loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Balozi Ruhinda: Ben Mkapa alikuwa na sifa zote nzuri za binadamu

FERDINAND Kamuntu Ruhinda, Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa Siasa, Mhariri na Balozi wa Tanzania katika nchi za Canada na China, alikuwa rafi ki wa karibu wa Benjamin Mkapa, Rais wa Tatu wa Tanzania, aliyefariki dunia Julai 23, mwaka huu na kuzikwa Julai 29 kijijini kwao Lupaso mkoani Mtwara.

Baada ya mazishi, Mzee Ruhinda, aliamua kutoa ushuhuda hadharani kuhusu rafi ki yake wa zaidi ya miaka 50. Hii ni sehemu ya kwanza ya ushuhuda huo unaotolewa katika sehemu tatu.

“Nimewaombeni mje kunisikiliza. Mnisaidie. Nataka kutoa ushuhuda, hadharani, kuhusu Benjamin Mkapa, rafiki yangu, ndugu yangu.” Hayo ndiyo yali- kuwa maneno ya ufunguzi ya Balozi Mzee Ferdinand Ruhinda katika mazungumzo yake wiki iliyopita na waandishi wa habari watatu waandamizi.

“Kifo chake kimenisikitisha na kunihuzunisha sana. Sina maneno sahihi na mwafaka kuelezea huzuni na masikitisho yangu. I will miss him. I will miss him very much.

Tulikuwa familia. Nilipopata matatizo ya kuugua, alinisaidia sana. Binafsi, kwa kweli amenisaidia mno, na mambo mengine siwezi hata kuyasema hadharani.

Sitaki kujenga tahayari kwa watu wengine. Sikuweza kushiriki kuuaga kimwili katika msiba, lakini baada tu ya msiba kutokea nimezungumza na mke wake,” anasema Balozi Ruhinda na kuongeza: “Siku moja kabla ya kifo chake, Ben alikuja kuniona, kama ambavyo ilikuwa kawaida yake ya kuja kuniona.

Alikuwa na utaratibu wa kuja kunijulia hali kila wiki hapa nyumbani. Alikaa hapo mlipokaa nyie. Hakukaa sana. Alikuja kunieleza yaliyokuwa yamejiri katika Mkutano Mkuu wa CCM kule Dodoma. Akaniambia pia wakati yuko Dodoma alikuwa ameshiriki mazishi ya Mzee wetu, Job Lusinde.

Kama nilivyosema, zamu hii hakukaa muda mrefu, kama ilivyokuwa kawaida yake.” Anasimulia zaidi Mzee Ruhinda: “Kwa kweli, ni kama vile alikuja kuniaga. Sikujua kama sitamwona wala kuzungumza naye tena. Aliniambia hajisikii vizuri, anaumwa. Nami nilimwona hali yake, nikamshauri tusikae sana kwenye mazungumzo, bali aende hospitali kujipima afya yake,” alisimulia Mzee Ruhinda, na kukaa kimya kwa dakika tatu hivi, akijaribu kudhibiti na kutuliza hisia zake.

Tangu kutokea msiba, Alhamisi ya Julai 23, mwaka huu, masikitiko na huzuni ya kifo cha Ben, ndivyo vilimfanya Mzee Ruhinda kwanza akae kimya, aomboleze kifo cha rafiki na ndugu yake, na kusubiri mazishi yafanyike kabla ya kutoa ushuhuda wake.

“Sikutaka kushiriki kwenye kneejerk reactions (kauli za hapo kwa hapo na kukurupuka).” Hakuna shaka kuwa Rais wa Tatu wa Tanzania, Mzee Benjamin William Mkapa, katika maisha yake marefu, na utumishi wake wa kutukuta, na wenye shughuli nyingi za umma, alikuwa na marafiki wengi.

Wengine wa miaka mingi, tangu shule, kama vile akina Mzee John Kambona na Mzee Philip Magani, ambao alisoma nao Ndanda na wote bado wanaishi. Hata hivyo, pengine, hakuna mtu alikuwa rafiki wa karibu zaidi (Wahaya wanasema fanfe – yaani marafiki wa kufa pamoja), na aliyeamini naye, kuliko Ferdinand Kamuntu Ruhinda, mtumishi mwingine wa kutukuka na wa miaka mingi wa umma.

“Nilikutana na Benjamin Mkapa kwa mara ya kwanza mwaka 1966, miaka 54 iliyopita, tukiwa bado vijana. Tangu wakati huo, tumekuwa marafiki. Tuliaminiana sana.

Nadhani sitakosea kusema kuwa tangu nijuane naye, haikupata kupita wiki mbili bila kukutana naye, ana kwa ana, ama kuzungumza naye kwa simu, ama kwa mawasiliano ya aina nyingine.

Na msinielewe vibaya, Ben alikuwa na marafiki wengi, na wa karibu, siyo mimi peke yangu,” anasema Balozi Ruhinda. Anaongeza: “Tulikutana katika mazingira ya kazi na tukawa marafiki wa kikazi na nje ya kazi.

Wakati huo mimi nimeajiriwa kama mwandishi wa habari katika Chumba cha Habari cha Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC) wakati huo.” “Yeye, Ben alikuwa anakuja kusoma habari za Kiingereza, wakati wa muda wake nje ya kazi.

Mimi nilikuwa mmoja wa watu waliokuwa wanatayarisha habari. Aliipenda kazi yangu na urafiki wetu ulianzia hapo. Nimemfahamu kwa muda mrefu sana, zaidi ya miaka 50. Kwa kweli, uhusiano wetu ulikuwa zaidi ya urafiki. Tulikuwa ndugu.”

Mzee Ruhinda anakiri kuwa ni vigumu kueleza kwa ufasaha hasa, nini hasa lililowavuta yeye na Mzee Mkapa kuwa marafiki kiasi hicho. “Tulikuwa watu tofauti sana mwanzoni. Sote tukitokea pande mbili tofauti kabisa za nchi… pembezoni mwa nchi.

Mmoja akitokea Kaskazini Magharibi kabisa na mwingine Kusini kabisa mwa nchi yetu. Mmoja anatokea Mto Ruvuma na mwingine akitokea Mto Kagera. Tuliunganishwa hasa na haiba zetu za kimaisha na kisiasa.” Anafafanua zaidi:

“Mwaka mmoja tu, baada ya kuwa nimejuana naye, unaotolewa katika sehemu tatu. “Nimewaombeni mje kunisikiliza. Mnisaidie. Nataka kutoa ushuhuda, hadharani, kuhusu Benjamin Mkapa, rafiki yangu, ndugu yangu.”

Hayo ndiyo yali kuwa maneno ya ufunguzi. nilijiunga na Gazeti la Nationalist lililokuwa linachapishwa pamoja na Gazeti la Kiswahili la Uhuru, ambako yeye alikuwa Mhariri Mtendaji. Nikafanya kazi chini yake, kwanza nikiwa Msanifu Habari (Sub-Editor), na baadaye kama Mhariri wa Habari (News Editor).”

“Utaona kuwa urafiki wetu ulianzia kwenye shughuli za uandishi wa habari. Urafiki wetu pia ulikuwa wa kisiasa. Kama mnavyojua nyie, uandishi wa habari hauna tofauti kubwa na siasa.

Baadaye, mwenzangu akaingia moja kwa moja kwenye siasa. Mimi nikabakia kwenye uandishi wa habari, lakini urafiki wetu ukabakia pale pale na kuzidi kukomaa,” anasema Mzee Ruhinda.

Kwa sababu ya haiba na tabia yake kuu ya kukataa kusijifu, wala kujitukuza, Mzee Ruhinda anakomea hapo kusimulia maisha yake binafsi. Lakini, alikuwa ni yeye alimyemrithi Mkapa katika nafasi ya Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Chama (TANU) mwaka 1972, wakati Mkapa alipoteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Serikali, baada ya kutaifishwa kwa Gazeti la The Standard kutoka kampuni ya kigeni ya LONRHO (London- Rhodesia), iliyokuwa inamilikiwa na mfanyabiashara maarufu wa Kiingereza, Tiny Rowlands. Baadaye, mwaka 1976, Ruhinda alimrithi tena Mkapa kwenye nafasi ya Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Serikali ya Daily News na magazeti dada.

Kuanzia kwenye miaka ya mwanzo ya 1980 mpaka alipostaafu utumishi wa umma, Mzee Ruhinda akafanya kazi chini na kwa karibu na Mzee Mkapa katika nafasi za Naibu Balozi wa Tanzania Sweden, na Balozi katika Canada na katika Jamhuri ya Watu wa China.

Uteuzi wa Mzee Ruhinda kutumikia katika nafasi ya juu kabisa ya uwakilishi wa Tanzania kwenye nchi ambazo zilikuwa na uhusiano mzuri, wa karibu sana, na wa miaka mingi na Tanzania, unathibitisha jinsi Mzee Mkapa pia alivyomuamini Balozi Ruhinda.

Kwa maana ya kwamba, hata kama Mzee Mkapa yeye hakumteua moja kwa moja Mzee Ruhinda kushika nafasi hizo, bado uteuzi huo usingefanywa na marais JK Nyerere na Ali Hassan Mwinyi, bila ushauri na ushawishi wa Mzee Mkapa, akiwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Balozi Ruhinda anasema kuwa hawezi kumsemea Hayati Mkapa kwenye kila eneo kwa sababu, kwa bahati nzuri, Rais huyo mstaafu amejisemea mwenyewe vizuri katika Kitabu chake cha My Life, My Purpose, kilichozinduliwa miezi minane kabla ya mauti yake.

Lakini Mzee Ruhinda anamwelezea Mzee Mkapa ifuatavyo: “Nataka kusema kile ambacho hakukisema katika kitabu chake kwa sababu ya tabia yake ya kukataa kujikweza.

Ben alikuwa mtu na binadamu kamilifu, kwa kadri inavyowezekana kwa binadamu. Kila sifa nzuri ya binadamu, Benjamin Mkapa alikuwa nayo,” anaeleza Mzee Ruhinda na kuongeza: “Wapo watakaosema kuwa namsifia Ben kwa sababu alikuwa rafiki yangu. Kweli, Ben alikuwa rafiki yangu. Lakini urafiki wetu haufuti ama kuondoa sifa zake nyingi.

Ben aliheshimu sana fikra tofauti na zake, hata kama hakukubaliana nazo. Hii ni sifa ambayo haijitokezi vizuri katika kitabu chake.” “Ben alikuwa humble, mnyenyekevu, asiyependa makuu. Wapo wanaosema kuwa alikuwa na jeuri na kiburi cha usomi (intellectual arrogance). Kwangu mimi, madai hayo ni tofauti tu ya mawazo na maoni binafsi ya watu (difference of opinion).” Anaongeza Mzee Ruhinda:

“Sifa ya kuheshimu tofauti ya mawazo ni sifa muhimu sana kwa kiongozi. Sifa hii, inafaa kwa viongozi wetu wa sasa na wajao. Ni muhimu waikubali sifa hiyo na kuiiga. Dunia hii, watu tuko wengi, na ili tuishi pamoja na kwa amani, ni lazima tuheshimiane, hata kama hatukubaliani.

Huu ni wajibu mkubwa zaidi kwa viongozi kwa sababu wao ndio kioo cha jamii.” Mzee Ruhinda anasimulia kuwa wala tabia ya Mkapa kuheshimu mawazo tofauti haikuanza aliposhika nafasi za juu za uongozi. Anasema kuwa tabia hiyo, alikuwa nayo maisha yake yote:

“Sijui kama jambo hilo naweza kulisema vizuri, ili nieleweke ipasavyo: Akiwa Mhariri wa Magazeti ya Chama na Serikali, akiwa Waziri, akiwa Balozi na akiwa Rais, Benjamin Mkapa alihimili na kuvumilia mawazo na maoni tofauti. Hata kwenye uvumilivu wake, yapo mawazo na maoni aliyakubali, na yapo mengine aliyakataa.

Kubwa ni kwamba hata aliyoyakataa hayakuwa chanzo cha chuki kwa waliyoyatoa. Ndiyo maana wakati wa utawala wake, viongozi wa vyama vya upinzani walipata fursa ya kufanya kazi zao vizuri na hata magazeti yalipanuka sana.”

“Kwake yeye, mawazo tofauti hayakuwa chanzo cha uadui wala chuki. Hiyo ndiyo ilikuwa tabia na hulka yake ya maisha. Hiyo ndiyo principle, yaani msingi mkuu wa mahusiano yake na binadamu wenzake. Na hilo ndilo urithi mkuu anayowaachia wanasiasa na viongozi wa sasa na wajao wa nchi yetu.” .

Mzee Ruhinda anasema kuwa hata wao kama marafiki hawakukubaliana kuhusu kila kitu pamoja na kuwa na tabia ya kujadili mambo mbali mbali kila walipokutana.

Anafafanua: “Muda mwingi tulijadili mambo mbali mbali. Mengine tulikubaliana na mengine tulitofautiana. Jambo moja, kwa mfano, ambalo tulitofautiana wakati wote ilikuwa kuhusu madaraka ya Rais, na hasa uteuzi wa watu kushika nafasi mbali mbali. Mimi niliamini na naamini kuwa Rais anateua watu wengi mno na hakuna utaratibu mzuri wa kumsaidia kuwachuja.

Anateua Baraza la Mawaziri, anateua ma-RC, anateua ma-DC. Wote karibu kutoka chama chake.” Anaendelea: “Iko siku moja, alimteua mtu mmoja kuwa mbunge.

Simtaji jina. Mimi nikamwendea na kumwuliza ‘je unamjua vizuri mtu huyo’. Naye akasema kuwa alikuwa hamjui vizuri. Mimi nikamweleza nilivyokuwa namjua yule mtu. Ben alisikitika sana.

Lakini maji yalikuwa tayari yamemwagika.” “Siyo lazima tuwe na Katiba mpya kubadilisha jambo hili. Lakini ni jambo lina uwezekano wa hatari kubwa. Tumeona katika nchi za jirani, marais wakiteua wake zao kuwa mawaziri,” anasisitiza Mzee Ruhinda.

Hata hivyo, tulikubaliana kuhusu mambo mengi. Jambo moja ambalo tulikubaliana wakati wote ni kuhusu Muungano na muundo wake. Tulikubaliana kuwa nchi yetu haikuwa na msisitizo wa kutosha kuhusu Muungano.

Pamoja na kwamba nchi yetu ni moja sasa, bado kuna watu wengi ambao bado wanazo hisia za Uzanzibari na Utanganyika. Tunahitaji kuongeza nguvu katika kubadilisha hisia hizi kwa sababu nchi hii sasa ni moja. Zilikuwa nchi mbili mwaka 1964, miaka 56 iliyopita.

Anaongeza kwa nini ameteua kulisisitiza jambo hili. “Nalisema hili kwa sababu ni jambo muhimu sana kwa ustawi wa taifa letu na hii ni mara yangu ya mwisho kufanya mahojiano na waandishi wa habari.”

“Kwangu mimi siyo tu kwamba Benjamin Mkapa alikuwa rafiki yangu. Lakini nimeishi naye, na nimeshuhudia na nilizipenda tabia zake nzuri na sifa zake nyingi.

Aliongozwa sana na utu. Alikuwa mpole. Kweli, pia alikuwa mkali, lakini hizo zote ni tabia nzuri tu za binadamu. Hata ukali si tabia mbaya, hasa ikiongozwa na utu, upole na haki, kama ilivyokuwa kwa Benjamin Mkapa.

Aliongoza nchi vizuri na kwa misingi thabiti ya haki.” Mzee Ruhinda pia anazugumzia suala jingine ambalo Mzee Mkapa alilizungumza katika kitabu chake, “utawala wa nchi yetu na misingi ya chaguzi zetu.”

Siku zote, mjadala umekuwa kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi. Kwangu mimi, suala kubwa si kuwepo ama kutokuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Kwangu mimi, muhimu ni kuwepo kwa chombo ama vyombo vinavyoaminiwa na wananchi na jamii, vilivyojengwa katika misingi ya utamaduni wetu, ili chaguzi zetu zikubaliwe na wananchi, zidumishe amani, na zisilete misuguano katika jamii.” Anafafanua,

“Hili ndilo jambo la msingi. Kuwepo kwa chaguzi za haki na zinazokubaliwa na wananchi, kwa sababu hata huko nchi za Magharibi hakuna kitu kinachoitwa Tume Huru za Uchaguzi.

Lakini utamaduni wa nchi hizo, umejengeka kiasi cha kuruhusu chaguzi zao kukubaliwa na wananchi na matokeo ya chaguzi hizo kutokuzusha mivutano isiyokuwa ya msingi.” Maoni yangu, anasema Mzee Ruhinda, ni wajibu wa Tume ya Uchaguzi kufanya kazi vizuri na kwa uwazi, na kujenga mazingira ya chaguzi za haki ambako wananchi wanapata taarifa nzuri, za kutosha na kwa wakati.

“Chukua mfano wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Uchaguzi Mkuu wa kwanza baada ya siasa za vyama vingi kurejeshwa nchini. Wakati wa kampeni ya uchaguzi ule, uliandaliwa mdahalo baina ya wagombea. Lakini mdahalo ule uliandaliwa na gazeti moja, na wala siyo na Tume ya Uchaguzi,” anasema Mzee Ruhinda na kuongeza: “Lakini tangu wakati ule, haujapata kuandaliwa mdahalo mwingine, na kwa maoni yangu, hiyo ni sehemu muhimu ya kazi za Tume ya Uchaguzi, yaani kuwawezesha wananchi wawajue vizuri wagombea wao, misimamo yao kuhusu masuala mbali mbali na maandalizi yao ya kuongoza nchi.

Uwazi wa namna hiyo utasaidia kujenga mazingira ya chaguzi zetu kuaminiwa zaidi na wananchi.” Anamalizia Mzee Ruhinda: “Napenda nimalizie kwa kutoa tena pole nyingi, na rambirambi za dhati ya moyo wangu, kwa familia ya Ben Mkapa  kwa mama na watoto na wajukuu na ndugu zake wote na pia kwa marafiki zake wengi na wote.

Nimefurahishwa na jinsi taifa letu lilivyomuaga na tulivyomsindikiza Ben Mkapa. Ameagwa kwa heshima na taadhima. Kwangu mimi, I Will Miss Him. I Will Miss Him Very Much! •

 

Waandishi wa makala haya ni waandishi waandamizi nchini. Kwa sasa Salva Rweyemamu na Saidi Nguba wanaongoza Kampuni ya Mawasiliano ya Pioneer Communications na Tido Mhando ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Habari ya Azam Media. Usikose sehemu ya pili ya makala haya: Uongozi wa Mkapa na Uchaguzi Mkuu wa 1995 na nafasi za Jakaya Kikwete, Salim Ahmed Salim na Augustine Mrema katika uchaguzi huo.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Salva Rweyemamu, Saidi Nguba na Tido Mhando

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi