loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

CCM yakabidhi vijana, wazazi, UWT mtambo wa ushindi

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ali amesema chama hicho kimewasha mtambo wa ushindi jana na kimejipanga kuhakikisha kinashinda Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.

Dk Bashiru alisema jana katika viwanja wa Makao Makuu ya CCM, (White House), jijini Dodoma kuwa, CCM Magufuli apeperushe bendera ya chama hicho kutokana na rekodi ya zaidi ya miaka 20 ndani ya Serikali.

Alisema baada ya kumaliza majaribio na kuwasha mtambo huo amekabidhi majukumu kwa jumuiya za chama kuhakikisha zinaendesha mitambo hiyo ili CCM ipate ushindi.

Dk Bashiru alisema vijana watafanya kazi ya kutafuta kura, kuzilinda kura zisiibwe sanjari na kulinda wapigakura.

Alisema, CCM itafanya kampeni za kampeni za kitanda kwa kitanda, nyumba kwa nyumba, paa kwa paa ili kuhakikisha ushindi unapatikana kwa nafasi ya Rais, wabunge, madiwani na hata Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Jumuiya ya Wazazi itakuwa na jukumu la kuendesha mitambo hiyo ya kisasa, kuangalia madereva, kushika breki, kufuata masharti ya barabarani wakati wa kupunguza mwendo ili kuhakikisha kampeni zinafanyika ndani ya siku 62 na ushindi unapatikana.

Alisema Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) wakiongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa UWT, Gaudentia Kabaka wataongoza kuhakikisha mitambo hiyo inapata mafuta, inawekwa maji na kukarabati mitambo hiyo ili endelee kufanya kazi wakati wa kampeni.

Dk Bashiru alipongeza idadi ya wanawake waliojitokeza kuwania nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi kwa kuwa imeongezeka mara mbili na hiyo inaonesha wazi kwamba wanajiamini na wapo tayari kuipa ushindi CCM.

Alisema, CCM ilimchagua Magufuli agombee urais kutokana na uwezo wake wa kuongoza, ni mcha mungu, mtii na ana msimamo katika kutetea maslahi ya Taifa.

Dk Bashiru alisema kutokana na sifa hizo za Magufuli, wajumbe 1,822 wa Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Julai 11, 2020 jijini Dodoma walimpa kura asilimia 100 ili apeperushe bendera ya chama hicho. 

Alisema, Rais Magufuli amepewa dhamana ya kupeperusha bendera ya chama hicho, kutokana na kufanya kazi nzuri akiwa Mbunge, Naibu Waziri na Waziri katika wizara tatu na kwamba, alifanya kazi nzuri zaidi katika Wizara ya Ujenzi ambako alijenga madaraja na barabara.

“Magufuli ni mtu wa watu, mnyenyekevu, kiongozi anayetetea haki za wanyonge na kiboko cha mafisadi na wala rushwa nchini,” alisema Dk Bashiru.

Alisema Magufuli si mkali kuliko yeye, ni mpole, lakini ni mkali kwa watu wanaotenda maovu, ni tishio la mabeberu, na kwamba Tanzania si shamba la bibi tena.

Dk Bashiru alisema huu ni mwaka wa uchaguzi, wagombea wana maneno mengi, wengine wanasema, ‘kazi na bata,’ lakini hafahamu msemo una maana gani, ni kula au kulala au kutembea na bata, lakini wana-CCM wasipoteze muda na kauli za kejeli na mizaha hiyo.

Alisema ana uhakika wa ushindi mkubwa katika nafasi ya urais, ubunge, udiwani na uwakilishi na kwamba, halmashauri zote nchini zitaongozwa na chama hicho.

Dk Bashiru alisema pia chama hicho kitapata ushindi kwa wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi, na pia CCM itashinda mapema kabisa katika uchaguzi wa urais Zanzibar.

Alisema, CCM haijafanya kazi na bata, imefanya kazi na Watanzania na haina misemo kwamba kura zitapigwa kwa vitu, madaraja, ndege, vivuko shule au umeme, bali Watanzania wataipigia kura.

Alisema CCM itapigiwa kura kutokana na kodi za wananchi ambazo zimetumika kujenga miradi ili kuwaletea maendeleo kwa kuwa bila madaraja, reli na elimu bure kwa watoto, bila uhakika wa chakula, vituo vya afya na usalama, amani na upendo na mshikamano, hakuna Tanzania.

Alisema Magufuli si king’ang’anizi wa madaraka, anafanya kazi na hiki ni kipindi cha pili na cha mwisho. 

“Si Rais wa kudumu wala si Mwenyekiti wa kudumu anafuata nyayo za hayari Mwalimu Julius Nyerere ya kuachia madaraka”alisema.

Dk Bashiru alisema usultani na kubadili bendera za vyama kila mwaka,  ameviachia vyama anavyoshindana navyo, yeye ni kiongozi wa kuzingatia muda wa madaraka.

Alisema jana Magufuli na mgombea Mwenza Samia walifika kuchukua fomu ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kusaini kitabu kuthibitisha kwamba wamechukua fomu na kulipia fomu sh milioni moja kama utaratibu unavyotaka.

Dk Bashiru alisema CCM itafanya kampeni za kistarabu na nidhamu lakini zenye joto kali. 

“Moto watakaowasha waangalie usije ukawababua waliojitokeza, Afadhali John Cheyo na Augustino Mrema walioona mbali na wameamua kumuunga mkono Rais Magufuli”alisema.

Magufuli na mgombea mwenza wake Samia wanatakiwa kutafuta wadhamini 2,000 nchini katika mikoa 10 ikiwemo miwili ya Zanzibar na minane ya Tanzania Bara.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi