loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali yaokoa tril 11.4/- mahakamani

SERIKALI imesema imeokoa zaidi ya Sh trilioni 11.4 kwa miaka miwili kutokana na uendeshaji madhubuti wa mashauri ndani na nje ya nchi.

Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akitoa ripoti kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Mwigulu Nchemba.

Alisema kuwa miongoni mwa fedha zilizookolewa, zinatokana na kushinda kesi mbalimbali ikiwemo ukamataji wa ndege za Kampuni ya Ndege nchini (ATCL), kesi zilizofunguliwa Afrika Kusini na Canada.

Alisema endapo wasingekuwa madhubuti kusimamia na uendeshaji wa kesi, fedha hizo zingelipwa kwa watu wasiostahili hivyo kusababisha hasara kwa taifa. Malata alisema ingawa ofisi hiyo imeanzishwa miaka miwili tu iliyopita, serikali imehakikisha inashinda kesi zote zenye maslahi ya umma.

“Tumekuwa tukisimamia mashauri yote ya madai na usuluhishi ndani na nje ya nchi kwenye mahakama zote na mabaraza zinazohusu serikali kuu, serikali za mitaa, kampuni binafsi, taasisi na mashirika ya umma,” alisema.

Malata alisema kuwa serikali ilikuwa inatumia fedha nyingi kulipa mawakili wa kujitegemea, waiwakilishe kwenye kesi nje ya nchi, na kwamba wapo baadhi walikuwa si waaminifu hivyo walisababisha serikali ishindwe.

Alisema kuwa katika bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2018/19, walipatiwa zaidi ya Sh bilioni 7.2 na kati ya hizo walitumia Sh bilioni 2.2 kuendesha mashauri nje ya nchi. Kwa mujibu wa Malata wamefanikiwa kusajili mashauri kielektroniki kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi na kuendesha mashauri kwa njia ya video.

Alitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa watumishi wakiwemo wataalamu wa kuendesha mashauri ya usuluhishi ili kupambana na mawakili wa nje ya nchi. Changamoto nyingine ni ukosefu wa ofisi katika mikoa yenye Mahakama Kuu na magari.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Nchemba alionya mawakili wa serikali na taasisi za umma, wanaotengeneza mazingira ya kushindwa kesi zenye maslahi ya umma. Alisema kwamba wanaofanya hivyo, watahesabika ni wahujumu uchumi.

Dk Nchemba alisema maslahi ya Watanzania, lazima yalindwe na kusiwe na taasisi au wakili ambaye kwa makusudi anasababisha serikali ishindwe kesi kutokana na kuahidiwa kiasi fulani cha fedha.

“Vita ya kiuchumi inachezwa kisheria hivyo ni lazima tuhakikishe tunashinda kwa kulinda maslahi ya Watanzania na wale waliozoea kutumia mbinu ovu tusiruhusu kuendelea nao…kwa sababu haiwezekani tushindwe kesi kwa sababu ambazo tunaziita ni technical (za kiufundi) ambazo tungeweza kuziepuka.”alisema.

Alisema wapo mawakili wa serikali ambao huahidiwa fedha endapo watasababisha serikali ishindwe kwenye mashauri. Alionya kuwa hilo halitakubalika.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi