loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Fomu wagombea urais kuanza kutolewa leo

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo inaanza kutoa fomu za uteuzi kwa wagombea urais na Makamu wa Rais wa Tanzania, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

Ratiba iliyotolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage iliwataka wanachama wa vyama vya siasa waliopitishwa kugombea urais, wafike Njedengwa jijini Dodoma kuchukua fomu hizo. NEC itatoa fomu hizo kuanzia leo hadi Agosti 25 mwaka huu.

“Tume inawatangazia kuwa fomu kwa ajili ya uteuzi wa wagombea wa kiti cha urais zitaanza kutolewa leo, Agosti 5, mwaka huu,” alisema Kaijage.

Kaijage alisema kuwa watu wenye sifa ya kugombea nafasi ya kiti cha urais, ambao watakuwa wameteuliwa na vyama vyao vya siasa vyenye usajili wa kudumu, wajitokeze katika kipindi hiki ili kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo.

Vyama kadhaa vya siasa tayari vimepitisha wagombea urais, kikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakachowakilishwa na Rais John Magufuli. Tundu Lissu amepitishwa kuwania nafasi hiyo kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Shibuda amepitishwa kugombea kupitia chama cha ADATadea, Profesa Ibrahim Lipumba atawania kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) na mgombea wa ACT Wazalendo anatarajiwa kufahamika leo.

Kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu zitaanza Agosti 26 mwaka huu na zitaendelea hadi Oktoba 27 mwaka huu. Watanzania wanatarajiwa kupiga kura Jumatano, Oktoba 28, mwaka huu. Rais John Magufuli ametangaza kuwa siku hiyo itakuwa ya mapumziko.

Tanzania kuna vyama 19 vyenye usajili wa kudumu. Vyama viwili kupitia wenyeviti wao Augustino Mrema wa TLP na John Cheyo wa UDP, walisema havitasimamisha wagombea wa nafasi ya urais kwa kuwa watamuunga mkono mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM.

Vyama vingine vyenye usajili wa kudumu ni Alliance for Democratic Change (ADC), Demokrasia-Makini, Democratic Party (DP), Sauti ya Umma (SAU), Alliance for African Farmers Party (AAFP) na Chama cha Kijamii (CCK).

Vingine ni National Reconstruction Alliance (NRA), United People’s Democratic Party (UDPD), National League for Democracy (NLD), Union for Multiparty Democracy (UMD) na NCCR-Mageuzi.

Katika uchaguzi wa 2015, vyama vinane vyenye usajili wa kudumu vilikuwa na wagombea katika nafasi ya urais.

Wengine waliogombea alikuwa Edward Lowassa wa Chadema, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Fahamy Dovutwa wa UPDP, Hashim Rungwe wa Chauma, Janken Kasambala wa NRA, Machmillan Lyimo wa TLP na Chifu Lutalosa Yembe wa ADC.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi