loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kosa la matumizi ya neno ‘tia’ katika ‘nimetia nia’

LUGHA yoyote ile hukua kwa sababu mbalimbali. Ongezeko la msamiati ndio msingi mkubwa wa ukuzaji wa lugha. Sababu za kukuza lugha huweza kuwa shughuli mbalimbali mfano za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. 

Shughuli kama hizi huweza ama kuibua neno jipya au kukuza matumizi ya neno/maneno ambayo yalikuwapo awali katika lugha husika lakini watu wengi hawakupata fursa ya kulisikia au kulitumia mara kwa mara. 

Kwa mfano, mlipuko wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya korona ulisababisha matumizi ya neno barakoaambalo lilikuwepo kutumika na kufahamika zaidi.

Katika wiki mbili zilizopita kulikuwa na tukio kubwa katika nchi yetu ambalo liliazima masikio ya kila mzawa na asiye mzawa. Hili lilikuwa tukio la uchukuaji fomu kwa watu mbalimbali wa vyama vya siasa kuomba kuteuliwa kugombea nafasi mbalimbali ndani ya vyama vyao. 

Binafsi kama mwanaisimu na mdau wa lugha ya Kiswahili nilivutiwa na jinsi mchakato ulivyokuwa umechangamka lakini pia nilivutiwa pia kwa sababu nilijua wazi kuwa lugha yetu ya Kiswahili ingekuzwa pia katika mchakato huo. 

Nimefuatilia kwa karibu sana mchakato wa suala zima la uchukuaji fomu kwa wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa na nilifuatilia matumizi ya lugha kwa karibu pia. 

Baada ya kufanya upembuzi wa kina nikagundua makosa katika matumizi ya neno TIAambalo limetumika katika sentensi mbalimbali za wagombea na hata wasio wagombea. 

Mfano, sentensi Mimi nimetia nia, Nimetia nia, na wewe katie nia, au wagombea wote waliotia nia wamepita n.k.  Ugunduzi huu pia umenikumbusha matumizi ya neno tiakwa wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili. Mara nyingi nimesikia watu wakisema, tia neno, sitii neno n.k. 

Kimsingi mchakato huu wa uchukuaji fomu kwa wagombea mbalimbali umechochea kitu fulani ndani ya lugha ya Kiswahili ambacho kilikuwa kimezoeleka nacho ni matumizi ya neno hilo tia. Kimsingi matumizi yaliyopewa neno tiakatika sentensi hizo si sahihi.

Mwanzo wa Mkanganyiko:

Yapo maneno katika lugha ambayo ni visawe. Haya ni maneno ambayo huweza kuwa na maumbo tofauti na matamshi tofauti pia lakini hurejelea kitu kimoja kimaana.  

Katika muktadha wa kiuchunguzi ilionekana wazi kuwa mkanganyiko unatokea kwa sababu ya baadhi ya watu walioanza kulitumia neno tia ndivyo sivyo kulichanganya na neno tangaza. 

Kwa maneno mengine ni kwamba walifikiri kuwa kutangaza niani sawa sawa na kusema kutia niajambo ambalo si sahihi. Walifikiri kuwa neno tia na neno tangaza ni maneno tofauti yanayorejelea dhana ile ile moja (visawe). 

Mtazamo huu si sahihi kwa sababu kwa mujibu wa Kamusi ya TUKI, toleo la tatu (2013:550 na uk. 564-565) maneno hayo yamepewa maana tofauti kwa kila neno. 

Ni kweli lugha ni ya jamii lakini hatuna budi kama wataalamu kuelekeza matumizi sahihi ya maneno hasa pale misingi ya matumizi yanapokiukwa au kupotoshwa. Sasa tuyachambue maneno yenyewe. 

Nenotiaambalo ni kitenzi, (tena kitenzi elekezi- kitenzi kinachoweza kuruhusu kuambatana na kiathiriwa cha tendo- yambwa/kitendwa, mtendwa) kwa mujibu wa kamusi ya TUKI toleo la (2013) lina maana kadhaa kutegemeana na muktadha au mazingira ya matumizi yake. 

Maana zake ni, 1. fanya kitu kiwemo ndani ya kingine (ingiza), 2. fanya kitu kiwe na hali fulani, 3. Adabisha mfano, tia adabu, 4. Fanya kitu kiwe na aibu, kiwe na hofu/mashaka n.k. 

Tia vile vile huweza kuwa aina ya ngoma ambayo huchezwa hadharani kwa mashairi kwa kutumia manyanga. Katika kupitia maana zote sijaona maana inayoelekea muktadha wa matumizi ya tia katika sentensi ambazo tumekwisha zitaja katika makala hii. 

Kwa mfano mtu akisema Ninatangaza niaje anaichukua nia hiyo na kuiweka wapi? Kimsingi hapa ni kwamba mtu huyu anataka nia yake ijulikane kwa watu. Kwa hiyo ni makosa kusema ametia nia katika muktadha wa kutangaza nia yake ijulikane kwa watu. 

Je, kutia nia ni kuadabisha? Kutia nia ni kufanya kuwe na hofu? Je, kutia nia ni kuzua aibu? Kwa uhakika matumizi ya neno tiakatika sentensi tia niani potofu. Hakuna namna yeyote ambapo unaweza kupata maana ya sentensi hiyo katika muktadha wa kusema kusudio, haja, lengo, dhamira n.k . 

Makala haya yameandikwa kwa wakati mwafaka kabisa kwani neno hili linaendelea kushika kasi katika matumizi huku likizua utatizi mkubwa. Sasa neno sahihi ni lipi? Katika kutaka kuelezea nia, dhamira, kusudi au lengo lipo neno sahihi kabisa katika Kiswahili sanifu ambalo linafaa kutumiwa badala ya neno Tia nia. Neno hilo ni tangaza niaau sema nia

Neno tangaza kwa mujibu wa kamusi ya TUKI toleo la (2013) ni kitenzi ambacho kina maana ya kutoa habari kwa mtu au watu kuhusu jambo fulani. Neno nia maana yake ni dhamira au kusudi au lengo la kutaka kutaka kukamilisha haja au jambo fulani.  

Kwa mantiki hii ni kwamba  tukiunganisha neno (tangaza na nia) tutapata maneno mawili yaani tangaza nia. Huu ndio muktadha sahihi kabisa kwa matumizi ya maneno hayo na si tia nia.

Ndio muktadha sahihi wa matumizi ya maneno hayo kwa sababu wakati wa zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali, mchukua fomu ana nia, dhamira, lengo au haja ambayo anataka kusema kwa mtu, au watu. Sasa namna ya kuwaambia watu juu ya kusudio, nia, dhamira au haja yake ni kutangaza na sio kutia. Hivyo katika lugha ya Kiswahili tunatangaza nia kwa maana ya kutoa habari juu ya haja, lengo, kusudi, dhamira yako au ya mtu juu ya jambo fulani. 

Mgombea anapotangaza nia ni kwamba ana mambo kadhaa ambayo anataka watu wayajue juu ya dhamira yake. Katika matumizi ya maneno tangaza na tia kamwe maneno haya hayawezi kutumiwa kumaanisha kitu kilekile bali kila neno lina matumizi yake tofauti kabisa. 

Nishauri tu kwamba tuipende lugha yetu ya Kiswahili, tusiharibu makusudi na wala tusiyapotoshe matumizi ya maneno yake. Nashauri pia waandishi wa habari wawe wanatumia Kamusi au uwauliza wataalamu ili kujua kama neno fulani wanalotumia ni sahihi katika lugha yetu adhimu ya Kiswahili au la.

Lugha ya Kiswahili ni urithi mkubwa na tunu kubwa tuliyoachiwa na watangulizi wa taifa hili. Lugha ya Kiswahili ina misingi yake ambayo inapaswa kuzingatiwa katika matumizi yake. 

Katika matumizi ya maneno yenye maana ya unyume au visawe huhitaji umakini mkubwa katika matumizi yake ili kuepukana na mkanganyiko katika matumizi ya maneno hayo. Kiswahili chetu ni urithi wetu.

Mwandishi wa makala haya yupo katika Idara ya Lugha na Isimu, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Arusha. Mawasiliano yake ni: 0752631092

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Lotha Loyewo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi