loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Lissu, Mwanga wachukua fomu za urais NEC

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amechukua fomu kwenye ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). 

Lissu pamoja na mgombea mwenza, Salumu Mwalimu,  walikabidhiwa mkoba wenye fomu na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu, Semistocles Kaijage jijini Dodoma. 

Wakati huo huo, mgombea urais Chama cha Demokrasia Makini (DM), Cecilia Mwanga amechukua fomu kugombea nafasi hiyo akiwa ameongozana na mgombea mwenza, Tabu Juma. 

Akizungumza baada ya kukabidhi fomu hizo, Kaijage alisema uteuzi wa wagombea utafanyika Agosti 25, 2020 na wanaweza kuwasilisha fomu zao kabla.

Alisema kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi, Tume inatakiwa kujiridhisha na sifa ya kuteuliwa kugombea nafasi hiyo.

Aliwapongeza wagombea hao kwa kujitokeza kuwania nafasi hiyo ya uongozi wa juu nchini.

Mkurugenzi wa Tume Dk Charles Mahera alisema wagombea hao wanatakiwa kutafuta wadhamini katika mikoa 10; minane ya Tanzania Bara na miwili Zanzibar. 

Mahera alisema kama wagombea watapenda, kati ya Agosti 22 na 24 wanaweza kufika kukagua fomu zao kabla ya uteuzi. 

Uchukuaji fomu za kugombea urais ulianza Agosti 5 na utakamilika Agosti 25, siku moja kabla ya kampeni  kuanza Agosti 26, 2020 zitakazohitimishwa Oktoba 27 kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi