loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Msajili aionya Chadema kuchezea Wimbo wa Taifa

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amekionya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kisithubutu kuongeza aya katika Wimbo wa Taifa, kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na ni kuunajisi wimbo huo.

Ameviasa vyama vingine vya siasa visijiingize kwenye mambo ya uvunjifu wa sheria na amevitaka visilazimishe vyombo vya dola, kuchukua hatua na kusema wanaonewa. Jaji Mutungi (pichani) alitoa onyo hilo jana, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya Chadema katika mikutano yake inayoendelea jijini Dar es Salaam, kueleza kusudio la kutaka kuongeza aya ya tatu katika Wimbo wa Taifa.

“Vyama vyote vya siasa kwa mujibu wa sheria vinatakiwa kujiendesha kwa kuzingatia Katiba ya Tanzania, Katiba ya Zanzibar na sheria zote za nchi. Sheria ya Vyama inamtaka Msajili kuhakikisha vyama vinazingatia sheria zote na Katiba,” alisema na kuongeza: “Jambo la kuchukua Wimbo wa Taifa na kuongeza aya ya tatu si jema. Sikutegemea chama cha siasa kikongwe namna ile kifanye uvunjifu wa sheria kwa makusudi tukae kimya”.

Jaji Mutungi alikumbusha kuwa wakati Rais John Magufuli alipofungua jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivi karibuni, aliwaeleza wanasiasa wasivichokoze vyombo vya dola, na wakifanya hivyo vitatekeleza wajibu wake, hivyo hategemei chama chochote cha siasa kuvichokoza vyombo vya usalama.

“Tupo kwenye maandalizi ya kujiandaa na uchaguzi mkuu, tunatarajia kwamba vyama vya siasa vitakuwa wakala wa amani kuelekea kwenye uchaguzi. Hakuna mtu wala taasisi iliyo juu ya sheria. Sheria ya vyama inavitaka vyama vya siasa kuzingatia sheria za nchi. Hiki kilichofanyika ni kunajisi Wimbo wa Taifa,” alisema.

Jaji Mutungi alisema kuwa ameanza kwa kutoa onyo badala ya kuwaandikia barua ili wajirekebishe, lakini alisema kuna mamlaka inahusika ambayo ni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo anaamini italifanyia kazi suala hilo kwa undani zaidi.

“Nawaonya Chadema wakati wanaendelea na mkutano waheshimu sheria za nchi. Nichukue fursa hii kuviasa vyama vingine vya siasa visijiingize kwenye mambo ya uvunjifu wa sheria. Kama tunataka kweli kuenzi amani tulionayo na taratibu zetu, tuheshimu sheria,” alisema Jaji Mutungi.

Alisema kuwa NEC inajitahidi kushirikisha wadau katika mchakato wa uchaguzi ili kuwe na uchaguzi wa amani, huru na haki. Jaji Mutungi alisisitiza vyama viheshimu sheria za nchi vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.

“Awali nilisema kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi, sheria nyingine hazijaenda likizo”alisema Jaji Mutungi. Alitoa mwito kwa Watanzania waangalie mienendo ya vyama vya siasa na wasikubali kuingizwa kwenye mkumbo wa kushiriki kuvunja sheria.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi