loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Jumuiya ya Afrika Mashariki haitavunjika

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imewatoa hofu wananchi wa jumuiya hiyo kuwa migogoro inayotokea baina ya nchi wanachama, haiwezi kusababisha kuvunjika kama inavyoelekezwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa na diplomasia.

Jumuiya hiyo imesema hayo siku chache baada ya kutokea sintofahamu, kufuatia Kenya kufungua anga yake kwa ajili ya ndege zake kwenda nchi mbalimbali na kuzuia baadhi ndege kutotua nchini humo ikiwamo Tanzania.

Baada ya Kenya kuchukua hatua hiyo, Tanzania ambayo tayari ilishatoa kibali cha ndege za Kenya kuingia nchini ilitoa tangazo la kusitisha ndege za nchi hiyo kuingia mpaka itakapotolewa taarifa nyingine.

Akizungumza na Habari- Leo jana, Naibu Katibu Mkuu wa EAC, Steven Mlote alisema hawajapata taarifa rasmi juu ya suala hilo, hivyo hatalizungumzia kwa undani, lakini alieleza kuwa anaamini haiwezi kuwa sababu ya kuvunjika kwa jumuiya hiyo.

Alisema leo Jumanne kutakuwa na kikao cha mawaziri wanaoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo kama kuna tatizo, wakiona kuna sababu, watajadili na kutafuta ufumbuzi.

“Katika kikao hicho tutaangalia kama kuna matatizo, kila mmoja ataeleza tatizo lililopo, hivyo EAC tutaona kama kuna hatua za kuchukua, lakini kama lilivyo kwa sasa siyo suala kubwa linaloweza kusababisha tatizo kubwa ndani ya jumuiya,” alisema.

Mlote alisema kuna masuala mengine hayahusiani na Jumuiya ya Afrika Mashariki, bali yanahusu nchi na nchi, hivyo ikionekana ni suala la nchi wataachiwa wahusika wakatafute ufumbuzi baina yao.

Alipoulizwa iwapo changamoto hiyo inatishia uhai wa jumuiya hiyo, alisema anaamini haiwezi kufikia huko na kuongeza kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo aliloliona mtandaoni mpaka atakapopata taarifa rasmi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutoka Tanzania, Dk Abdullah Makame alisema kwa Kenya kuzuia anga yake, hakuna afya kwa jumuiya kwani lengo la kuwa na mtangamano ni kuondoa mipaka baina ya nchi zote wanachama.

Dk Makame alitoa wito kwa mawaziri katika nchi hizo, kukutana mapema kujadiliana na kufikia muafaka. Alisema kuwa suala hilo likikaa kwa muda mrefu, litakuwa na athari kubwa za kiuchumi kwa pande zote.

“Hili siyo suala la marais kukaa bali ni mawaziri kwa kuwashirikisha wataalamu katika nyanja husika, lakini sidhani kama litakaa kwa muda mrefu kwani ikichukua muda mrefu inaweza kuathiri na maeneo mengine muhimu,” alisema.

Alisema jambo kama hilo siyo jipya kutokea kwa Tanzania na Kenya, lakini ni vema pande hizo mbili zikakutana na kujadiliana na kupata ufumbuzi wa haraka.

Baada ya kutokea kwa mzozo huo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kidplomasia, walieleza kuwa kitendo cha nchi moja kuzuia nyingine kuingia nchini mwake kinaweza kusababisha kuvunjika kwa EAC.

Wachambuzi hao walisema mizozo kama hiyo, ndiyo iliyosababisha hapo awali jumuiya hiyo kuvunjika mwaka 1977. Waliitaka sekretarieti ya EAC kuingilia kati wakati suala hilo liwa bado halijaanza kuleta madhara.

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi