loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wachina 6 kortini kwa kuongoza genge la uhalifu

RAIA sita wa China wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kukutwa na nyara za serikali.

Raia hao ni Jin Erhao (35) anayejishughulisha na usafirishaji, Chengfa Yang (49) mfanyabiashara, Ren Yuangqing (55) Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji ya Sinota, Shu Nan (50) mfanyakazi katika kampuni hiyo, Chen Shinguang (45) Meneja katika kampuni hiyo na Gu Jugen (57) Meneja Ufundi wa kampuni hiyo, wote wakiwa ni wakazi wa Mtaa wa Sokoine, Ilala jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo juzi na kusomewa mashtaka mbele Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate ambapo upande wa Jamhuri uliwakilisha na Wakili wa Serikali, Salim Msemo akishirikiana na Wakili wa Serikali, Eliya Athanas huku upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Ibrahim Bendera.

Akiwasomea mashtaka, Wakili Msemo alidai katika shtaka la kwanza wanakabiliwa na kosa kuongoza genge la uhalifu na kudai Agosti Mosi, 2020 katika mtaa wa Sokoine, Ilala jijini Dar es Salaam washtakiwa wote kwa pamoja na kwa makusudi walisimamia genge la uhalifu lililopelekea kupatikana kwa tausi mmoja mwenye thamani ya dola za Marekani 500 sawa na Sh 1,155,000 za Tanzania kinyume na sheria ya wanyama pori.

Katika shtaka la pili Wakili Msemo alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa la kupatikana na mali iliyopatikana kwa njia isiyo halali ambapo inadaiwa Agosti Mosi, 2020 katika mtaa wa Sokoine jijini Dar es Salaam washtakiwa hao walikutwa na nyara ya serikali ambayo ni Tausi mmoja mwenye thamani ya Sh 1,155,000 kinyume na sheria ya wanyama pori.

Aliendelea kudai kuwa katika shtaka la tatu washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kukutwa na nyara za serikali ambayo ni tausi mmoja mwenye thamani ya Sh 1,155,000 kosa wanalodaiwa kulitenda Agosti Mosi, 2020 katika mtaa wa Sokoine, Ilala jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasomea mashtaka Wakili Msemo alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na upande haukuwa na pingamizi la dhamana lakini waliomba masharti yawe makali kulingana na mashtaka yalivyo.

Akitoa masharti ya dhamana hakimu Kabate aliwataka washtakiwa hao kila mmoja kupeleka wadhamini wawili wa kuaminika walio ndani ya Mamlaka ya Mahakama (Ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani) watakaosaini bondi ya Sh 500,000 kila mmoja.

Pia aliwataka kuwasilisha pasi zao za kusafiria mahakamani na kuwapa amri ya kutokusafiri nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila ruhusa ya mahakama.

Wakili wa utetezi Bendera alidai mahakamani hapo kuwa pasi za kusafiria za washtakiwa hao kwa sasa zinashikiliwa na polisi hivyo uwezekano wa kuziwasilisha kwa wakati ule haukuwepo ambapo Hakimu Kabate alimtaka kuwasilisha uthibitisho iwapo ni kweli pasi hizo ziko mikononi mwa polisi.

Aliwataka mawakili wa pande zote kushirikiana kupata uthibitisho huo ili waweze kuwapatia washtakiwa dhamana.

“Wakili Msemo mnaweza kushirikiana kupata uthibitisho, hata kwa simu, mimi nipo mkipata uthibitisho tutakamilisha dhamana lakini kwa Sasa washtakiwa watabaki mahabusu mpaka tupate uthibitisho,” alisema Hakimu Kabate.

Washtakiwa walirudishwa mahabusu na kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 20, mwaka huu itakapotajwa tena.

SERIKALI ya Awamu ya Tano chini ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi