loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bil 4.8/- zanufaisha kaya 5,922 Kilwa

MPANGO wa Kunusuru Kaya Maskini chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umetumia zaidi Sh bilioni 4.8 na kuzinufaisha kaya 5,922 za Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.

Takwimu hizo ni za kipindi cha miaka saba.

Mratibu wa Tasaf katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Stelah Omari alibainisha hayo katika semina ya siku moja kwa wakuu wa idara na vitengo iliyolenga kuwajengea uelewa juu ya miradi inayofadhiliwa na mpango huo na kutekelezwa katika vijiji 58 vya kata 23 za wilaya hiyo.

Alisema tathmini ya wilaya hiyo inaonesha kuwa katika kipindi cha miaka saba kuanzia mwaka 2013 hadi 2019, zaidi ya kaya 700 zimeondoka katika mstari wa kaya masikini zaidi na kuweza kujitegemea kutokana na kuwezeshwa na mpango huo.

Mwaka 2013 kulikuwa na kaya 5,922 zenye uhitaji, lakini sasa zimebaki kaya 5,205 zinazoendelea kuhudumiwa na mpango huu ambapo Sh 4,882,066,790 zimetolewa,alisema.

Kwa mujibu wa Stelah, kupungua kwa idadi ya wanufaika kunatokana na wengi wa wanufaika waliokuwa wakihudumiwa na mpango huo awali, kufanya kazi kwa bidii kuzalisha na kuweka akiba hadi kujikomboa na kutoka kwenye mstari wa kaya masikini.

Kiongozi wa timu ya Uhakiki wa Kaya Masikini wa Tasaf, Yassin Mkwepu, alisema sasa taarifa za wanufaika zitahifadhiwa katika mfumo wa kielektroniki ilikuwa na takwimu sahihi zaidi zitakazosaidia kuwezesha kaya za walengwa kutumia fursa za kuongeza kipato na huduma za jamii kuziondoa kwenye lindi la umasikini.

Katika semina hiyo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf na kiongozi wa timu ya Tasaf kitaifa, Andrew Kibona, aliwataka wakuu wa idara na vitengo wilayani hapo kushirikiana na Mratibu wa Tasaf kiwilaya ili kufikia malengo ya kupunguza umasikini.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Godfrey Jafari, aliihakikishia Tasaf aliwahimiza wakuu wa idara wote kuwa sehemu ya mpango huo ili kuondoa kasoro zinazojitokeza. 

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Kilwa

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi