loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Agizo la Magufuli kupanua Dumira-Feri latekelezwa

SERIKALI ya Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa huo imeanza kufanya tathmini ya jinsi ya kupanua barabara katika eneo la Dumila – Feri katika Barabara Kuu ya Dodoma – Morogoro ili kujenga vibanda vya wafanyabiashara.

Utakelezaji huo ni baada ya agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Agosti 5, mwaka huu alipozungumza na wafanyabiashara wadogo katika eneo la Dumila Darajani wilayani Kilosa mkoani humo alipokuwa njiani akielekea mkoani Dodoma.

Rais aliagiza na kutaka wafanyabiashara wa eneo la Dumila maarufu kama Feri ambao wako kandokando ya Barabara ya Dodoma - Morogoro kujengewa vibanda vya kufanyia biashara zao.

Katibu Tawala wa Mkoa huo, Emmanuel Kalobelo pamoja na timu yake juzi walifika eneo la Dumila kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa agizo la Rais kwa kufanya tathmini ya jinsi ya kupanua barabara katika eneo hilo ili kujenga vibanda hivyo vya wafanyabiashara.

Kalobelo akiwa katika eneo hilo la Dumila alisema agizo la Rais limeanza kutekelezwa kuanzia siku hiyo na kwamba hadi kufikia Agosti 10 mwaka huu vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya kazi hiyo vitawasili eneo la tukio na kuanza kazi.

Pamoja na kutoa ufafanuzi huo, Katibu Tawala huyo alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Asajile Mwambambale kuanza kutafuta fedha kwa ajili ya kazi hiyo na kuanza ujenzi wake haraka badala ya kusubiria fedha zilizoahidiwa na Rais.

Kalobelo pia aliwagiza wataalamu wanaochora michoro ya vibanda vitakavyojengwa eneo hilo kuhakikisha vibanda hivyo vinakuwa rafiki kwa makundi yote wakiwemo wajasiliamali wa kupita vyakula pamoja na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda ili makundi yote yaliyokuwa yanafanya biashara eneo hilo kutoathiriwa na mpango huo mpya.

“Natoa wito kwa uongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Kilosa pamoja na wafanyabiashara wa eneo la Dumila, kutoa ushirikiano wakati wote wa ujenzi wa vibanda hivyo na kuhakikisha msaada huo unawanufaisha wafanyabiashara halisi waliokuwa wanafanya biashara  eneo hilo badala ya kuingiza watu wasiohusika au hawakuwepo hapo awali,” alisema Kalobelo.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo pamoja na kumshukuru  Rais kwa msaada wa Sh milioni 100  za kuwajengea wafanyabiashara maeneo bora ya kufanyia biashara zao, alisema kazi aliyoiagiza Rais imeanza kutekelezwa  kwa kuwatambua wafanyabiashara wa eneo la Feri - Dumila na kwamba watafanya kazi hiyo kwa umakini na haraka ili wananchi wanaohusika waweze kunufaika na msaada uliotolewa na Rais mapema.

Meneja wa Tanroads, Mkoa wa Morogoro, Nkolante Ntije alisema agizo la Rais pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara lililenga pia usalama wa wafanyabiashara wa eneo hilo.

Ntije alipandekeza vibanda vitakavyojengwa eneo hilo vijengwe upande mmoja wa kushoto wa barabara ukitokea Dodoma kwenda Morogoro ili kupunguza watu kukatisha mara kwa mara barabarani hali inayoweza kusababisha ajali.

Hata hivyo, aliuomba uongozi wa wilaya ya Kilosa ambao unadhamana ya kutoa wataalamu wa kuchora michoro ya vibanda vitakavyojengwa eneo hilo, kuwapatia michoro hiyo mapema ili nao waanze kazi ya hiyo kwa haraka.

Awali Mwenyekiti wa kijiji cha Magole , Hamad Seleman akizungumza kwa niaba ya wananchi wa eneo la Dumila – Feri  aliahidi kutoa ushirikiano wa dhati wakati wote wa ujenzi wa vibanda hivyo na kwamba atasimamia ipasavyo mali zote zitakazoletwa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi kwa vile  mradi huo umeletwa kwa ajili yao na ni mali yao.

SERIKALI ya Awamu ya Tano chini ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi