loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uchimbaji bati kurejea Kyerwa Septemba

SHIRIKA  la Madini Nchini (Stamico) litaanza kununua madini ya bati wilayani Kyerwa mkoani Kagera ifikapo Septemba ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kuchimba tena baada ya kuyakimbia machimbo kwa miezi saba.

Hayo yamebainishwa na  Waziri wa Madini, Doto Biteko alipozuru mgodi wa bati maarufu kama tini, wilayani Kyerwa na kukuta shughuli za wachimbaji 200 zimesimama huku ajira zaidi ya 4,000 zikiwa zimesimimishwa.

Mwaka 2019 serikali ilifungua soko la madini hayo katika tarafa ya Kaisho  yalipo madini hayo. Hatua hiyo ilikuja baada ya mwekezaji kujenga kiwanda cha kuongeza thamani madini hayo yaliyopigwa marufuku kusafirishwa nje ya nchi bila kuongezewa thamani.

Kwa mujibu wa wachimbaji, ni miezi zaidi ya saba sasa kukiwa hakuna anayefika katika soko hilo kununua madini jambo lililowafanya wachimbaji kukimbia na kuacha machimbo na shughuli nyingine za kibiashara zikiwa zimesimama.

Akiwa wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Rashidi Mwaimu alimwambia Waziri Biteko kuwa, kwa sasa kuna tani 47,000 ambazo hazijanunuliwa na zimepimwa na kuwekwa stoo huku kukiwa hakuna anayeendelea na uchimbaji.

Waziri Biteko amewahakikishia kuwa, serikali itanunua madini yao ifikapo Septemba na kuwahimiza kurejea katika shughuli zao za uzalishaji.

Katika ziara hiyo, Biteko alimtembelea mwekezaji wa kuongeza thamani ya madini hayo Tanza Plus, Salimu Mhando aliyesema kuna kipindi alinunua madini hayo kwa wingi akaongeza thamani na baadaye yakashuka bei katika soko la dunia hali iliyomsababishia hasara.

Alibainisha kuwa, baada ya kuwekeza katika teknolojia ya kuongeza thamani ya madini hayo, mtaji wake umepungua hivyo anajipanga ili kuurejesha na kununua tena madini hayo.

Amesema kiwanda chake kina uwezo wa kuongeza thamani kwa tani 1,200 kwa mwezi na kwamba akipata mtaji, anaweza kununua madini yote ya wachimbaji na kiwanda chake kinaweza kutumika kuongeza thamani ya madini hayo kwa nchi zote zinazouza madini hayo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo mkoani Kagera (Karema), Osward Makanzu, kwa upande wake amesema  hadi sasa zaidi ya wachimbaji 4,000 waliokuwa katika mgodi huo hawajulikani wanafanya shughuli gani nyingine.

Amesema  endapo mnunuzi atapatikana, wanachi wanaweza kuchimba madini mengi zaidi kutokana na tafiti zilizofanyika awali kuonesha uwepo wa kiasi kikubwa cha bati.

Mmoja wa wachimbaji wadogo aliyechimba kwa miaka saba, Jakson Kachumis, amesema serikali imepoteza mapato mengi katika kipindi ambacho wachimbaji wamesimama uchimbaji.

Aidha Kachumis ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kupeleka umeme katika mgodi huo kwa kuwa zana  wanazotumia katika uchimbaji ni za zamani na wanashindwa kutumia mitambo ya uchimbaji kutokana na kutokuwepo kwa umeme.

SERIKALI imezindua Mpango Mkuu ...

foto
Mwandishi: Diana Deus, Kyerwa

Post your comments

Habari Nyingine