loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali: Hatutaweza kumpunja Mtanzania biashara madini

SERIKALI imesema inatoa bei halali ya madini inayonunua kutoka kwa wachimbaji wadogo, na kwamba haiwezi kumpunja Mtanzania yeyote huku ikitoa onyo kwa watoroshaji madini nje ya nchi kuwa inatambua mbinu zote mpya zinazotumiwa hivyo hawatafanikiwa.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Madini, Dotto Biteko wakati wa tukio la kununua madini ya Tanzanite kutoka kwa mchimbaji mdogo, bilionea Saniniu Laizer ya uzito wa kilo 6.33 yenye thamani ya Sh bilioni 4.846.

Laizer alikabidhiwa hundi jana na tayari ameshalipa mrabaha wa Sh milioni 290.7, ada ya ukaguzi Sh milioni 48.46 na ada ya huduma kwa halmashauri ya Simanjiro ya Sh milioni 14.5.

Amesema serikali imemlipa bilionea Laizer fedha yake bila kumpangia isipokuwa tu imempangia kodi anayopaswa kulipa ambayo hata hivyo ameshailipa.

“Serikali haipo hapa kumpunja Mtanzania yeyote, tumelifanyia uthaminishaji jiwe hili la Tanzanite na wathamini watatu kufanya uthamini ili kuondoa minong’ono ya watu wengine wanaopenda kuchimba kwa mdomo, nataka kuwapa salamu yule mtanzania anayechimba kwa haki hataonewa na yeyote.

"Sisi watanzania tumeamua uchumi wa madini yetu yatunufaishe wenyewe, tumechoka kuwa madalali wa wageni kuchukua madini yetu yawanufaishe nchi zao, Rais (John Magufuli) amefanya kazi kubwa kuthamini wachimbaji, zawadi pekee mnayoweza kumpa rais ni kulipa kodi kwa ukamilifu, muachane na biashara ya kutorosha madini, anayedhani anaweza kutorosha niwahakikishieni hatatoboa, hata mbinu zote za kutorosha ambazo ni mpya hawakuwahi kuwa nazo, tumeshazijua, unapopumua hivi mjue na sisi tupo pembeni.

Amesema wachimbaji hawana sababu ya kuficha madini, bali wajiunge na mchakato wa uwazi wa biashara ya madini unaofanywa na serikali.

“Mnapokuwa wachimbaji wawili watatu muwe na uhakika mmoja wapo atatupa taarifa lolote linapotokea. Lete madini yako uza kwa uwazi, katanue mwenyewe unapotaka, serikali haitakupangia cha kutumia,"amesema

Kwa upande wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo amesema ukuta huo wa Mirerani licha ya kulindwa vizuri na kuchangia kudhibiti utoroshaji wa madini bado kunahitajika ufungwe vifaa vya kisasa vya ulinzi vya kitaalamu zaidi.

“Wizara ya Madini iangalie kwa umakini ili kuimarisha ulinzi, unaweza kulinda mlango, ukuta lakini mtu akapitisha madini kwenye viatu na kumvua akaona kama anadhalilishwa lakini vifaa vikiwepo unamwambia vua viatu tuachie madini yetu,”amesema.

foto
Mwandishi: Maulid Ahmed

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi