loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bilionea akanusha kupunjwa na serikali

MCHIMBAJI wa madini, bilionea Saniniu Laizer amekanusha taarifa kuwa serikali inamdhulumu inaponunua madini yake na amesema wanaosema hayo wamepotoka.

Laizer alisema hayo jana Mirerani wilayani Simanjiro, Manyara kwenye tukio la kuiuzia serikali madini ya tanzanite yenye kilogramu 6.33 zenye thamani ya Sh bilioni 4.846 Alisema kuwa wachimbaji wapo vizuri na serikali na kama serikali itauziwa madini, nchi itafikia malengo na kwamba viongozi wapo makini na pia Rais John Magufuli anawapenda wanyonge.

“Sisi tumeridhika na bei ya serikali kwa sababu hakuna longolongo na hakuna dhuluma yoyote…Rais wetu anafanya vizuri sana kutuletea viongozi kama hawa”alisema Laizer.

Katika tukio hilo, Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema kuwa serikali inatoa bei halali ya madini kwa wachimbaji wadogo, haipo kumpunja Mtanzania yeyote na ameonya wanaoyatorosha.

Alisema serikali imemlipa Laizer fedha yake bila kumpangia matumizi. “Serikali haipo hapa kumpunja Mtanzania yeyote, tumelifanyia uthaminishaji jiwe hili la tanzanite na wathamini watatu kufanya uthamini ili kuondoa minong’ono ya watu wengine wanaopenda kuchimba kwa mdomo,”alisema Biteko.

Aliwafahamisha Watanzania wanaochimba kwa haki kuwa hawataonewa na yeyote, na kwamba Watanzania wameamua madini yawanufaishe wenyewe kwa kuwa wamechoka kuwa madalali wa wageni wanaochukua madini yao.

“Rais(John Magufuli) amefanya kazi kubwa kuthamini wachimbaji, zawadi pekee mnayoweza kumpa Rais ni kulipa kodi kwa ukamilifu, muachane na biashara ya kutorosha madini, anayedhani anaweza kutorosha niwahakikishieni hatatoboa, hata mbinu zote za kutorosha ambazo ni mpya nazo tumeshazijua, unapopumua hivi ujue na sisi tupo pembeni”alisema Biteko.

Alisema wachimbaji hawana sababu ya kuficha madini, wajiunge na mchakato wa uwazi wa biashara ya madini unaofanywa na serikali. “Mnapokuwa wachimbaji wawili watatu muwe na uhakika mmoja wapo atatupa taarifa lolote linapotokea.

Lete madini yako uza kwa uwazi, katanue mwenyewe unapotaka, serikali haitakupangia cha kutumia. Serikali itakupangia kwenye kodi zake tu, mzee Laizer ni mwaminifu, mwema sana, mwingine angefuata propaganda za maneno ya wengine, ya wachimbia mdomo, yeye hakufanya hivyo”alisema.

Alisema kuwa baada ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanza kulinda ukuta wa Mirerani, hali ni shwari na kwamba utoroshaji wa hovyohovyo haupo. Ukuta huo umejengwa kwenye mzingo wa kilometa 28.5 kuzunguka machimbo ya tanzanite Mirerani.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema tangu ukuta wa Mererani ujengwe mapato yatokanayo na Tanzanite yameongeka.

Alitoa mfano kuwa mwaka 2018 kabla kujengwa ukuta huo, mapato yalikuwa Sh milioni 238 na baada ya kujengwa ukuta huo yameongezeka mwaka huo 2018 kuwa Sh bilioni 1.4 na kwa mwaka jana mapato yamefikia Sh bilioni 1.998.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo alisema ukuta huo wa Mirerani, licha ya kulindwa vizuri na kuchangia kudhibiti utoroshaji wa madini, bado panahitajika vifaa vya kisasa vya ulinzi vya kitaalamu zaidi.

“Wizara ya Madini iangalie kwa umakini ili kuimarisha ulinzi, unaweza kulinda mlango, ukuta lakini mtu akapitisha madini kwenye viatu na kumvua akaona kama anadhalilishwa, lakini vifaa vikiwepo unamwambia vua viatu tuachie madini yetu,”alisema.

Aliishukuru Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuipa JWTZ Sh milioni 100 za kujenga nyumba za walinzi wa ukuta huo wa Mirerani.

Akizungumzia madini ya Laizer, Biteko alisema Juni 29, 2020 serikali ilipata taarifa kuwa kwenye mgodi wa Laizer kuna kipande cha kilo 6.33 kilichopatikana wakati wa usafishaji eneo la uzalishaji wa awali wa Juni 17 mwaka huu.

Madini hayo yalipatikana wakati wa kuondoa miamba, iliyokaribia kuanguka ili kuendelea na kazi ya kuchoronga. Hii ni mara ya pili kwa bilionea Laizer kuiuzia serikali madini ya tanzanite.

Kwa mara ya kwanza Juni 17 mgodi huo wa Laizer uliopo Kitalu C, ulifanya uzalishaji wa kilo 32.872 za tanzanite katika umbali wa mita 1800 chini ya ardhi. Thamani ya madini hayo ni Sh bilioni 8.458, malipo ya mrabaha wa ada ya ukaguzi yaliyopokelewa ni Sh mil 507. 50.

Kulikuwa na vipande vikubwa visivyokuwa vya kawaida ambayvo havijawahi kupatikana Mirerani. Kipande cha kwanza kilikuwa na uzito wa kilo 9.27 chenye thamani ya Sh bilioni 4.368, mrabaha wa serikali alilipa Sh milioni 262.1, ada ya ukaguzi Sh milioni 43. 68 na ushuru wa huduma kwa halmashauri Sh milioni 13.

Kipande cha pili kilichopatikana kilikuwa na uzito wa kilo 5.103 chenye thamani ya Sh bilioni 3.375, mrabaha wa serikali ulilipwa Sh milioni 202.53, ada ya ukaguzi ililipwa Sh milioni 33.7 na Sh milioni 10 ada ya huduma kwa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.

Wakati huohuo, Serikali imekataa kuuza tanzanite ya mabilioni na inajipanga kuwa na utalii wa madini yanayochimbwa nchini na tayari imeanza mkakati kutekeleza hilo, ikiwa ni pamoja na kuyanunua kwa wachimbaji wadogo.

Waziri wa Madini, Biteko alisema kuwa Wizara ya Madini na wadau wengine, watakaa kuona namna madini yanayochimbwa nchini, yatakavyotumika kwa utalii ili hata watu kutoka nje ya nchi, waje kutalii na Watanzania wasiende huko kuona madini ambayo yalitoka Tanzania.

“Nimekuwa napata simu nyingi zingine za mabalozi wetu wanasema wamepata wanunuzi wa madini haya, nimewajibu hapana, Rais (John Magufuli) ameshasema fedha ipo tutanunua wenyewe.

Mwingine jana nimepata simu ya Mthailand na Kiingereza chake kigumu cha Kithailand, anasema ana pesa za kununua kilo hizi sita kwa bei yoyote, nikasema tutanunua wenyewe “alisema Biteko kwenye tukio hilo la serikali kununua tanzanite yenye kilogramu 6.33 kutoka kwa bilionea Laizer.

“Lazima tuwe na jeuri kwenye mali yetu, acha wao waje kuangalia mawe yetu kuliko sisi tunapanda ndege masaa mengi kwenda kuangalia jiwe letu wenyewe.

Hatuwezi kufanya biashara ya madini yetu kuwapelekea halafu kesho tunapanda ndege kwenda kuangalia madini yaliyotoka kwetu, Rais (Magufuli) amesema hilo hapana, tuyafanye wenyewe na tuanzishe utalii wa madini hapa kwetu” alisema Waziri Biteko.

“Tunatamani Tanzania iwe hub (kitovu) ya biashara ya madini Afrika na inawezekana, wote wanaofanya biashara ya dhahabu inafanyika Dubai au Geneva na ukienda huko hukuti shimo la dhahabu wala almasi.

Ubelgiji wao ndo wenye dhahabu nyingi na almasi nyingi. Tutafanya dhambi gani sisi tukifanya biashara hiyo?”alihoji. Laizer alikabidhiwa hundi jana na tayari ameshalipa mrabaha wa Sh milioni 290.7, ada ya ukaguzi Sh milioni 48.46 na ada ya huduma kwa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro ya Sh milioni 14.5.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alisema “Kuna nchi (hakuitaja) ina jiwe la tanzanite la kilo tatu, watu wanalipa fedha kwenda kuliangalia jiwe lililotoka Tanzania. Sasa tutapiga kelele dunia nzima waje kuangalia Tanzania kubwa zaidi hapa, sisi kinara duniani. Serikali ya Awamu ya Tano ni ya wachimbaji wadogo kutajirika”.

foto
Mwandishi: Maulid Ahmed

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi