loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Samia ataka taasisi za fedha kuongeza mikopo

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan (pichani) ametoa wito kwa taasisi za kifedha nchini kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kwa wakulima, wavuvi na wafugaji ili waweze kuongeza mitaji na uzalishaji na kuongeza tija zaidi katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Makamu wa Rais, Samia alitoa wito huo juzi wakati akizindua Maonesho ya Kilimo maarufu NaneNane 2020 yanayofanyika kitaifa Uwanja wa Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu yakiwa na kauli mbiu “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020”.

Alisema licha ya taasisi hizo kuwa wachangiaji wakuu wa maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, bado kuna umuhimu kwao kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kwa wadau wa kilimo huku akibainisha kipindi hiki ni asilimia tisa ya mikopo iliyotolewa na taasisi hizo ndio imekwenda kwenye sekta ya kilimo.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema wizara yake imeanzisha mpango mpya wa usajili wa wakulima ili kuiwezesha serikali kujua taarifa muhimu za wakulima ikiwemo aina ya mazao wanayozalisha, kiwango cha uzalishaji wao na msaada wanaohitaji serikalini.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC, Theobald Sabi alisema taasisi za fedha zina nafasi kuboresha ustawi wa sekta ya kilimo. “Ndio sababu NBC inabuni huduma kuwasaidia wadau wa sekta hii muhimu kama huduma ya ‘NBC Shambani,”alisema na kuongeza:

“Tunajivunia kuwa sehemu ya maonesho haya tukiwa washiriki na wadhamini muhimu. Maendeleo ya kilimo yamekuwa ni miongoni mwa vipaumbele vyetu na tunakuwa mstari wa mbele kukuza sekta hii muhimu,” alisema.

Alisema benki hiyo imekuwa ikidhamini maonesho hayo kwa mwaka wa tatu mfululizo ambapo mwaka huu imechangia udhamini wa Sh milioni 40 ili kufanikisha maonesho hayo.

Sabi alisema benki hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan- Trade) wameandaa mafunzo maalumu kwa wafanyabiashara wakiwemo wadau wa kilimo katika kipindi chote cha maonesho hayo, wakilenga kuwajengea uwezo zaidi kibiashara.

Maonesho hayo yanalenga kutoa jukwaa kwa wadau wa kilimo nchini kubadilishana utaalamu hususani kiteknolojia, kutafuta masoko mapya sambamba na kupata fursa ya kukutana na watunga sera muhimu kuhusu sekta hiyo.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Simiyu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi