loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mawakili watakiwa kuepuka mivutano

OFISI ya Wakili Mkuu wa Serikali imesema haitasita kuwasilisha rufaa katika Mahakama za juu kwa ajili ya kupata nafuu nyingine inapoona sheria zinakiukwa.

Aidha imesema ina jukumu la kusimamia na kuhakikisha sheria zinasimamiwa na kwamba jamii ina jukumu la kuzingatia wajibu na haki zao zisimamiwe. 

Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata jana aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa, baada ya hukumu hiyo, baadhi ya mawakili walipinga uamuzi wa Mahakama kwamba inashindwa kusimamia Katiba ya Tanzania.

Aliyasema hayo wakati akizungumza kuhusu hukumu ya Mahakama ya Rufaa iliyotengua uamuzi wa Mahakama Kuu Tanzania ulioelekeza kuwa Kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kwa kufanya makosa yaliyoainishwa na kifungu hicho kutokuwa na dhamana.

Aliwaasa mawakili kukumbuka wajibu wao bila kujiingiza katika mivutano ya mihimili na endapo hawakuridhishwa na uamuzi wakate rufaa ili wasikilizwe upya na si kulalamika.

Aliongeza kuwa kama jamii inadai sababu za kupelekwa kwa maombi hayo ni ubambikiziwaji wa kesi, lazima uwepo ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai hayo na kwamba katika kesi hiyo hoja hiyo haikuzungumzwa.

"Mahakama kwa kauli moja ilikubaliana na hoja za Serikali kwamba kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 ya Sheria za Tanzania hakikinzani na Katiba ya nchi," alisema Malata.

Alisema jopo la majaji watano waliotoa uamuzi katika kesi hiyo ikiwemo Jaji Stella Mugasha, Dk Gerald Ndika, Jacobs Mwambegele, Mwanaisha Kwariko na Ignas Kitusi, lilibainisha kuwa masharti ya kifungu hicho hayakiuki matakwa ya Ibara ya 13 (3) na 15(1) (2) ya katiba.

Kwa kujibu wa hukumu hiyo, uamuzi ya Mahakama Kuu Tanania haukuwa sahihi kwa sababu Katiba ndio inayoruhusu baadhi ya makosa kutokuwa na dhamana.

"Kwa mfano makosa ya mauaji je, ingekuwa watu wanaofanya matendo ya mauaji wanaachwa kwenye jamii wale ndugu wa waliouawa wangefurahi? Na ndio maana Bunge liliamua kuweka sheria hii ili makosa makubwa kama haya ya mauaji na mengine ya uhujumu uchumi, biashara haramu za binadamu, dawa za kulevya na uhaini kutokuwa na dhamana," alisema Malata na kuongeza;

"Unapoua usitarajie Mahakama itakupa dhamana kwani ingeruhusiwa kufanya hivyo, kungekuwa na athari kubwa kwenye jamii ikiwemo usalama wa mtenda kosa, anaweza kuuawa, kupoteza mashahidi na pia  itaruhusu kuendelea kwa vitendo vya mauaji katika jamii."alisema.

Malata alifafanua kuwa masharti yaliyomo katika Katiba yanafafanua msingi wa haki, uhuru na uwajibikaji na hayaharamishi sheria iliyotungwa wala kuzuia sheria yoyote kutungwa au jambo lolote kufanywa kwa mujibu wa sheria hiyo.

"Kwa ajili ya kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru na haki za watu binafsi, kuhakikisha ulinzi na usalama wa jamii, afya ya jamii, mipango ya maendeleo ya nchi ya kukuza taifa," alisema.

Pia alisema kifungu hicho kililenga katika kutekeleza vifungu vya 13(3) kuhusu wajibu wa mamlaka nyingine za nchi zinazowajibika kulinda usalama wa raia na mali zao.

Aidha, alisema katiba kama sheria mama inapaswa kutafsiriwa kwa mapana yake kwa kuzingatia malengo, maudhui yake katika kulinda haki ya kila mtu na jamii kwa ujumla na kwamba ikitafsiriwa bila kuhusisha sheria nyingine ni rahisi kuleta sintofahamu katika jamii.

Alisisitiza kuwa utaratibu wa kuzuia dhamana ni wa kikatiba kwa kuwa wakati Ibara ya 15(1) ya Katiba inampa mtu haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru, ibara ya 15 (2) inaruhusu haki na uhuru wa mtu kuingiliwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria lengo ni kulinda haki na usalama wa jamii.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) walikata rufaa hiyo namba 175/2020 wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu katika shauri namba 29/2019 lililofunguliwa na Dickson Sanga akitaka makosa hayo yawe na dhamana kwa madai kuwa kifungu kilichokuwa kinazuia dhamana, kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi