loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ufumo kupima madereva EAC kuzinduliwa kesho

MFUMO wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa madereva na mizigo katika nchi za Afrika Mashariki (RECDTS), utazinduliwa katika mipaka mitano ya nchi za Afrika Mashariki kuanzia kesho mpaka Agosti 31.

Kwa kuanzia, mfumo huo utazinduliwa katika mpaka wa Rusumo kati ya Tanzania na Rwanda kesho na kufuatiwa na mpaka wa Mutukula kati ya Tanzania na Uganda Agosti 14 na Agosti 21 utazinduliwa katika mpaka wa Malaba kati ya Kenya na Uganda.

Agosti 28 mfumo huo utazinduliwa katika mpaka wa Namanga kati ya Tanzania na Kenya na mwisho itakuwa katika mpaka wa Kobero kati ya Tanzania na Burundi Agosti 31.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Teknolojia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Daniel Murenzi, akizungumza katika makao makuu ya EAC, Arusha jana, alisema nchi wanachama wa jumuiya hiyo zimekubaliana kuanza kutumika kwa mfumo huo.

Alisema mfumo huo licha ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona kupitia madereva wa malori, pia utapunguza adha ya kupima mara kwa mara virusi hivyo katika kila nchi.

Uzinduzi wa mfumo huo unafanyika baada ya kufanikiwa kwa awamu ya kwanza ya majaribio iliyoanza Juni 15, mwaka huu.

“Mfumo huu pia utasaidia wanaotumia njia nyingine za usafiri ikiwamo mabasi ya abiria yanayosafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine pamoja na magari ya kawaida yatakaporuhusiwa kuanza kutoa huduma,” alisema. 

Awali, akizungumza na HabriLEO, Murenzi alisema tayari maabara zote katika nchi wanachama zimeunganishwa kwa ajili ya kupima virusi vya corona.

“Baada ya mfumo huo kuzinduliwa Ijumaa kwa ajili ya madereva na makondakta wa malori kutoka nchi za jumuiya na waliopima kupatiwa cheti kinachotambulika na EAC, wiki mbili zijazo tunatarajia kuanza kupima wananchi wengine wanaoingia na kutoka katika nchi hizo.”

"Mfumo huu ambao umechelewa kidogo kuzinduliwa kutokana na kusubiri idhini ya mawaziri wa EAC pamoja na kuunganishwa kwa maabara, utaondoa changamoto zilizokuwapo awali ikiwamo madereva na makondakta kupimwa ugonjwa huo katika kila nchi," alisema. 

Murenzi alisema watakaofika mpakani bila kupimwa watafanyiwa vipimo, kwani EAC imesaidia kila nchi vifaa vya kupima na kisha kuingizwa kwenye mfumo utakaonekana katika mipaka mingine hivyo kutorudia kupima.

Hata hivyo, alisema baada ya kuingia kwenye nchi nyingine, mhusika atapimwa joto na akibainika kuwa na dalili za ugonjwa wa covid-19 atatakiwa kubaki nchini mwake.

Imeelezwa kuwa, hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto iliyojitokeza ya madereva wa malori kuzuiwa kuingia katika baadhi ya nchi kwa madai ya kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona kutoka nchi moja kwenda nyingine.

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi