loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Alama ya kudumu aliyoiacha Mkapa kwa 'wajukuu' Kusini

KABLA ya miaka ya 2000, wananchi wa mikoa ya kusini (Lindi na Mtwara) walikuwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara iliyosababisha usumbufu na kuwakosesha fursa za maendeleo ikiwemo uwekezaji.

Historia ya nchi inadhihirisha hili, kwani mikoa hiyo kwa muda mrefu imekuwa nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na mikoa mingine, hali ambayo sasa inaondoka hatua kwa hatua baada ya kufunguka kwa miundombinu inayoiunganisha mikoa hiyo na mingine, likiwamo Daraja la Rufiji maarufu pia Daraja la Mkapa.

Daraja hilo lenye urefu wa meta 970.5 lilizinduliwa Agosti 2, mwaka 2003 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa aliyoitoa mwaka 1998 ya kuunganisha mikoa ya kusini na mikoa mingine pamoja na nchi jirani. Lengo la Mkapa lilikuwa ni kurahisisha ufanyaji wa biashara kati ya wananchi wa mikoa ya kusini na maeneo mengine ndani na nje ya nchi na kuchochea uwekezaji.

Daraja hilo liligharimu Dola za Marekani milioni 30 (zaidi ya Sh bilioni 65 kwa wakati huo) na kwa hakika, wakazi wa mikoa hiyo baada ya kifo cha Mkapa, wanalielezea daraja hilo kama alama muhimu ya urithi aliyowaachia na watakayomkumbuka nayo vizazi baada ya vizazi.

Mwandishi wa makala haya, alipata fursa ya kuhudhuria maziko ya Rais Mkapa Kijijini Lupaso, wilayani Masasi, mkoani Mtwara ambapo alizungumza na watu mbalimbali wakiwamo wananchi wa kawaida na viongozi kuhusu Mkapa.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa anamuelezea Mkapa kwamba alikuwa mtu msikivu, alama ya mageuzi ya kiuchumi, mnyenyekevu na mwenye busara na hekima nyingi aliyekuwa radhi kubadili ratiba yake wakati alipostaafu na kumpa mtu muda wa kumsikiliza.

"Mimi binafsi ni mnufaika mkubwa wa hekima za Mkapa, ni mtu aliyeweza kubadili ratiba yake ili akusikilize, mimi mara nyingi alinipa fursa hii ya kunisikiliza,” anasema Byakanwa.

Anasema kuwa wananchi wa Mtwara na mikoa ya kusini kwa ujumla watamkosa sana Mkapa lakini wataenzi mazuri aliyowatendea ikiwamo kupatikana kwa Daraja la Mkapa lililopo Ikwiriri, mkoani Pwani.

Byakanwa anasema kabla ya daraja hilo, wananchi wa mikoa hiyo walipata mateso makubwa safarini na kwamba abiria walishazoea kutumia siku tatu, nne mpaka wiki moja kutoka Mtwara au Lindi kwenda Dar es Salaam na mikoa mingine inayolazimu kupita eneo la mto Rufiji.

Anakiri kwamba, sasa hali ya kiuchumi na ustawi wa maisha ya wakazi wa kusini imebadilika. Anasema zipo fursa nyingi za uwekezaji na shughuli za kibiashara zimeshamiri na hivyo kuwaalika wawekezaji zaidi kwenda kuwekeza mkoani Mtwara kwani ni salama na panafaa sana.

Ujasiri wa Byakanwa anadai unatokana na uwepo wa Daraja hilo la Mkapa. Mwanakijiji wa Lupaso, Mohamed Kitambi, anasema Mkapa amewatangaza watu wa kusini kimataifa kwani Daraja la Mkapa limebeba jina la mwanakijiji mwenzao na limetokana na nguvu zake, hivyo watamuenzi milele.

Anasema vizazi baada ya vizazi vitakuta alama hii isiyofutika na kwa uhakika, maendeleo yanayoendelea kupatikana kusini, yametokana na chachu ya daraja hilo.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Lupaso wakati Mkapa akiwa Rais, Athanas Luchapa, anasema Mkapa alipokuwa madarakani alifanya mengi ya kitaifa na kwa kijiji hicho pia.

Anasema pamoja na kushiriki kukarabati Kituo cha Afya cha Lupaso (cha Kanisa) ili wanakijiji akiwamo na yeye, wapate huduma kwa karibu na haraka, aliondoa kilio cha wananchi wa kusini kwa kutimiza ahadi yake ya kuwajengea daraja (Daraja la Mkapa).

“Tulikuwa tukiongea mara kwa mara akiniambia sitatibiwa Ndanda (Hospitali ya Misheni) bali hapa hapa kijijini, hivyo alikiangalia kituo hiki cha afya kwa jicho la tofauti sana," anasema Luchapa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, anasema Mkapa alikuwa kiongozi jasiri, aliyetumia busara na hekima alizojaaliwa kuijenga nchi na wananchi.

Zambi anasema Lindi watamuenzi kwa kuwezesha miundombinu iliyobaki kama alama kwao likiwamo Daraja la Mkapa ambalo sasa linatumika kama sehemu ya utalii lakini pia limefungua njia ya kurahisisha uwekezaji na maendeleo kwa watu wa kusini.

Diwani wa Lupaso ambaye ni mtoto wa mdogo wa Mkapa, Doglas Mkapa, anasema amekuwa diwani kwa miaka mitano iliyopita katika Kata hiyo na hivi karibuni amepita bila kupingwa katika kura za maoni ikiwa ni matokeo ya kufuata nyayo za uongozi za baba yake mkubwa, Hayati Mkapa.

Anasema Mkapa amelitumikia taifa na kutatua kero za watu wengi ikiwemo kufungua fursa za uwekezaji na kujenga miundombinu. Anasema aliwajenga wengi kuwa viongozi bora na yeye (Doglas) ni miongoni mwa watu waliojengwa na Mkapa.

Aliyekuwa Mpambe (ADC) wa Rais Mkapa kwa miaka 10, Brigedia Jenerali mstaafu, Augustine Gailanga, anasema yeye kama ilivyo wananchi wa kusini na Watanzania wengine, amejifunza mengi kwa Mkapa ikiwamo nidhamu, busara, hekima na kutafakari kabla ya kuamua jambo linalogusa maslahi ya taifa.

Nao wafanyabiashara wa maduka, nyumba za kulala wageni na waendesha pikipiki za kubeba abiria maarufu kama bodaboda mjini Masasi wanasema watamkumbuka Rais mstaafu Mkapa kwa kusaidia kujenga miundombinu ikiwamo ya barabara iliyochochea kushamiri kwa biashara wilayani humo.

Dereva wa bodaboda katika Stendi ya mabasi Masasi, Issa Shaibu, anasema Mkapa alikuwa ni taa ya watu wa Kusini, walijivunia yeye na alifanya mengi ikiwamo kujenga barabara na kuwezesha ujenzi wa daraja la Mkapa lililofungua njia kwa kuunganisha mikoa mingi na mikoa ya kusini na kuifanya Masasi ichangamke kibiashara.

Yapo mengi aliyofanya Mkapa yanayoleta mapinduzi ya uchumi nchini na hili la Daraja la Mkapa ni moja ya mambo makubwa mengi aliyofanya Mkapa enzi akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu.

WAKATI Rais John Magufuli ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine