loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wizara yatimua mkandarasi mradi wa maji Nyang’hwale

KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Anthony Sanga( pichani) amesitisha mkataba na mkandarasi Kampuni ya PET Cooperation Ltd na Al Baruwani Investment Ltd kwa kuwa ameshindwa kukamilisha kwa wakati Mradi wa Maji wa Nyamtukuza wilayani Nyang’hwale mkoani Geita.

Msimamizi wa mradi huo, Meneja wa Wakala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Geita, Nicas Ligombi amesema utekelezaji wa wa mradi huo umefikia asilimia 65.

Alisema jana kuwa mradi ulianza kutekelezwa Januari 2014 na ulipangwa kukamilika ndani ya miezi sita, yaani mwezi Julai 2014.

Sanga alisema kuwa amechukua uamuzi wa kusitisha mkataba na mkandarasi huyo, baada ya kutembelea mradi huo Agosti Mosi mwaka huu, kuona utekelezaji wake na hakuridhishwa.

“Mkataba ulikuwa wa miezi sita lakini sasa imefika miaka sita na kama sasa ujenzi wake umefikia asilimia 65, kwa hesabu ya haraka inamaanisha kwamba tukimuachia mkandarasi aendelee tunahitaji miaka mingine mitatu yaani mwaka 2023 ndipo utakamilika, hili halikubaliki,” alisema.

Alisema Rais John Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015, aliahidi wananchi watapata maji.

“Mwaka 2015 wakati wa kampeni Rais aliahidi kufikisha maji hapa Karumwa makao makuu ya wilaya ya Nyang’hwale, haitakuwa sawa arudi tena kuomba kura hapa mwaka huu halafu akute ahadi yake aliyoitoa haijakamilishwa, hili sisi kama wizara hatuwezi kulikubali,” alisema Sanga.

Alisema mkandarasi hatapewa muda wa nyongeza, kukamilisha mradi huo. Aliagiza mradi huo sasa ukamilishwe na wataalamu wa ndani kwa mfumo wa force account. Alimuelekeza Mkurugenzi wa Ufundi Ruwasa, Deusdedit Magoma kusimamia maelekezo hayo.

Sanga alitoa siku mbili kwa Ruwasa Mkoa wa Geita na Mwanza na Mamlaka za Maji Geita (Geuwasa), Mwanza (Mwauwasa) na Mamlaka ya Maji Kahama Shinyanga (Kashwasa) kufanya maandalizi ya kuanza ukamilishwaji wa mradi.

“Siku mbili zinawatosha kufanya maandalizi na ikifika Jumatano (Agosti 5, 2020) timu ya wataalamu iwe imeripoti kwa Mkuu wa Wilaya tayari kuanza kazi na hakikisheni wataalamu wanakuwa hapa muda wote na sio kulala Geita na utekelezaji unapaswa kufanyika usiku na mchana hadi mradi utakapoanza kutoa maji,” alisema Sanga.

Alisema kuwa ifikapo Agosti 5, mwaka huu wizara hiyo itapeleka Sh milioni 100 na kwamba kabla ya mwezi huu kumalizika, fedha nyingine zitapelekwa. Sanga alisema kuwa kuna zaidi ya miradi 1,425 yenye changamoto inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, ukiwemo huo wa Nyamtukuza.

“Hatuwezi kuwabembeleza wakandarasi, miradi yote ya Wizara ya Maji ambayo inasuasua tunakwenda kuwapokonya na tutajenga kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani na pia wakandarasi hao hawatapewa tena kandarasi za miradi ya maji.

Serikali hii ya Awamu ya Tano inachohitaji ni kuona wananchi wanapata maji, na sio maneno,” alisema katibu mkuu huyo.

JAMII imehadharishwa dhidi ya tabia ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Geita

Post your comments

Habari Nyingine