loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Chanjo ni muhimu katika kuokoa maisha

CHANJO zimesaidia kuokoa maisha ya mamilioni ya watu duniani kote katika kipindi cha miaka 100 iliyopita.

Chanjo pia zimekuwa hakikisho la makuzi salama ya watoto na afya bora kwa watu wazima. Kabla ya uwepo wa chanjo, dunia ilikuwa si sehemu salama sana, na mamilioni ya watu walikuwa wakipoteza maisha kila mwaka kwa magonjwa ambayo sasa yanaweza kudhibitika.

Kwa mfano, chanjo zimewezesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na surua kwa asilimia 80 baina ya mwaka 2000 mpaka 2017, linabainisha Shirika la Afya Duniani (WHO).

Takribani watu milioni 2.6 walikuwa wakipoteza maisha kila mwaka kutokana na surua kabla ya chanjo ya kwanza ya ugonjwa huo kuanza kutumika kwenye miaka ya 1960.

Kwa hapa Tanzania chanjo imesaidia sana kupunguza gharama ambazo familia mbalimbali na Taifa kwa ujumla zingeingia katika kutibu maradhi yatokanayo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ambayo pia yana tabia ya kusambaa kwa kasi pale watu wanapikuwa hawajapata chajo.

Mratibu wa malariamkoa wa Pwani, Mhando Muya, anasema pale ambapo idadi kubwa ya watu wanapopokea chanjo, inasaidia kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na pia husaidia kuwalinda wale ambao hawana kinga ama hawawezi kupata chanjo.

Muya anasema matokeo ya usambaaji wa magonjwa ya surua na polio ni kielelezo kinachoonesha jamii bila kinga ipo kwenye hatari ya kupata maambukizi kutoka nchi jirani. Hivyo anasema, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inafanya kila iwezalo kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa wakati katika vituo vyote vinavyotoa huduma za chanjo nchini.

Muya anasema serikali kwa kushirikiana wa wadau mbalimbali imewezesha upatikanaji wa chanjo zote za kuzuia magonjwa yanayozuilika. Anasema mkakati wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kwa sasa ynalenga magonjwa ya kifua kikuu, dondakoo, kifaduro, polio, surua, rubella, pepopunda, homa ya ini, homa ya uti wa mgogo, kichomi, kuhara na saratani ya mlango wa kizazi.

Anasema kwa hapa nchini tumefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa ndui, dondakoo, kifaduro, polio na pepopunda na kwamba wodi za surua zimefungwa.

“Mafanikio haya makubwa yametokana na kufanikiwa kuwapatia chanjo zaidi ya asimilia 80 ya watoto walio na umri wa chini ya mwaka mmoja,” anasema Muya. Anasema kwa takwimu za mwaka 2018/2019, Tanzania imefikia kiwango cha uchanjaji cha asimilia 99, na hiyo ni hatua kubwa iliyofikiwa na Serikali katika kupambana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Kutokana na mafanikio hayo, kwa sasa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imeanza kukusanya na kutunza takwimu kwa kutumia mfumo wa vishikwambi (tablets).

Licha ya kiwango cha chanjo kuendelea kuwa juu, anasema bado kumekuwa na idadi ya watoto wasiokamilisha chanjo na wasiochanjwa katika baadhi ya maeneo na hivyo kusababisha uwezekano wa milipuko ya surua.

Anasema wizara imetoa huduma za chanjo kuwa kipaumbele cha kwanza katika afya, hivyo Serikali inafanya kila iwezalo kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa wakati katika vituo vyote vinavyotoa huduma za chanjo hapa nchini.

Muya anasema licha ya mafanikio haya makubwa, bado tunayo changamoto ya watoto ambao hawajapata au hawajakamilisha ratiba ya chanjo hasa mabinti kwa upande wa chanjo dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.

“Ni muhimu kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo zake kwa wakati ili kudhibiti milipuko ya magonjwa, hasa kwa kuzingatia kuwa kumekuwepo na milipuko ya ugonjwa wa polio nchi za jirani tunazopakana nazo,” anasema Muya.

Muya anasema ili mafanikio yaweze kufakiwa kwa kiwango kikubwa anawataka waandishi wa habari kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa huduma za chanjo kutokana na faida zake.

Naye Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dafrosa Lyimo, anasema baadhi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo husababisha ulemavu na kifo.

Dk Lyimo, anasema surua husababisha magonjwa ya nimonia, degedege, mtindio wa ubongo, utapiamlo, upofu na kifo wakati rubella husababisha ugonjwa wa moyo kwa watoto, uziwi, figo, mtindio wa ubongo, matundu kwenye moyo na madhara ya uti wa mgongo.

Pia ugonjwa wa polio anasema huleta ulemavu wa viungo na kifo, hivyo chanjo inabaki kuwa njia rahisi na sahihi ya kumlinda mtoto kiafya. Dk Lyimo pia anawaomba waandishi wa habari waliopata mafunzo kuhusu masuala ya chanjo kukanusha upotoshaji mbalimbali unaojitokeza katika jamii kuhusu chanjo.

Anashauri ni muhimu huduma za chanjo zitolewe sehemu za wazi, zenye hewa ya kutosha huku umbali wa mita moja toka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine ukizingatiwa.

Hatua hiyo anasema ni ili kupunguza athari za maambukizi ya corona (COVID-19). Licha ya mafanikio yaliyopatikana kwenye chanjo zingine, chanjo ya HPV (human papillomavirus) ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 imeelezwa kwamba bado kiwango cha uchanjaji kipo chini.

Ofisa Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk Furaha Kyesi, anasema saratani ya mlango wa kizazi ina athari kubwa kwa afya ya wanawake ulimwenguni kote. Hivyo anasema katika kukabili tatizo hilo serikali imeanzisha chanjo hiyo ambayo ni salama, haina madhara na inatolewa bila malipo katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya na mashuleni.

Anasema ni muhimu msichana aliyeanza kupatiwa chanjo hiyo akamilishe dozi mbili za chanjo ambapo dozi ya pili hupewa miezi sita baada ya kupata dozi ya kwanza.

Kwa upande wake mshauri mwandamizi mkuu na Meneja wa Mradi wa Programu ya Kukinga saratani ya mlango wa kizazi (HPV), Dk MaryRose Giattas, kutoka Shirika la Jhpiego, anasema ili kuweza kufikia malengo ya chanjo hiyo kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 ambao wengi wapo shuleni ni vyema zikaanzishwa klabu za HPV mashuleni.

Dk Giattas, anasema hatua hiyo inapaswa iende na mkakati wa kuwaelimisha na kushirikisha viongozi wa serikali wa ngazi za mitaa, vitongoji, vijiji, kata, wilaya na mikoa ili wafahamu faida ya chanjo kwa mtoto na msichana wenye umri wa miaka 14.

Anasema, ni muhimu kwa walimu na maofisa chanjo ngazi ya kituo kutoa elimu katika mikutano ya wazazi na walezi ili watambue faida ya chanjo kwa watoto wao katika kuwasiaidia kuwakinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika.

Naye Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Manispaa ya Morogoro, Rukia Chembe, anasema kwenye shule za sekondari bado elimu na uhamasishaji wa kutosha kuhusu faida ya chanjo hizi haujafikishwa.

Chemba anatolea mfano wa Manispaa hiyo kwamba ina shule za sekondari zaidi ya 50 lakini ni shule 10 tu ambazo wasichana wenye umri wa miaka 14 waliweza kupatiwa chanjo ya HPV na hata hivyo baadhi hawajakamilisha dozi ya pili.

Kaimu Ofisa Eimu Sekondari katika manispaa hiyo, anasema licha ya kuwepo manufaa, bado baadhi ya wanafunzi wa kike wenye umri wa miaka 14 ambao wengi wapo kidato cha kwanza na cha pili ni wagumu kukubali kutokana na kutaka kwanza wapate ridhaa ya wazazi wao.

WAKATI Rais John Magufuli ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Habari Nyingine