loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanaume suluhisho vipigo kwa wanawake

SHIRIKA lisilo la kiserikali la masuala ya ukatili wa kijinsia la Kawie Social Development (KASODEFO) Maswa mkoa wa Simiyu, limesema suluhisho la kukomesha vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto lipo kwa wanaume.

Limesema, licha ya serikali na wadau kuendelea kukabili janga hilo, linalonyima haki wanawake litaisha wanaume wakishirikishwa kulipiga vita.

Akizungumza kwenye Maonesho ya Kilimo maarufu Nanenane kitaifa viwanja vya Nyakabindi mkoa Simiyu, Meneja mradi wa shirika hilo, Marius Isavika alisema wanaume ndio wenye uwezo wa kumaliza tatizo hilo.

Isavika alisema shirika hilo katika mradi wao ambao wanaoutekeleza mkoani humo wa uimarishaji upatikanaji wa haki kupitia msaada wa kisheria endelevu, wameona kuna haja ya wanaume kushirikishwa katika mapambano.

Alisema mradi huo wameanza kutekeleza tangu mwaka 2016 na kubaini wanaume wamekuwa hawashirikishwi kila hatua hali ambayo imesababisha matukio hayo kuendelea nchini.

“Mashirika mengi yamekuwa yakiwashirikisha waathirika pekee (wanawake) kupiga vita hili lakini kume tunakosea, lazima wanaume washirikishwe kila hatua ili waweze kutatua matatizo yao wenyewe,”alisema Isavike.

Alisema lazima serikali na wadau wabadilishe mfumo na kuanza kuwajumushia wanaume ili waweze kutambua kile ambacho wanawafanyia wake au watoto wao ni unyama na siyo sahihi.

Mratibu huyo alisema katika kutekeleza mradi huo, wamegundua vitendo vimeendelea kuwepo lakini vinapungua kufuatia wanawake kutambua haki zao na pa kupeleka madai yao.

“Wengi(wanawake) hawajui kama ni haki yao kumiliki ardi, uchumi wa familia, wana haki kwenye mali wanazozalisha, kati ya kesi 10 ambazo tumepokea, nane zinahusu ukatili wa kijinsia na migogoro ya ardhi,” alisema.

Alisema kuwa shirika hilo limeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii jinsi ya kupambana na ukatili ikiwa pamoja na kutoa msaada wa kisheria kwa wenye matatizo.

JAMII imehadharishwa dhidi ya tabia ya ...

foto
Mwandishi: Happy Mollel, Bariadi

Post your comments

Habari Nyingine