loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tume yataka wasimamizi kufuata kanuni, sheria

MKURUGENZI wa Taifa wa Tume ya Uchaguzi, Dk Wilson Mahera amewataka waratibu wa mikoa, wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa mikoa ya Arusha na Manyara kuhakikisha wanazingatia kanuni, sheria na maelekezo watakayopewa na tume na kuonya kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Dk Mahera alisema hayo jana jijini Arusha wakati akifungua mafunzo kwa waratibu wa mikoa, wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi yanayofanyika kwa siku tatu Jijini Arusha katika ukumbi wa ofisini ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Hotuba ya ufunguzi ya Dk Mahera ilisomwa na Mkurugenzi wa Idara ya elimu ya mpiga kura Tume ya Uchaguzi Taifa, Dk Cosmas Mwaisobwa na washiriki 116 kutoka katika mikoa ya Arusha na Manyaraa walishiriki lengo ni kutaka uchaguzi kuwa huru na haki wenye kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya tume ya uchaguzi.

Dk Mahera alisema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatiwa kwani hatua na taratibu ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama sio kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.

Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha siku tatu za mafunzo zinawabadilisha na kupata uzoefu, kujadili namna ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na pia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa pamoja na kuwa baadhi ya washiriki kuwa na uzoefu katika kuendesha uchaguzi, wahakikishe wanazingatia maelekezo watakayopewa na tume badala ya kufanya kwa mazoea lakini pia kuhakikisha wanazingatia matakwa ya katiba ya nchi ,sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi.

Alisema washiriki hao wameteuliwa na kuaminiwa kufanya kazi kwa sababu wana uwezo wa kufanya kazi hiyo jambo la muhimu ni kujiamini na kujitambua na wanapaswa kuzingatia katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na tume na sio vinginevyo.

Dk Mahera aliwataka waratibu wa mikoa ,wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao muhimu kwa kushirikisha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika masuala ambayo wanastahili kushirikishwa.

Alisema vile vile ni muhimu kwao kuhakikisha wanayajua na kuyatambua vyema maeneo wanayofanyia kazi ikiwepo miundombinu ya kufika katika kata na vituo vya kupigia kura ili kurahishisha shughuli za upigaji kura kuanza mapema na kumalizika katika muda uliopangwa.   

Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Dk John Pima ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Arusha alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha washiriki kufuata maadili ya kazi yao ikiwa ni pamoja na kuzingatia viapo walivyoapa.

Dk Pima alisema iwapo kila mmoja atawajibika na kutii kiapo alichoapa ikiwa ni pamoja na kutunza siri kamwe uchaguzi hautakuwa na changamoto yoyote.

Mkurugenzi wa Halmshauri ya Longido Mkoani Arusha, Dk Jumaa Mhina alisema kuwa jimbo lake lina jiografia ngumu sana lakini amejipanga kikamilifu kukabiliana na hilo ili siku ya upigaji kura vifaa vyote viwe vimefika siku moja kabla ya upigaji kura kitaifa.

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: John Mhala, Arusha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi