loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwinyi alivyoibua ‘faraja’ msiba wa Mkapa

TAIFA la Tanzania hivi karibuni lilipita katika majonzi makubwa ya kuondokewa na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa (82), aliyefariki dunia Julai 23 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kutokana na mchango wake katika Taifa, wengi waliuelezea msiba wake kama ni pigo kubwa la pili kwa Tanzania kumpoteza kiongozi wa juu na aliyewahi kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote nchini, baada ya msiba wa aliyekuwa Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki Oktoba 14, 1999.

Kwa hakika msiba wa Mkapa, ulisababisha huzuni kubwa, simanzi na vilio kila kona ya nchi hasa kutokana na ukweli kwamba, kifo chake kimekuwa cha ghafla kwani siku chache kabla ya kufariki dunia, alihudhuria vizuri Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma.

Baada ya shughuli za kumuaga zilizofanyika jijini Dar es Salaa zikijumlisha siku saba alizotangaza Rais John Magufuli za maombolezo, mwili wa kipenzi huyo wa Watanzania, mzee wa uwazi na ukweli, ulipelekwa kijijini kwao Lupaso, wilayani Masasi, mkoani Mtwara alikochagua azikwe.

Mkapa wakati akiwa hai, alichagua azikwe kijijini humo, kwenye eneo la makaburi ya familia, pembeni mwa kaburi la baba yake, mzee William Matwani, aliyefariki dunia Novemba 21, mwaka 1994.

Maelfu ya waombolezaji walihudhuria maziko ya Mkapa yalioendeshwa kwa utaratibu wa kidini na kijeshi.

Viongozi walipata nafasi kupitia mahojiano ya vyombo vya habari na siku ya maziko, kuzungumza jinsi wanavyomfahamu Mkapa.

Siku ya maziko, Julai 29 mwaka huu, miongoni mwa viongozi wa kiserikali waliopata nafasi ya kutoa salamu za pole ni pamoja na Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein.

Kikwete alimwelezea Mkapa kama kiongozi hodari, aliye na utambuzi wa mambo yenye manufaa kwa watu wake. Anasema kwa muda wote aliofanya kazi na Mkapa tangu akiwa mbunge wa jimbo la Nanyumbu na yeye (Kikwete) akiwa Katibu wa CCM Wilaya ya Masasi, alijifunza kufanyakazi kwa ajili ya watu na kushughulikia matatizo ya wananchi.

Baada ya Kikwete kuzungumza kuhusu Mkapa na kutaka Watanzania tuenzi mema mengi aliyowafanyia, Rais mstaafu Mwinyi alikaribishwa naye kutoa salamu za pole kwa familia na wananchi wote.

Mwinyi alianza hotuba yake kwa kumuomba Mungu amsamehe Mkapa makosa yake kwa kuwa naye ni binadamu na huenda amemkosea muumba wake. Hotuba ya Mwinyi ya kumsihi Mungu amrehemu Mpaka ilikuwa ni zaidi ya asilimia 70 ya hotuba nzima.

“Ndugu yetu Mkapa ni mwanadamu kama walivyo wengine, labda katika maisha yake aliwahi kufanya kosa asilolipenda muumba wetu. Katika hali kama hii, mwenzetu akiondoka, jambo la kwanza ni kumwombea usalama kwa Mwenyezi Mungu endapo kakosea”.

Mwinyi alitoa pole kwa Mama Anna ambaye ni mjane wa Mkapa, watoto, watu wa mkoa wa Mtwara, ndugu na jamaa kutokana na msiba huo, akisema Mkapa alikuwa mtu mwema sana lakini alisiyekuwa na mchezo katika kazi.

Alimpa pole Rais Magufuli na kumpa jina la ‘Mzee Magufuli’ akimpongeza kwa kushika nchi ikiwa katika hali mbaya na kufanya kazi iliyohusiwa itekelezwe na Mungu kwa kuwaondolea watu tabu, umasikini na mashaka ambayo ni kazi ya kila kiongozi na ambayo pia ilifanywa na Mkapa.

“Nafsi yangu kama zilivyo nafsi zenu imegubikwa na huzuni kwa kuondokewa na ndugu yetu, kaka yetu, mwenzetu Mkapa, katika hali kama hii muhimu ni kumuombea mwenzetu kama ana makosa Mungu amuwie radhi, Mkapa alikuwa mtu mwema sana na mfanyakazi kweli kweli,” alisema Mkapa.

Hata hivyo, Rais mstaafu Mwinyi hakuishia kumwombea Mkapa rehema na dua, pongezi kwa Magufuli na pole kwa familia na Watanzania, bali aliwatoa waombolezaji kwenye dimbwi la majonzi na kuwapa simulizi kuhusu mara ya kwanza kuvaa viatu na kuwapa faraja na furaha ya ghafla familia na waombolezaji.

Mwinyi alisema katika kusanyiko hilo (maziko), kuwa kuna jambo limemuhuzunisha sana. “Mimi ndiye mkubwa kuliko wote hapa, mimi nimezaliwa mwaka 1925, nimeona mengi, leo nimeona hapa watu, vijana kwa wazee waliopita mbele yenu katika kumuaga ndugu yetu.

“Jambo dogo nimeliona kwenu ninyi, kwangu mimi halikuwa dogo limeniathiri sana,” alisema Mwinyi na kuwaweka watu katika hali ya kutaka kujua mzee amekerekwa na nini. Akaendelea, “Nimeona watu wote wamevaa viatu, mtasema leo mzee Mwinyi ana nini kwani kuvaa viatu ni ajabu? Wakati wangu mimi, tumezaliwa, tumekulia Unguja, tumekwenda katika madarasa, tumekwenda shule, tumekwenda mote, miguu chini (peku).

Kauli hiyo ikaanza kukunjua nyuso za waombolezaji na kuanza kutabasamu lakini bila kujua mzee Mwinyi anataka kusema nini. “Mimi nimevaa viatu mara mbili.

Mara ya kwanza nilipokwenda jandoni (hapo kikaibuka kicheko kwa waombolezaji wote akiwamo Rais Magufuli).

Mara ya pili nina miaka kumi na tatu nilichuma karafuu nikapata hela nikanunua viatu, na nikahakikisha viatu hivyo havitakwisha (kicheko tena kwa waombolezaji), basi badala ya kuvivaa nikavifunga nikaviweka begani ili visiishe,” alisema Mwinyi na kusababisha umati wote uangua kicheko.

“Hiyo ndio kazi ya kiongozi yoyote, kuhakikisha anainua hali ya wananchi wake, ndivyo tulivyojaribu kufanya na ndivyo anatekeleza Rais wetu wa leo Magufuli, na ndivyo alivyofanya ndugu yetu, mdogo wetu marehemu mzee Mkapa, tuendelee kumwombea asamehewe kama ana makosa yoyote, kama nilivyosema inawezekana wakati mwingine ana madoa madoa, aendele huko na karatasi jeupe lisilo na doa,” alimaliza Mwinyi.

Aliposimama Rais Magufuli, alimtania mzee Mwinyi kuwa hakueleza viatu alivitundika kwa muda gani, kauli iliyoamsha kicheko tena.

Baadhi ya waombolezaji walisikika wakisema, Mwinyi amewafanya kuwa wajukuu na yeye ni babu, hivyo ametumia hekima alizojaaliwa, kuwapa simulizi iliyorejesha faraja kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki katika msiba huo mkubwa uliolikumba Taifa la Tanzania.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi