loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tari-Kibaha na ukuzaji uchumi kupitia sukari

“Tumia teknolojia za kilimo na utawala bora kwa ukuaji wa uchumi wa viwanda.” Hii ndiyo kaulimbiu iliyotumika katika Siku ya Mkulima iliyoandaliwa katika Kituo cha Taasisi ya Utafi ti wa Kilimo Kibaha (Tari Kibaha), mkoani Pwani.

Kaulimbiu hiyo inawakutanisha watafiti na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa zao la miwa. Kupitia kaulimbiu hiyo, mkulima Lejino Nyavenga kutoka Bonde la Kilombero Ukanda wa Luhembe mkoani Morogoro, anaeleza anavyotumia teknolojia na mbegu bora kutoka Kituo cha Kibaha.

Teknolojia hiyo imemwezesha yeye na wenzake kupata mavuno bora kutoka tani 15 kwa ekari moja hadi kufikia tani 50. Nyavenga mwenye shamba la ekari 35 anasema kupitia kaulimbiu hiyo, sasa anauona uchumi wa viwanda nchini kwa kuwa kilimo kimeboreka kutokana na kupata ushauri, teknolojia na mbegu bora kutoka kwa watafiti wa kilimo.

“Tari-Kibaha wanatusaidia sana kupata mbegu bora kutokana na hali halisi ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha magonjwa mbalimbali,” anasema.

Anasema, Tari-Kibaha pia imewawezesha kuboresha kipato kutokana na elimu wanayoipata na kwamba, kabla ya mafunzo hayo, katika ekari moja mkulima alipata kati ya tani 15 na 25, lakini baada ya mafunzo wakulima waliozingatia teknolojia wanapata wastani wa tani 50 au zaidi.

Anasema kituo hicho kimetoa mwanga na dira kwa wakulima hali iliyowawezesha kuona ubora wa kilimo cha miwa kwa kuwa wamewekewa mazingira mazuri ya upatikanaji wa pembejeo.

Hata hivyo, wanaitaja changamoto inayowakabili kuwa ni utaratibu wa uvunaji kutokuwa sawa hivyo kupendekeza uvunaji ufanywe kiukanda tofauti na hali ilivyo sasa. “Tunashauri kuwe na mizani ya nje ambayo atakaa mwekezaji na mkulima ili kupata matokeo halisi tofauti na sasa miwa kupimiwa kwa mwekezaji bila kuwepo mkulima,” anasema.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga anasema, sekta ya sukari inahitaji kasi kubwa ya uwekezaji kutokana na ukweli kuwa nchi ina mahitaji makubwa ya sukari ikilinganisha na kiasi kinachozalishwa.

Anasema mahitaji ya sukari nchini yamekuwa yakibadilika mwaka hadi mwaka kulingana na hali ya mahitaji kwa mwaka husika. “Mathalani, msimu wa uzalishaji wa mwaka 2019/2020 mahitaji ya sukari yalikadiriwa kuwa tani 710,000.

Kati ya hizo, tani 545,000 ni sukari ya matumizi ya kawaida na tani 165,000 ni kwa matumizi ya viwandani. “Makadirio ya uzalishaji wa sukari kwa viwanda vyote nchini kwa mwaka 2019/2020 ulikuwa ni tani 378,449 sawa na asilimia 67.7 ya sukari inayokadiriwa kwa matumizi ya kawaida, na hivyo basi, kuwa na upungufu wa sukari wa asilimia 32.3,” anasema.

Anasema serikali imeweka mikakati madhubuti kuanzia msimu wa mwaka 2020/2021 kuhakikishia nchi inajitosheleza kwa sukari kwa kuviagiza viwanda vya sukari nchini kuongeza uzalishaji.

Tayari Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kimepanga kuongeza mitambo yenye uwezo wa kuchakata miwa kutoka tani za miwa 110 hadi 310 kwa saa, hivyo kuongeza wakulima wadogo kutoka 6,500 hadi 12,000 ambao watachangia ongezeko la sukari kutoka tani 130,000 hadi 265,000.

Aidha, kiwanda cha TPC kimepanga kuboresha zaidi miundombinu ya uzalishaji kwa kuondoa chumvi kwenye baadhi ya sehemu ili kuongeza uzalishaji kutoka tani 91,400 hadi tani 104,399.

Nacho kiwanda cha sukari cha Kagera kinaimarisha uzalishaji wa kilimo cha miwa cha umwagiliaji na kuboresha uwezo wa kiwanda kuchakata miwa kutoka tani 75,569 mpaka kufikia tani 99,500. Kiwanda cha sukari Mtibwa kina mpango wa kuongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 31,139 mpaka tani 65,000.

Hasunga anasema, serikali imeweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kuzingatia fursa zilizopo za uzalishaji sukari ikiwemo ardhi nzuri na mahitaji makubwa ya soko hususani la ndani.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa mitaji katika sekta ya sukari kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya uzalishaji. “Miradi hiyo ni pamoja Mkulazi I na Mkulazi II mkoani Morogoro, uanzishwaji wa viwanda vya sukari katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo Chamwino (Dodoma), Geita, Kasulu (Kigoma), Rufiji (Pwani), Songea (Ruvuma) na Bagamoyo (Pwani),” anasema.

Hivyo kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya sukari, viwanda na wakulima wa miwa, Tari-Kibaha inafanya tafiti mbalimbali katika zao la miwa zinazojibu changamoto za wakulima na wenye viwanda.

Meneja wa Kituo cha Tari- Kibaha, Dk Hildelitha Msita anasema wanahakikisha wakulima wanapata mbegu bora zenye uzalishaji wenye tija kulingana na maeneo na hali ya hewa husika.

“Hii itawezekana kwa kuwa na uzalishaji wa mbegu kupitia njia ya chupa na kwa kutumia vikonyo,” anasema. Tari-Kibaha pia inaanzisha vitalu MAKALA Tari-Kibaha na ukuzaji uchumi kupitia sukari vya mbegu kuwezesha wakulima kupata mbegu karibu na maeneo ya uzalishaji na kutoa elimu ya kilimo bora cha miwa kupitia njia mbalimbali yakiwamo mashamba darasa, simu na vyombo vya habari.

Aidha, kituo kinagundua na kusambaza teknolojia mbalimbali za kudhibiti magonjwa, wadudu na magugu. Ndiyo maana katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2014 hadi 2019, Serikali kupitia Tari imegundua aina tano za mbegu za miwa yaani N30, N41, R 570, R 575 na R 579 zilizothibitishwa kitaifa kwa kilimo cha umwagiliaji.

“Mbegu hizi zina uwezo wa kutoa mavuno mengi ikilinganishwa na mbegu za zamani zilizokuwa zikitumiwa na wakulima na kutoa mavuo ya wastani wa tani 60-160 kwa hekta moja,” anasema.

Pia aina nne za mbegu zinazostahimili ukame ambazo ni TZ93-KA-120, TZ93-KA-122, N47 na R570 zimejaribiwa katika maeneo mbalimbali yanayozalisha miwa ya kutengeneza sukari na kuonesha matokeo chanya.

Zipo katika hatua za mwisho za utathimini. Mkurugenzi Mkuu wa Tari, Dk Geofrey Mkamilo anawataka watafiti wa kilimo kuhakikisha matokeo ya utafiti yanayopatikana yanakwenda kwa wakulima na kuleta tija katika uzalishaji.

Mkamilo anasema, matokeo hayo yawekewe nguvu sambamba na kutangaza matokeo hayo kwani watafiti, “lengo letu ni kuhakikisha tunaongeza tija katika upatikanaji wa sukari,” anasema.

Naye Mwakilishi kutoka Bodi ya Sukari Tanzania, Buzingo Lusomyo anasema wakulima wameongeza uzalishaji kutokana na matokeo ya utafiti yanayolenga kuongeza tija, kufuata kilimo bora cha miwa pamoja na ongezeko la wakulima.

“Wakulima wadogo wana umuhimu, lakini tunaona umuhimu wao ukipewa nguvu na utafiti. Utafiti ukifanyika wa kutosha na matokeo ya utafiti yakazingatiwa, utasaidia kuongeza uzalishaji wa miwa na uzalishaji wa sukari nchini,” anasema.

Anasema japo uzalishaji umeongezeka, bado changamoto ya sukari ipo pale pale. “Uzalishaji umeongezeka, lakini hautoshelezi mahitaji; hili ni jambo ambalo bado tunatakiwa tulitafutie jibu.

Moja la eneo la kupata jibu ni matumizi ya utafiti baada ya utafiti kufanyika ipasavyo. Matumizi ya utafiti yakiwa bora katika maeneo ya wakulima, viwanda na mashamba ya wazalishaji wakubwa, yatasaidia kupunguza ile nakisi,” anasema.

Katibu wa Mfuko wa Maendeleo wa Wadau wa sukari, Dk Nephat Mkula anasema watafiti wamekuwa wakifanya kazi nzuri, lakini nyingi hazitambuliki hivyo anawasihi kutobweteka na matokeo yanayopatikana, bali yalete tija kwa wakulima.

“Lakini watafiti msije kujiona kama wa kawaida sana. Mnachofanya siyo cha kawaida mkitoe nje kule nje wapo hao wakulima, anasema. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Tari, Dk Yohana Budeba anaipongeza serikali kwa kuanzisha taasisi hiyo kwa kuwa imeleta mageuzi ya kilimo nchini kwa kujibu changamoto za wakulima kupitia utafiti unaofanywa.

Anawataka wananchi kutumia teknolojia ambazo watafiti wamezitambua ili kupata tija katika mazao yao. Tasnia hii nchini Tanzania ina viwanda vitano vinavyozalisha sukari, kati ya hivyo vikubwa ni vinne na cha kati kimoja ambavyo ni Kilombero na Mtibwa vilivyopo Morogoro.

Vingine ni Kagera kilichopo mkoani Kagera, TPC kilichopo Kilimanjaro na cha kati ni Manyara kilichopo Manyara

KAMPUNI ya uchimbaji ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi, Bariadi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi