loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ninja arejea Yanga, Kisu atua Azam

BEKI wa kati, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amerejea Yanga huku golikipa, David Kisu akijiunga na Azam FC akitokea Gor Mahia ya Kenya kwa mkataba wa miaka miwili kila mmoja.

Ninja aliitumikia klabu hiyo mwaka juzi na mwaka jana, alikwenda Marekani kwenye timu ya La Galaxy kucheza soka la kulipwa ingawa hakudumu muda mrefu.

Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Wakili Simon Patrick, alisema wamefurahi kumrejesha mchezaji huyo kwani ni mmoja wa mabeki wanaotegemewa kuisaidia timu hiyo.

“Usajili unaendelea vizuri, tayari tumemrejesha Ninja na bado mambo mazuri yanakuja, kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao kuhakikisha tunafanya vizuri,” alisema.

Usajili huo kwa wachezaji wa ndani ni wa tano, ambapo tayari wamekamilisha kwa beki Bakari Mwamnyeto kutoka Coastal Union, Zawadi Mauya kutoka Kagera Sugar, Yassin Mustapha kutoka Polisi Tanzania na Waziri Junior kutoka Mbao FC.

Yanga wameweka wazi kuwa wanatarajia kuingia kambini Agosti 10, kujiandaa na msimu mpya huku wakiendelea na harakati za usajili wa kimataifa.

Wakati huo huo, Azam FC imesema usajili wa golikipa Kisu ni sehemu ya mapendekezo ya benchi lao la ufundi.

Kipa huyo aliyewahi kuzichezea timu za Njombe Mji na Singida United, kabla ya kutimkia nchini Kenya, amekuwa na msimu nzuri akiwa na Gor Mahia baada ya kucheza mechi 15 na kati ya hizo tisa hajaruhusu nyavu  kutikiswa.

Kisu hatasahaulika Kenya kwani aliwahi kufunga goli kwa mpira mrefu aliopiga kutoka golini kwake na kwenda kuingia kwa wapinzani katika mchezo ambao timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Bandari.

Huo ni usajili wa tano kwa Azam FC kwa ajili ya msimu ujao, wengine waliosajiliwa ni Awesu Awesu, Ally Niyonzima, Ayoub Lyanga na Ismail Aziz Kada. 

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi