loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ajira nyingine 12,000 za walimu zaja

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amebainisha kuwa serikali inaendelea na taratibu ili kuajiri walimu 12,000 watakaofundisha shule za msingi na sekondari.

Aidha amesema serikali imeweka mikakati kuhakikisha shule zote za sekondari, zinakuwa na maabara za sayansi na itanunua magari kwa ajili ya maofisa elimu wa wilaya zote nchini.

Serikali tayari imenunua magari 30 kwa ajili ya maofisa elimu wa mikoa yote. Jafo alielezea hayo jana jijini Dodoma alipokuwa akieleza mafaniko ya miaka mitano ya serikali kwa upande wa sekta ya elimu wakati wa siku ya pili ya maadhimisho ya Siku ya Tamisemi.

Alisema kwa kipindi cha miaka mitano, walimu zaidi ya 18,000 wameajiriwa na kupelekwa shule za msingi na sekondari.

“Nafahamu bado kuna changamoto ndio maana Rais alitoa maelekezo ajira za walimu zingine zitolewe na ametoa maelekezo ya ajira zaidi ya 12,000, taratibu zinaenda vizuri na zitakapokamilika mtasikia tunaongeza ajira kwa shule za msingi na sekondari.” alisema Jafo.

Alisema katika miaka mitano iliyopita, Sh trilioni 1.09 zimetolewa kwa ajili ya elimu bila malipo ili kuwawezesha watoto wa masikini wapate elimu. Jafo alisema kati ya hizo, fedha zaidi ya Sh bilioni 502 zimetolewa kwa jili ya elimu ya shule za msingi na Sh bilioni 593.9 zimeenda sekondari.

“Mwaka 2016 watoto wengi walifurika kwenye shule zetu wakati zikiwa zimekadiria watoto 200 hadi 400, zingine ziliweza kusajili hadi wanafunzi 1,000, kwa mfano shule za Nyakanazi na Majimatatu watoto wengine walisajiliwa wakiwa na miaka 10 kutokana na miaka mitatu nyuma walikosa fursa hiyo,”alisema.

Kwa mujibu wa Jafo, zaidi ya Sh bilioni 501 zimetolewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu ikiwemo ujenzi wa mabweni, nyumba za walimu, ofisi. Jafo alisema hadi kufikia mwezi Juni 2020, ujenzi wa shule za msingi mpya 905 ulikuwa umekamilika hivyo kuongeza idadi ya shule za msingi kutoka 16,899 mwaka 2015 hadi 17,804 mwaka 2020.

Alisema kuwa pia vyumba vya madarasa 17,215 vimejengwa na kuongezeka kutoka vyumba 108,504 mwaka 2016 hadi 125,719 mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 13.7. Jafo alisema kuwa ujenzi wa vyumba 3,049 vya madarasa, unaendelea na ukikamilika madarasa kwenye shule za msingi yataongezeka hadi 128,768.

Alisema kuwa kazi iliyofanywa na serikali imepunguza uhaba wa madawati kutoka madawati 3,024,311 mwaka 2015 hadi kufikia 8,095,207 sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 200.

Jafo pia alisema kuwa serikali imejenga shule mpya za sekondari 228 hivyo kuongezeka kutoka shule 4,708 mwaka 2016 hadi 5,330 mwaka 2020. Alisema kuwa serikali pia imejenga vyumba 227 vya maabara za masomo ya sayansi kwa gharama ya Sh bilioni 2.63.

Katibu Mkuu wa Tamisemi, Joseph Nyamuhanga alisema kuwa uwekezaji na maboresho yaliyofanyika katika sekta ya elimu kwa shule za msingi na sekondari, umeongeza kiwango cha ufaulu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kutoka asilimia 67.84 mwaka 2015 hadi asilimia 81.50 mwaka 2019.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi