loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Askofu Nzigilwa apewa neno la hekima kudumu katika utume

ASKOFU mpya wa Jimbo Katoliki Mpanda, Eusebius Nzigilwa amekumbushwa kuwa uaskofu ni utumishi na si heshima hivyo aendelee kuwa mnyenyekevu.

Askofu Nzigilwa pia amekumbushwa kuwa amekabidhiwa waumini wa mijini na vijijini na anapaswa kuwafikia wote kuwapa huduma za kichungaji sawa. Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, Joseph Mlola, aliyasema hayo alipokuwa akihubiri katika ibada ya misa takatifu ya kumsimika Askofu Nzigilwa kuwa kiongozi wa kanisa hilo Jimbo la Mpanda.

Waumini jimboni humo wameombwa kumpokea Askofu Nzigilwa awe kiongozi wao mpya, wamuombee na kumpa nafasi ya kuwaongoza ili auishi vyema utume wake na kujenga uhusiano mwema kwa wote.

Papa Francis katika Hati yake ya Kitume kwa Kanisa la Tanzania kuhusu uteuzi wa Nzigilwa, amesema moja ya sababu za kumteua kusimamia jimbo hilo ni mwenendo mwema na utume mzuri wa kiaskofu aliouonesha.

Jimbo la Mpanda halikuwa na Askofu kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, baada ya Papa Francis kumteua aliyekuwa Askofu wa jimbo hilo, Gervas Nyaisonga, kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya Desemba 21, mwaka 2018.

Mei 13, mwaka huu Baba Mtakatifu Francis alimteua Askofu Nzigilwa awe Askofu wa Jimbo la Mpanda. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam na mwaka huu ametimiza miaka 25 ya upadre.

“Uaskofu wa kweli ni huduma na si heshima, ni utumishi. Sote tunaalikwa na tuna wajibu wa kuwa waombezi wake ili atekeleze wajibu huo muhimu aliokabidhiwa na Mungu” alisema Askofu Mlola.

“Mumpokee kwa moyo wa upendo Askofu mpya, mpeni nafasi kwa kumsikiliza na kuandamana naye katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji, mpeni nafasi ya kuwaongoza, mtamsaidia kuishi vyema zaidi wito wake katika jukumu la kiaskofu, kujenga uhusiano kwa wote,” alisema.

Alimweleza Askofu Nzigilwa kuwa waumini wa Mpanda wapo mijini na vijijini hivyo awatembelee wote kwa kuwa wote wanamuhitaji.

“Kusudia kufanya kama Kristo, kuwatembelea wa mijini na vijijini kwa kuwa wote wanakuhitaji, ukawaimarishe na kuwaleta pamoja chini ya mchungaji mmoja,” alisema Askofu Mlola na akauliza

“Najiuliza Wanampanda mmemtendea nini Mungu kuwapa mchungaji huyu mzoefu? Lakini si kwamba mmempa Mungu chochote bali ni kwa kuwa anawapenda,” alisema Askofu Mlola.

Awali wakati Nzigilwa akisimikwa, hati ya kitume ya Baba Mtakatifu Francis, ilisomwa Kilatini na ikatafsiriwa kwa Kiswahili ili kuthibitisha uteuzi wake. Katika hati hiyo, Papa Francis alimuelezea Askofu Nzigilwa kuwa ameonesha mwenendo mwema na amefanya utume mzuri wa Kiaskofu.

JAMII imehadharishwa dhidi ya tabia ya ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine