loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Morrison asaini Simba, Yanga yatoa neno

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili kama mchezaji huru “Morrison is Red” hiyo ni kauli iliyotolewa jana kwenye mtandao wa kijamii wa Simba na kuweka picha ya mchezaji huyo akiwa amevaa jezi nyekundu akisaini mkataba.

Hiyo ni dhahiri kuwa mchezaji huyo ni mali yao na ataitumikia Simba kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

Baada ya Simba kuchapisha picha za Morrison, uongozi wa Yanga umesema unafuatilia kwa karibu kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii na ikithibitika hatua kali na za mfano zitachukuliwa kwa pande zote zinazohusika.

“Uongozi unawataka wanachama na wapenzi wa Yanga kuwa watulivu kwani mchezaji Bernard Morrison ana mkataba hadi 2022 na shauri baina yake na klabu bado liko mikononi mwa TFF na Jumatatu litasikilizwa,” ilisema taarifa ya Yanga iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana.

Mchezaji huyo alijiunga na Yanga kwenye dirisha dogo la usajili kwa mkataba wa miezi sita ambapo alionesha kiwango bora na hivi karibu Yanga waliridhishwana kiwango chake na kumuongezea mkataba wa miaka miwili na amejumuishwa kwenye kikosi kwa ajili ya msimu ujao.

Lakini kuna sintofahamu kati ya mchezaji huyo na klabu yake ya zamani mwenyewe akisema hakusaini mkataba na viongozi wakisema alisaini suala ambalo lilifikia hatua ya kupelekwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kutolewa maamuzi.

Kabla ya kumaliza msimu huu alianza kuonesha vitendo vya utovu wa nidhamu akisusia baadhi ya mechi na katika mchezo dhidi ya Simba alicheza chini ya kiwango na kumlazimisha kocha, Luc Eymael kumbadilisha kabla ya mchezo kuisha na yeye alionesha kutofurahishwa, na hatimaye kuondoka uwanjani kabla mechi haijaisha.

Baada ya hapo, zikaibuka tetesi za yeye kusajiliwa na Simba ingawa awali walipokuwa wakiulizwa walidai taarifa hizo siyo za kweli. Licha ya Simba kutoweka wazi gharama za usajili wake, tetesi zinaeleza kuwa alipewa zaidi ya Sh. milioni 200 ambazo ni kiwango kikubwa kuzidi kile alichopewa Yanga ndio maana alivutiwa na kuondoka.

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Hersi Said ambaye ndiye aliyemleta mchezaji huyo alisema juzi kama kweli Simba imeamua kumsajili mchezaji huyo basi huenda wao walihusika kumpa kiburi mchezaji huyo.

“Ikiwa watamtangaza basi wataudhihirishia umma kuwa wao ndio waliokuwa wanahusika kumpa kiburi kwa yale aliyokuwa anayafanya nje na ndani ya uwanja, maana kesi ipo kwenye kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya TFF, “. alisema

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi