loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wasimamizi wa Uchaguzi Mkuu waonywa ushabiki

WASIMAMIZI wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata na jimbo wametakiwa kuepuka ushabiki wakati wa kutekeleza majukumu yao kuepusha vurugu katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Nzega Mjini, Philemon Magesa alitoa wito huo wakati wa kufunga mafunzo ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi mkuu kutoka kata 20 za halmashauri hiyo.

Magesa alisema ili wasimamizi wasaidizi wawe salama katika mchakato huo, ni vyema wakazingatia katiba, sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi huo.

Aliwataka wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, washirikishe vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika masuala ambayo wanastahili kushirikishwa.

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi Glays Barthy aliwataka walioteuliwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) ambao ni wanachama wa vyama vya siasa kuhakikisha wanajitoa katika vyama vyao kusimamia uchaguzi kwa umakini ikiwa ni pamoja na kujiepusha kutoa maoni ambayo yanaweza kusababisha uvunjifu wa sheria za uchaguzi na kanuni zake.

“Muwe makini na makundi mliyomo kwa kuepuka kutoa maoni ambayo yanaweza kusababisha kuonekana unashabikia upande fulani na kusababisha vurugu,” alionya na kusisitiza kwamba katika kipindi chote cha uchaguzi kujizuia kujadiliana na makundi mbalimbali.

Wakati huo huuo kutoka Songwe, wasimamizi wasaidizi wa uchguzi ngazi ya kata katika Majimbo ya Vwawa na Mbozi wilayani Mbozi wamepata mafunzo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuhakikisha wanasimamia na kukamilisha vema mchakato wa Uchaguzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Hanji Godigodi akifungua mafunzo hayo yatakayochukua siku tatu, alisema yanayotolewa na NEC kuhakikisha wasimamizi hao ngazi ya kata kuhakikisha wanafanikisha mchakato wa uchaguzi unamalizikasalama pasipokuwa na vurugu wala migogoro yoyote.

Alisema Wilaya ya Mbozi yenye majimbo mawili ya Vwawa na Mbozi vituo vya uchaguzi vimeongezeka kutoka 535 mwaka 2015 na kufikia vituo 675. Jimbo la Mbozi vimeongezeka vituo 74 na Vwawa ni vituo 66.

Mwenyekiti wa Uchaguzi Wilaya ya Mbozi alisema kuwa wasimamizi wa uchaguzi wanasisitizwa na kupewa mafunzo ili kuhakikisha wanazingatia taratibu na kanuni zitakazotolewa katika miongozo mbalimbali ili kuweza kufanikisha kusimamia uchaguzi utakaofnyika Oktoba 29.

Alisema changamoto ambayo huwa inajitokeza mara nyingi kwenye uchaguzi ni vyama vya siasa kupitisha muda na kuongeza kuwa mwaka huu wamaejipanga kutoa elimu kwa vyama vishiriki uchaguzi kwa amani na usalama mkubwa.

Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Mbozi, Nemes Chami akiwaongoza wasimamizi hao wa uchaguzi kula viapo vya kujitoa katika vyama vyao na kusaini kiapo cha kutunza siri baada ya mafunzo alisema kuwa wasimamizi wanatakiwa kuzingatia kiapo walichosaini na kuwa tayari kutunza siri.

“Tunaposema umejitoa kwenye chama chako ujitoe kweli kweli tunaomba muwe wazalendo, yote tunayoambiwa ni siri katika mchakato huu wa uchaguzi iwe siri kweli kweli,” alisema Chami.

Katika hatua nyingine kutoka Arusha, msimamizi wa uchaguzi Jimbo, Dk John Pima amewataka wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, kata, maofisa uchaguzi na ofisa ugavi wa halmashauri kufuata taratibu za uchaguzi zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi ili kujenga mazingira rafiki kwa wapiga kura na kupelekea uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 28, 2020 kuwa huru na haki.

Dk Pima alitoa maelekezo hayo jana alipokuwa akifungua mafunzo ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, kata, maofisa uchaguzi na ofisa ugavi wa halmashauri katika ukumbi wa mikutano Ofisi yaMkuu wa Mkoa wa Arusha.

Alisisitiza kuwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, kata, maofisa uchaguzi na ofisa ugavi wa halmashauri wanatakiwa kufahamu kuwa wameaminiwa na kuteuliwa kwa sababu wana uwezo wa kufanya kazi hiyo hivyo mambo muhimu wanayotakiwa kuzingatia ni kujiamini na kujitambua na kwamba wanapaswa kuzingatia katiba ya nchi, Sheria za uchaguzi na kanuni zake, maadili ya uchaguzi na maelekezo yote yaliyotolewa na tume.

Kutoka Mbinga, Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Mbinga mjini Grace Quintine amewataka wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata, kufuata kanuni na sheria za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 Mwaka huu.

Quintine alitoa rai hiyo jana wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa maofisa hao katika Ukumbi wa Halmashauri ya mji Mbinga ambayo yanalenga kuwajengea uwezo katika kusimamia uchaguzi huo na kuongeza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 74 kifungu kidogo cha 6, Tume imepewa jukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Madiwani,Wabunge na Rais.

Alisema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatia kwani hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato huo.

Ofisa Msaidizi wa Uchaguzi jimbo la Mbinga mjini Amos Sangana alisema katika jimbo hilo kuna kata 19 ambapo jumla ya watendaji 30 wamepewa mafunzo kwa ajili ya kwenda kusimamia uchaguzi mkuu ngazi ya kata.

Alisema tume inatarajia mara baada ya mafunzo hayo watendaji hao watakwenda kusimamia kikamilifu mchakato wa uchaguzi kwa kuanzia zoezi la utoaji fomu na uteuzi wa wagombea.

Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya mji Mbinga Elizabert Moshi aliwataka maofisa hao kuwa makini wakati wote wa mchakato wa uchaguzi mkuu na kujiepusha kufanya kazi kwa mazoea au kufuata maelekezo kwa watu wasiohusika na tume ya uchaguzi.

 

Imeandikwa na Mwandishi Maalumu, Tabora, Baraka Messa, Songwe, Veronica Mheta, Arusha na Muhidin Amri, Mbinga.

RAIS John Magufuli ameagiza ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi