loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

DIT yapewa Kamati ya wataalamu wa Tehama

SERIKALI imezindua Kamati Maalumu ya Ushauri ya Wataalamu wa Viwandani katika Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kusaidia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuzalisha wataalamu wenye ujuzi mkubwa wa kupambana katika soko la ajira kupitia viwanda.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilipo alizindua kamati hiyo jana jijini Dar es Salaam yenye lengo la kuwezesha taasisi hiyo kupata ushauri wa kutekeleza mradi wa Kituo cha Kikanda cha Umahiri wa Tehama (RAFIC) chini ya mradi mkubwa wa EASTRIP unaogharimu Sh bilioni 37.

Dk Akwilipo aliitaka kamati kufanya kazi ya kushauri DIT iongeze umahiri wa Tehama katika kuzalisha wataalamu wenye ujuzi mkubwa na kufikia lengo la Serikali la uchumi wa viwanda utakaozalisha ajira nyingi hasa kwa kundi la vijana kama alivyobainisha Rais John Magufuli Novemba mwaka 2015 alipozindua Bunge.

Aliipa kamati maeneo manne ya utekezaji ikiwamo kutoa mapendekezo yatakayoboresha mitaala ya ufundishaji na ufundi na kusaidia DIT kuimarisha uhusiano na viwanda kuzalisha ajira, kusaidia taasisi kujua mwelekeo wa soko, kuishauri namna bora ya kuzalisha wahitimu wenye ustadi, weledi na ufanisi na kuongeza elimu kwa vitendo

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Sanctus Mtsimbe, alimhahikishia Katibu Mkuu kuwa watatekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa kwa kuwa kamati ina wataalamu wabobezi katika eneo la Tehama na kuifanya DIT kuwa kituo kikuu cha umahiri ndani na nje ya nchi kitakachozalisha wataalamu wa hali ya juu.

Awali, Mkuu wa DIT, Profesa Preksedis Ndomba, alisema mradi wa EASTRIP unafanyika katika nchi tatu (Ethiopia, Kenya na Tanzania) na kwa Tanzania vyuo vinne ikiwamo DITvilichaguliwa kuutekeleza. Hapa nchini ulizinduliwa mwaka jana na utakamilika mwaka 2024.

Mbali na Mtsimbe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati, wajumbe wengine na maeneo walikotoka kwenye mabano ni James Kilaba (TCRA), Jumanne Mtambalike (Sahara Ventures), Samwel Mujinja (TRA), Harold Temu(Electriplan (T) Ltd), Esther Mengi (Serensic Afrika), Profesa Patrick Nsimama, Dk Joseph Matiko na Dk John Msumba, wote kutoka DIT. 

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi