loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mtanzania ashinda tuzo mfatifu bora kimataifa

MTANZANIA Hamenya Mpemba ameshinda Tuzo ya Mtafiti Bora wa kimataifa katika jimbo la Inner Mongolia nchini China kutokana na utafiti wake uliofanikisha kugundua uwapo wa mbwa mwitu katika hifadhi jimboni humo. 

Ugunduzi huo ulifanyika kupitia kamera nyingi alizofunga katika eneo la pori la Hifadhi ya Taifa ya Hanma iliyopo jimboni humo huku ikielezwa, watafiti wengi wamekuwa wakifanya utafiti eneo hilo bila mafanikio ya kumuona mnyama huyo ambaye tangu awali alisadikiwa kuwapo kutokana na viashiria mbalimbali. 

Tuzo hiyo ilikuwa ikishindaniwa na watafiti kutoka mataifa mbalimbali duniani na idadi ya waliojitokeza kwenye mabano ni Pakistan (9), Marekani (1), Thailand (4), Australia (8), Urusi (5) na Tanzania ikiwakilishwa na Mpemba (pichani) ambao walianza masomo kuanzia miaka ya 2015. 

Akizungumza na gazeti hili, Mpemba (36) anayesoma Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Uhifadhi wa Wanyamapori katika chuo cha Northeast Forest, mjini Harbin, China, alisema utafiti uliompa ushindi sehemu ndogo ya aliowahi kufanya jimboni humo na tuzo imetolewa na taasisi ya hifadhi za asili jimboni humo.

Utafiti uliangalia athari za uwapo wa viashiria mfano picha, sauti, harufu vya wanyama wakubwa wapatikanao au waliowahi kupatikana maeneo hayo; hususani chui milia, dubu kwenye pori kwa mtawanyiko na tabia za wanyama wengine. 

“Mimi na wenzangu tulikuwa tukitumia zaidi kamera maalumu za kusomea wanyamapori . Hufungwa sehemu ya mti ambayo itawezesha kumpiga picha mnyama yeyote atayepita eneo husika…Wakati naendelea na utafiti huo mkubwa ndipo nilipofanikiwa kumpata mnyama huyo kwenye moja ya kamera tulizosambaza porini,” alisema. 

Kwa mujibu wa mtafiti huyo, eneo waliloweka kamera lipo mbali katikati mwa hifadhi inayotajwa kuwa ni ngumu kufanya tafiti kutokana na mazingira ya milima na mabonde makubwa.

Baada ya ugunduzi, aliamua kuandika chapisho la kisayansi kuripoti juu ya kuonekana kwa mnyama huyo mahali hapo na kufanikiwa kuchapisha utafiti huo katika jarida la kimataifa la Zuolojia la Pakistani. 

Mpemba ambaye yupo nchini mkoani Arusha, aliliambia HabariLeo kwamba taarifa za ushindi alizipokea mwanzoni mwa wiki hii baada ya kutumiwa tangazo husika na marafiki zake waliopo China. “Nasubiri kuipokea ana kwa ana maana hivi sasa nipo Tanzania,” alisema. 

Kijana mwenye machapisho manane ambayo yote yanahusu tabia, uhusiano, uwepo, mazingira na maisha ya wanyamapori kwa ujumla, anaendelea na masomo ya Shahada ya Uzamivu katiaka Chuo cha Northeast Forestry mjini Harbin jimbo la Heilongjiang. 

Alianza mwaka 2015 na ilikuwa amalize mwaka huu lakini kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ugonjwa wa Covid 19, anatarajia kumaliza mwakani. 

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi