loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkapa: Ningependa vyama vilenge kujenga umoja na ustawi wa taifa

Ijumaa iliyopita tulianza kuchapa hotuba ya Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Bemjamim Mkapa aliyoitoa Desemba 31, 2004 ikiwa ni salamu za mwaka mpya wa 2005 ambao ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi.

Tunaendelea na hotuba hiyo kujikumbusha alichosema mkapa wakati Taifa likijiandaa kwa uchaguzi mkuu kama ilivyo kwetu mwaka huu.

Ndugu Wananchi, Hatukuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kujenga chuki miongoni mwa Watanzania.

Hivyo, tuwaogope sana wanaohubiri chuki kwa kisingizio cha ushindani wa kisiasa. Ushindani tunaoutaka sisi ni wa hoja, ni wa fikra, ni wa mikakati na mipango ya maendeleo.

Tunashindanisha Ilani za Uchaguzi za Vyama. Ningependa vyama vyote vya siasa viwe na malengo makuu yanayofanana –umoja, amani, upendo, maendeleo na ustawi wa taifa na wananchi.

Kinachotutofautisha na tunachoshindania kiwe mipango na mikakati ya kufikia malengo hayo. Tunapoingia kwenye mwaka wa uchaguzi, napenda vyama vyote, na wananchi wote, turejee kwenye maadili haya na malengo haya.

Nasema maneno haya kwa uchungu wa nchi yetu, na sijui nitumie lugha gani tuelewane. Tushindane kwa sera na mikakati; tusishindane kwa ubabe na vitisho. Na sera haiwezi kuwa KUINGIA IKULU.

Sera ya kuingia IKULU ni sera ya ubinafsi; tena ubinafsi wa hali ya juu. Maana, hoja si kwenda IKULU; hata tausi wanaishi IKULU. Hoja ni unakwenda IKULU kuwafanyia nini Watanzania? Atafutaye kuongoza Watanzania lazima awe mnyenyekevu, anayejua anatafuta kutumwa, hatafuti kutumikiwa.

Hayo ndiyo maadili ya Taifa waliyotuachia waasisi wetu. Nataka mwaka wa 2005 tujikumbushe maadili hayo, na tukubaliane miongoni mwa vyama vyote vya siasa kuyazingatia na kuyafuata.

Tarehe 28 Juni 1962, wakati akiwasilisha Bungeni muswada wa kuifanya iliyokuwa Tanganyika kuwa Jamhuri, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alizungumzia kwa kina umuhimu wa kuwa na maadili ya kitaifa, yanayozingatiwa na kila raia mwema na kila kiongozi. Alisema:

Hoja lazima ijengwe kwamba hatimaye kinga madhubuti ya haki za raia, uhuru wa raia, na mambo yote wanayoyathamini, hatimaye yatahifadhiwa na maadili ya kitaifa.

Taifa linapokuwa halina maadili yanayowezesha Serikali kusema: “Hatuwezi kufanya hivi, huu si U-Tanganyika”. Au watu kusema: “Hili hatuwezi kulivumilia, huu si U-Tanganyika.” Iwapo watu hawana maadili ya aina hiyo, haisaidii sana hata kama wangekuwa na Katiba iliyoandikwa vizuri sana.

Bado raia wanaweza kukandamizwa... Tunachopaswa kukifanya ni kujenga maadili ya taifa hili, kila mara kuimarisha maadili ya taifa hili, maadili yatakayomfanya Rais yeyote yule kusema, “Ninayo madaraka ya kufanya jambo hili chini ya Katiba, lakini sitalifanya, maana huu si U-Tanganyika.”

Au kwa watu wa Tanganyika, iwapo wamekosea na kumchagua mwenda wazimu kuwa Rais, mwenye madaraka ndani ya Katiba ya kufanya XYZ, akijaribu kufanya hivyo, watu wa Tanganyika waseme, “Hatutakubali hili lifanyike, hata alitake Rais au Rais maradufu, hatulikubali, maana huu si U-Tanganyika.”

Ndugu Wananchi, Nimenukuu kwa kirefu maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kwa sababu naamini hapa tulipofika kwenye mageuzi ya kisiasa tunaanza kutetereka na hivyo tunahitaji sana kuzingatia busara zake.

Naomba wananchi mniunge mkono kuwa mwaka 2005 uwe wa kurejea kwenye maadili ya kitaifa—maadili ya kutetea kwa nguvu zote uhuru, umoja, amani, utulivu, upendo na mshikamano. Huu ndio uwe U-Tanzania.

Tuwe na maadili yanayotusukuma kupinga kwa nguvu zote ubaguzi, udini, ukabila, chuki na visasi.

Mwaka 2005 tukatae kiongozi wa dini kutuchagulia chama au mgombea. Tuseme hapana, huu si U-Tanzania.

Tukatae chama au kiongozi wa chama anayetumia udini, ukabila au umajimbo kutafuta madaraka. Tuseme, hapana! Huo si U-Tanzania. Tumkatae kiongozi wa siasa, au hata raia mwenzetu, ahubiriye chuki, uhasama na ubaguzi wa aina yo yote ile.

Tuseme hapana! Huo si U-Tanzania. Wananchi mkiamua, na kukubaliana nami, nchi yetu itang‘oa mbegu zote zinazopandwa za chuki, ubaguzi na fujo, na kuturejesha kwenye maadili ya ki-Tanzania. Hiyo ndiyo changamoto kubwa kuliko zote mwaka wa 2005. La sivyo, katika miaka michache ijayo, Tanzania haitakuwa tofauti na nchi nyingine za Kiafrika wanakouana wenyewe kwa wenyewe.

Na vurugu za kisiasa ni kama yule jini kwenye hadithi za Alfu Lela Ulela; akishatoka kwenye chupa ni vigumu sana kumrejesha. Tumwombe Mungu apishie mbali, lakini pia kila raia mwema adai kwa bidii zote kuheshimiwa kwa maadili yetu ya kitaifa.

Tunapoelekea kwenye uchaguzi watakuja wengi kwa kivuli cha Asasi Zisizokuwa za Serikali ati kutuelimisha kuhusu demokrasia. Wanaoijua Tanzania, na raia wake, wanajua sisi si mbumbumbu wa siasa wala demokrasia. Sisi ni mfano kwa wengine, mfano wa uhamasishaji wa kisiasa na kimaendeleo. Sisi pia ni waumini wa uhuru, usawa na kujitegemea.

Na SISI WENYEWE NDIYO WAJUZI NA WATETEZI WA U-TANZANIA! HALI YA KIUCHUMI Ndugu Wananchi: Kwa ujumla, uchumi wetu umeendelea kuwa bora mwaka hadi mwaka kufuatia utekelezaji wa mageuzi ya uchumi yenye lengo la kuongeza uwekezaji na uzalishaji bidhaa bora, na kutoa huduma bora.

Mitaji katika sekta za umma, hasa miundombinu ya kiuchumi na kijamii, na katika sekta binafsi, imeendelea kuongezeka. Pamoja na ukame wa msimu uliopita, bado uchumi wetu umeendelea kukua kwa karibu asilimia 6, na mfumuko wa bei bado upo chini ya asilimia 5.

Mapato ya serikali yameendelea kuongezeka. Wastani wamapato ya Serikali Kuu kwa miezi mitano iliyopita, Julai -Novemba 2004, ni Sh bilioni 133 kwa mwezi.

Mapato haya yakichanganywa na misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka nje, na msamaha wa kiasi fulani cha madeni ya nje tuliopewa, ndiyo huiwezesha Serikali kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi kama vile barabara, madaraja na vivuko; na miundombinu ya kijamii kama vile shule za msingi na sekondari, ujenzi na ukarabati wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, na kuviwekea vifaa vya kisasa.

Yote haya ni kwa faida ya Watanzania wote. Hivyo wanaosema kuwa mageuzi ya uchumi tuliyoyafanya hayana faida kwa wananchi wa kawaida si wakweli.

HALI YA KIJAMII:

Ndugu Wananchi, Serikali inatumia sekta za huduma za jamii kuhakikisha kwamba mafanikio kwenye uchumi mkuu na mageuzi yake yanawafikia wananchi wa kawaida, mijini na vijijini.

Chini ya mwavuli wa Mkakati wa Kupunguza Umaskini, unaoshirikisha wadau wote, tumeendelea kuboresha huduma za jamii, ikiwemo elimu, afya na maji, na kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI na malaria.

Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) unaendelea kuleta mafanikio mengi. Matatizo yake ya awali yameshughulikiwa. Mwaka 2005 ni wa kukamilisha yaliyobaki ili kuhakikisha kuwa, ifikapo mwaka 2006, kila mtoto wa Kitanzania, wa kike na wa kiume, anapata elimu bora na kamili ya msingi.

Wanafunzi wengi zaidi sasa wanasoma, walimu wengi zaidi wameajiriwa, vyumba vya madarasa bora na vingi zaidi vimejengwa, na elimu inayotolewa ni borazaidi.

Kiashiria muhimu cha mafanikio ya MMEM ni kufaulu kwa wanafunzi wamalizao elimu ya msingi. Na kama mlivyosikia, mwaka huu 2004, watoto wetu wa kike na wa kiume waliomaliza elimu ya msingi wamefanya vizuri kwenye mitihani yao kuliko wakati wote tangu tuanzishe Baraza la Mitihani la Tanzania mwaka 1973.

Tarehe hizi ni muhimu, na ninazitaja makusudi. Maana wapo wapuuzi wanaodai kuwa elimu ya msingi leo ni duni kuliko ilivyokuwa miaka ya 1970.

Kweli hapo katikati kulikuwa na matatizo, lakini mwenye akili ataona jinsi tulivyoshughulikia matatizo hayo kupitia MMEM. Matokeo ya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi tangu tuanzishe MMEM ni kama ifuatavyo: Mwaka 2002, wanafunzi waliofaulu walikuwa 27 tu kwa kila 100, au asilimia 27.4.

Mwaka 2003, waliofaulu waliongezeka hadi 40 kwa kila 100, au asilimia 40.1. Mwaka huu, 2004, waliofaulu walifikia karibu 49 kwa kila 100, au asilimia 48.6. Hakuna maelezo mengine ya mafanikio haya makubwa, kwa kipindi hiki kifupi, ila kwamba ni matokeo ya mpango mzuri, uliotekelezwa vizuri.

Tena kasi ya kufaulu wasichana imekuwa kubwa kuliko wavulana. Wakati ambapo ongezeko la kufaulu wavulana kutoka mwaka 2003 hadi 2004 ni asilimia 7.9, ongezeko la kufaulu wasichana ni asilimia 9.3.

Nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Elimu na Utamaduni, viongozi wenzake na watumishi wa wizara, na hasa walimu, wanafunzi na wazazi wote kwa kazi nzuri sana.

Naomba tuanze mwaka mpya kwa kuazimia kwenda mbele daima, kurudi nyuma mwiko. Na kamwe tusikubali kuyumbishwa na wachache wasioona jema, waliokosa shukrani na wasiofurahia mafanikio haya ya wazi ambayo ni mwanzo mzuri wa kuboresha elimu nchini.

Viwango hivi vya kufaulu vinaongeza umuhimu wa kupanua elimu ya sekondari. Kazi hiyo inaendelea kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES), na tayari mwaka unaoanza wa 2005 tutaongeza sana idadi ya wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza.

Hapa Dar es Salaam, kwa mfano, idadi ya vijana wetu watakaoanza kidato cha kwanza  mwaka 2005, kwenye shule za serikali, ni 4,143 ikilinganishwa na 2,885 tu mwaka 2004.

Hili ni ongezeko la asilimia 44 katika mwaka mmoja tu! Na bado wapo wachache ambao hawataki kuona na kukiri kuwa Serikali ipo makini kwenye jambo hili.

Itaendelea kesho

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi