nishati ya umeme na kwamba maji hayo kutoka kwenye mito mbalimbali imekuwa na manufaa kwa taifa.

“Kwa mfano mito ya Wami, Kilombero, Ruvu, Zigi, Ruaha na Pangani yote inatiririka kutoka  miinuko ya maeneo mbalimbali katika Misitu ya Milima ya Tao la Mashariki  na ina manufaa makubwa kwa shughuli za kilimo kwenye maeneo ya mabondeni,” alisema.

Dk Mushumbusi alisema mito ya Kilombero na Ruaha inatiririsha maji ambayo ni muhimu katika kuzalisha umeme hapa nchini katika vituo vya Mtera, Kidatu, Kihansi na kwenye mradi mpya wa Julius Nyerere.

Hata hivyo, alisema nishati ya umeme inayotumia maji kutoka Misitu ya Milima ya Tao la Mashariki inachangia takribani asilimia 50 ya nishati ya umeme wa taifa.

Dk Mushumbusi alisema serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto za uharibifu wa misitu ikiwemo kuifanyakuwa misitu ya asili ambapo ulinzi wake umeongeza na kufanya utafiti mbalimbali ili kuboresha ulinzi wa misitu hiyo.

Mratibu wa mradi huo, Dk Chelestino Balama alisema utengenezaji wa mfumo wa kutoa taarifa za uharifu wa misitu iliyopo kwenye  milima ya Tao la Mashariki ni miongoni mwa mradi iliyofadhiliwa na na Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki katika mwaka 2019/20.

Dk Balama alisema  lengo la mfuko huo ni kusaidia jamii kutoa taarifa za uhalifu wa misitu kwa mamlaka zinazohusika ili ziweze kuchukua hatua stahiki na kwa wepesi , wakati , kwa ajili  ya kupunguza athari za uhalifu katika misitu ya Tao la Mashariki.

Alisema katika utengemezaji wa mfumo huo, watafiti wa Tafori walikusanya mahitaji ya mfumo kutoka kwa wadau, waliitengeneza na kuujaribu pamoja na kutoa mafunzo kwa baadhi ya vijiji vinavyozunguka misitu ya Tao la Mashariki.

“Mfumo huu ni wa kieletroniki kwa kutumia simu, ni mfumo thabiti na una usiri mkubwa wa mtoa taarifa na utasaidia kuthibiti uhalifu kwenye misitu ya Tao la Mashariki… mfumo huu utaanza  kutumika mwaka huu wa fedha wa 2020/21  kwa vile  kuwa tayari mafunzo yametolewa kwa vijiji vinavyozunguka milima ya tao la Mashariki,” alisema Dk Balama.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki, Raymond Killenga alisema misitu ya Tao la Mashairiki ina vivutio mbalimbali hivyo kutoa fursa kwa utalii wa ekolojia, lakini pia misitu hiyo inahifadhi viumbe hai ambavyo havipatikani mahali pengine duniani.

Killenga alisema hali ya hewa na madhari nzuri iliyoko katika misitu hiyo inawezesha kilimo cha mazao mbalimbali na kuchangia kwa kiasi kikibwa katika kulisha jamii za mijini, kuinua kipato kwa jamii za wakulima na hatimaye kupunguza umaskini wa wananchi .

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi