loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

…Ataka wanawake waache umbea

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema ndimi za wanawake zina nguvu sana lakini wengi wanazitumia kueneza umbea badala ya mambo mazuri ya maendeleo.

Mama Samia ameyasema hayo jana jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa Baraza Kuu Maalum la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT). Amesema Mwenyezi Mungu amewapa wanawake uwezo wa kubeba mazito na kwamba wanayabeba hayo si kwa kilo zake ila kwa umuhimu wake.

“Vifua vyetu vina mazito sana, ndio maana wengine leo tunahesabu miaka 42 ya ndoa, miaka 50 ya ndoa, miaka 10 ya ndoa, si rahisi, tuna mazito yanapita lakini tunayabeba vifuani kwetu” alisema Mama Samia.

Alisema wanawake pia wana uwezo mkubwa wa akili na hilo linathibitika kutoka na shughuli wanazozifanya’

“Lakini wanawake tuna uwezo mkubwa wa ndimi zetu. Na hapa nataka nipige mstari, uwezo mkubwa wa ndimi zetu. Tukifanya mazuri, tukizitumia ndimi zetu kwa mazuri taifa hili litakwenda mbali sana. Kwa sababu wanawake ni wasambazaji wakubwa wa habari, sasa bahati mbaya tunatumia ndimi zetu kueneza umbea zaidi kuliko kuliko yale ya maendeleo” alisema Mama Samia.

Aliagiza wanawake wajirekebishe, watumie ndimi zao kwa mazuri, walisemee taifa lao, wawasihi viongozi wao ili taifa liende mbele. 

Mama Samia alisema, wanawake pia wana nguvu kubwa ya kutenda na kama wakishirikiana wanaume hawana uwezo wa kuwashinda. Pia aliwataka wanawake hso kujiandaa na kujipanga kwa uchaguzi ili kuhakikisha CCM inapata ushindi mkubwa.

Alipongeza umoja huo kwa kuongeza idadi ya wanachama kutoka 1,752,145 mwaka 2018 hadi wanachama 1,934,744 katika mwaka huu.

 Samia alikemea na kutaka makundi ya uchaguzi yavunjwe na wale watakaobainika kujihusisha nayo chama kitawachukulia hatua.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments