loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwaka mmoja ajali ya Moto Morogoro, ujafa ujaumbika

UKIWA umetimia mwaka mmoja tangu kutokea kwa ajali ya moto ambao kiini chake kilikuwa ni kupinduka kwa lori la mafuta katika eneo la Msamvu mkoani Morogoro na kusababusha vifo vya zaidi ya watu 100, bado makovu ya ajali hiyo hayajapona mioyoni mwa Watanzania.

Ni ajali mbaya iliyozua simanzi na majonzi makubwa kwa watanzania kutokana na kusababisha vifo na majeruhi wengi. Chen Pius, mfanyakazi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) anayejishughulisha na ku toza ushuru wa maegesho ya magari katika eneo la Msamvu, Mkoani Morogoro ni miongoni mwa wa watu waliokumbwa na ajali hiyo mbaya.

Waswahili wanasema ‘usilolijua ni sawa na usiku wa giza’ ndivyo hadithi ya Chen, maarufu kama Zakayo (mtonza ushuru) unavyoweza kuanza kuisimulia.

Anasema, akiwa aliamka salama usalamini, lakini saa chache baadaye siku hiyo ya Jumamosi Agosti 10, mwaka 2019, akajikuta akichungulia kaburi bila kutazamia.

Anasimulia kwamba siku hiyo, akiwa na mashine ya kukatia tiketi kwa njia ya kielektroniki (EFD) mkononi mwake, alianza kukusanya ushuru wa magari yanayoegeshwa katika eneo hilo la Msamvu asubuhi hiyo kama kawaida.

“Nilikuwa nakusanya ushuru wa magari kama kawaida yangu, mara madereva wawili wa bodaboda wakanifuata na kuniambia: ‘Chen itabidi uende kwenye ajali, dereva aliedondoka kwenye ile ajali anahitaji msaada na anataja jina lako.

Ndipo ikanibidi nipande bodaboda huku nimeshika mashine yangu ya EFD mkononi. Nilikuwa ninajiuliza huyo anayetaja jina langu pengine ananifahamu.

“Nilipofika eneo la ajali nikakuta watu wanne wanamwokoa huyo dereva. Baada ya kumuokoa na kutoka nje ya gari alianza kuwaambia watu waache waliokuwepo akitahadharisha kwamba kuiba mafuta gari litalipuka.

“Baada ya dereva kuona watu hawamsikilizi alianza kukimbia kusikojulikana, ndipo na mimi ilibidi niondoke eneo lile. Nikasogea umbali wa hatua 30 kisha nikachukua simu yangu ili nipige watu picha walivyokuwa wanagombania kuiba mafuta.

“Ghafla nilisikia kishindo cha moshi mkali uliokuwa na moto unanifuta nilipo. Kutahamaki nikajikuta ninaaanza kuungua. Ilibidi nitupe simu yangu, chini pamoja na mashine ya EFD na kuanza kukimbia katika uelekeo ambao sikujua ninapokwenda,’’ Chen anasema.

Anasema licha ya kukimbia, moto uliendelea kumfuata na kumuunguza vibaya sehemu ya mgongoni na usoni. Kwa bahati sehemu alipotokea wakati akiendelea kukimbia alipatiwa msaada na dereva mmoja wa bodaboda na kisha kufikishwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro huku akiwa amepoteza fahamu.

“Fahamu ziliponirudia nilijikuta niko hospitalini huku vitanda vingi vya majeruhi wenzangu wa moto vikiwa vimenizunguka,” anasema. Chen anasema ukiwa ni mwaka mmoja leo tangu mkasa huo utokee, bado kumbukumbu za tukio hilo ni ‘mbichi’ kwenye kichwa chake utadhani ni tukio la jana.

Anasema aliposikia kwa mara ya kwanza kuhusu ajali hiyo, hakupanga kabisa kwenda kushuhudia lakini alipoombwa kwenda kutoa msaada kwa dereva ndipo akaamua kwenda.

“Madereva bodaboda wale wawili walinifuata kwa pamoja, wakaniuliza kwamba wewe si mkata ushuru? Basi yule dereva kwenye lile gari lililopata anaita jina lako. Hebu nenda kwanza.

Bila kuniambia hivyo wala nisingekwenda,” anasema. Chen anaamini kwamba juhudi zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano zimechangia kwa kiasi kikubwa watu wengi waliounguzwa moto kwenye ajali hiyo akiwemo yeye kupona kutokana kuamua kugharamia matibabu yote.

“Naipongeza Serikali kwa dhati kabisa namna ilivyojitoa kwa ajili yetu, hatujui ni gharama kiasi gani ilitumia ili kuhakikisha majeruhi wote tunapona japo sio wote tuliopona ila baadhi yetu tumepona.

Tena katika kipindi chote cha zaidi ya miezi minne za matibabu, gharama za chakula na na mavazi zilikuwa pia juu ya Serikali. “Ninakiri kwamba, kama siyo serikali wengi wetu tusingeweza kumudu gharama hizo.

Jeshi la Wanachi nalo lilikuwa msitari wa mbele kuhakikisha tunapatiwa matibabu. Vilevile Jeshi lilisaidia kuzima moto kwenye eneo la ajali. Ninalishukuru sana,’’ anasema.

Mbali na kugharimia matibabu yao, chakula na mavazi wakati wakiwa hospitalini, Serikali pia iliwaandalia utaratibu maalumu wa kuwasaidia majeruhi hao walionusurika kwenye ajali hiyo kwenda kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kila mwezi na kupatiwa shilingi 50,000 kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Malengo ya msaada huo ni kuwawezesha waathirika hao kujikimu kimaisha na kujipanga upya. Chen anamshukuru pia mwajiri wake, TARURA kwani licha ya kutoweza kufanya kazi kwa zaidi ya miezi sita hakusitisha mshahara wake.

Ingawa hajapona na kurudi timamu kwenye hali yake ya kawaida, mtoza ushuru huyo anashukuru kazi anayoifanya sio ya kutumia nguvu kubwa zaidi ya kutumia akili, hali inayomfanya aendelee kuifanya vizuri na hivyo kutimiza wajibu wake vyema.

Wito anaotoa kwa Watanzania ni kuacha mara moja tabia iliyozoeleka ya kuiba mafuta pale malori ya mafuta yanapopata ajali.

Anakemea pia tabia ya baadhi ya watu kuataka kujinufaisha na ajali hata kama si ya malori ya mafuta kwa kuwapora majeruhi badala ya kuwasaidia. Anawaomba wananchi kwamba ikitokea ajali machoni mwao watoe taarifa haraka kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na siyo vinginevyo.

 

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Khalif Mwenyeheri

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi