loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hongera Askofu Nzigilwa, waunganishe waumini wa Mpanda kiroho na kimwili

JIMBO Katoliki la Mpanda jana lilipata rasmi kiongozi wa kuliongoza baada ya Askofu Eusebius Nzigilwa kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo hilo baada ya kuteuliwa na Baba Mtakatifu Francis Mei 13, mwaka huu.

Askofu Nzigilwa nimemfahamu kwa muda mrefu wakati akiwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Sina wasiwasi na weledi, nidhamu na utayari wake wa kumtumikia Mungu katika wito aliyomuitia kutokana na falsafa yake ya “Unyenyekevu na Upendo”.

Bila shaka watu wa Dar es Salaam watakubaliana nami kwamba kwa upande wa Kanisa Katoliki, Askofu Nzigilwa akiwa jijini humo alitumika kuwaunganisha waumini wa imani tofauti, kwa kuhimiza umoja wa makanisa na kupitia Kamati ya Mahusiano ya Watu wa Dini mbalimbali, alilinda na kuwaongoza waumini aliyowasimamia kuheshimu imani nyingine.

Mara kadhaa mimemsikia katika mahubiri akihimiza amani, upendo na umoja wa kweli unaolinda na kujenga maisha yenye furaha kwa wote bila kujali tofauti za kiimani, kiitikadi na kikabila.

Jana alisimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo la Mpanda, baada ya jimbo hilo kukaa bila kiongozi kuanzia Desemba mwaka 2018 baada ya aliyekuwa askofu wa jimbo hilo, Gervas Nyaisonga kuteuliwa na Baba Mtakatifu kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya.

Nzigilwa ameaminiwa na Kanisa Ulimwenguni kuwa anaweza kuliwakilisha vyema katika utume wa kuwaongoza watu wa Mungu na kielelezo chema cha kanisa kwa kuunganisha waumini wa imani Katoliki na wananchi wengine katika kuimarisha amani, umoja na utulivu nchini.

Katika Hati ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francis iliyosomwa jana, Papa alieleza wazi kuwa moja ya sababu za kumkabidhi jimbo ni mwenendo mwema na utendaji kazi mzuri wa kitume, aliyouonesha tangu alipoteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Kama alivyosema Askofu wa Jimbo la Kigoma katika mahubiri yake jana kuwa uaskofu ni huduma na utumishi zaidi ya heshima, Nzigilwa akiwa na sifa zote hizi na uzoefu ndani yake wa utume huo, ni wazi hatofumbwa macho na heshima hiyo aliyopewa na kanisa na kujisahau kuwa ni mtumishi wa watu, bali atasimamia vyema falsafa yake ya unyenyekevu na upendo.

Natamani Askofu Nzigilwa awe sababu ya waumini wa Mpanda kuwa wamoja zaidi na si tu waumini, bali wananchi wa eneo hilo waone kwa vitendo maana ya Injili ya Upendo inayohubiriwa kila siku ndani ya Kanisa na aliyokuwa akiihubiri wakati wote alipokuwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa kujengwa kiroho na kimwili bila kujali tofauti zao za kiimani.

Umuhimu wa viongozi wa dini kwa taifa lolote unajulikana, na hii bila shaka ndio sababu ya Rais John Magufuli jana kumtumia salamu za pongezi Nzigilwa na pia Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera kumhakikishia askofu kuwa serikali itashirikiana na kanisa kuwaletea wananchi maendeleo.

Kama ambavyo Nzigilwa amekuwa akiomba maombi kila mara ili aweze kutimiza utume wake, wakati huu bila ni muhimu kwa kila mtu mwenye hofu ya Mungu kuwaombea viongozi wote wa kiimani, mapadre na mashehe, kwani dhamana walionayo si tu kulinda na kueneza imani zao, bali kuimarisha umoja, upendo na uzalendo ili maendeleo ya kweli yapatikane na kuinufaisha nchi nzima.

KAMPENI za uchaguzi kwa ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi