loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tukumbuke maslahi mapana ya taifa tukielekea Oktoba 2020

FUKUTO la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani linazidi kushika kasi huku wagombea wa kiti cha urais wakiwa wameshachukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wakati hilo likikamilika, wagombea ubunge na udiwani nao wataanza kuchukua fomu katika majimbo yao na kata ili kujiandaa na kampeni zitakazoanza Agosti 26 hadi Oktoba 27 mwaka huu.

Hiyo ndiyo faida ya uchaguzi mkuu katika mfumo wa vyama vingi ambapo kila chama kinajiandaa kwenda kunadi Ilani na Sera zake kwa wananchi ili kupata ridhaa ya kuongoza nchi.

Jambo la msingi kati ya hayo yote ni ule umuhimu wa vyama vya siasa na wagombea wa ngazi zote kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na utulivu kipindi chote cha kampeni, wakati wa kupiga kura, wakati wa kusubiri matokeo, wakati wa kutangazwa matokeo na wakati wa kuapishwa kwa mshindi wa kiti cha urais.

Tunaamini kwamba siasa na uchaguzi siyo vita, shari au ugomvi, bali ni mambo tunayohitaji katika kupata viongozi bora kwa ustawi wa taifa na nchi yetu.

Ni vyema basi kwa vyama vyote na wagombea wake kuepuka lugha za uchochezi, matusi, kashfa, dharau, kejeli, kubeza na kutumia uongo katika kutafuta kura ili kulinusuru taifa na vurugu za aina yoyote.

Kwa kuwa na utamaduni wa kunadi sera wala si matusi na uongozi kutasaidia kuwapa nafasi wananchi kupima safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa juu na pia kuwa vinara duniani katika masuala yanayohusu umoja na amani.

Ili Tanzania iendelee kutunza heshima yake ya kuwa kisiwa cha amani na utulivu na mfano bora wa amani duniani, tunatoa wito pia kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutofumbia macho aina yoyote ya ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi utakaofanywa ama na chama au mgombea yeyote.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ihakikishe inafuatilia kwa karibu kampeni hizo ili kujiridhisha kama vyama, wagombea na wafuasi wao wanazingatia dhana nzima ya amani na utulivu wa Taifa letu.

Tunaamini kwamba kama wanasiasa wakizingatia utaratibu wa kunadi sera kwa heshima wakiacha wananchi wapembue wenyewe chuya na mchele Taifa hili litaendelea kuwa na sifa yake ya amani na utulivu.

TAIFA linaomboleza vifo vya watoto 10 wa Shule ya Msingi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Habari Nyingine