loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waziri amwaga machozi

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo (pichani) amemwaga machozi jijini Dodoma, akikumbuka jinsi wananchi walivyokuwa wakipata adha na kupoteza maisha kutokana na ukosefu wa huduma za afya.

Jafo alimwaga machozi jana wakati akizungumzia mafanikio ya miaka mitano ya maboresho ya huduma ya afya ya msingi yaliyowezeshwa na kusimamiwa na serikali.

Jafo alikuwa akizungumza katika siku ya kwanza ya maadhimisho ya ‘Siku ya Tamisemi’.

Alisema wananchi wengi walikuwa wakipoteza maisha kwa kukosa huduma za afya, lakini katika miaka mitano ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli sekta hiyo imepewa kipaumbele ili kuondoa adha kwa wananchi.

“Kuna watu wenye uwezo hawafahamu kwamba Watanzania walikuwa wanateseka, walikosa kupata huduma za afya, na wanasafiri zaidi ya kilometa 140 kufuata huduma, kina mama wanapata matatizo ya fistula baada ya kupata uchungu kwa muda mrefu na vituo vipo mbali”alisema Jafo.

Hii ni mara ya pili kwa Jafo kutoa machozi hadharani akiwa waziri. Mara ya kwanza alifanya hivyo alipokagua ujenzi wa daraja linalounganisha vijiji vya Mbuchi na Mbwela mkoani Pwani, ambalo kukamilika kwake kutarahisisha wananchi upatikanaji huduma zikiwemo za afya. Jafo alisema jana kuwa huenda kuna Watanzania wanaoishi mijini wasiofahamu kuwa taifa limepoteza watu wengi kwa kukosa huduma za afya.

“Nimetembea nchi hii kuna watu walishakata tamaa, wapo kwenye mazingira magumu, fikiria mtu anayeishi Kijiji cha Mbwela kule Kibiti, ambapo kutoka Kibiti hadi kufika kupata huduma za afya ni kazi, nenda kwa Watanzania wa Wampembe iliyoko wilayani Nkasi mkoani Rukwa, hadi kufika Namanyere kufuata huduma ni watu wangapi tumewapoteza maisha katika mazingira hayo?”aliuliza Jafo.

“Kuna eneo linaitwa Mwilepwa hata gari na pikipiki kufika ni tabu, lakini Rais Magufuli alipotoa zaidi ya shilingi bilioni 500, ambapo kati ya hizo zaidi ya shilingi bilioni 300 zilielekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu zimekwenda kuondoa adha kwa wananchi kama hawa,”alisema.

Jafo alisema wakati Rais Magufuli anaingia madarakani mwaka 2015, kulikuwa na vituo 115 tu ambavyo vilikuwa vina uwezo wa kutoa huduma ya upasuaji.

Kwa sasa vituo 487 vimekamilika. Aidha, alisema tangu nchi ilipopata Uhuru mwaka 1961 hadi Rais Magufuli anaingia madarakani, kulikuwa na hospitali za wilaya 77 kati ya halmashauri 185.

“Mpaka sasa kwa awamu ya kwanza hospitali 67 zimekamilika, zikaongezwa zingine na sasa jumla ya hospitali 99 zinajengwa, hizo za kwanza zimeanza kutoa huduma na hizo zingine zipo hatua mbalimbali ya ujenzi, tuna kila sababu ya kumshukuru Rais,”alisema.

Jafo alisema pia zaidi ya zahanati 1,198 zimejengwa kwa kipindi cha miaka mitano huku akina mama wajawazito waliojifungua katika vituo hivyo vipya ni 219,764 na waliopata huduma ya upasuaji ni 18,826.

“Wagonjwa wengine wakiwemo kina baba zaidi ya 6,000 wamefanyiwa upasuaji wa kawaida kwenye vituo hivyo, na kina baba wengine wametengeneza familia zao katika vituo hivi, wazee zaidi ya 100,000 walipata huduma.

“Niwashukuru wataalamu wangu kwa kuwa wamekuwa ni injini ya kuhakikisha mambo yanasonga katika sekta ya afya, idara hii ilikuwa mfu, lakini Rais ameibeba idara hii na sasa inafanya kazi,”alisema Waziri Jafo.

Awali, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Grace Maghembe, alisema kuna mikoa mitano ilikuwa haina hospitali za rufaa za mikoa, lakini kwa sasa zimejengwa.

Aidha, alisema uboreshaji wa huduma za afya zikiwemo za kibingwa nchini, umechangia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi.

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia afya katika ofisi hiyo, Dk Dorothy Gwajima alisema kuwa uwepo wa miundombinu hiyo uende sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wananchi ili kuwavutia wengi zaidi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa (CHF).

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Dodoma

1 Comments

  • avatar
    KASIAN CHANG'A
    04/08/2020

    Saafi sana

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi