loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali ya Lebanon yajiuzulu

WAZIRI Mkuu wa Lebanon, Hassan Diab (pichani) ametangaza kujiuzulu kwa serikali yake kutokana na mlipuko mkubwa uliotokea hivi karibuni katika Bandari ya Beirut.

Tangu kutokea kwa janga hilo wiki moja iliyopita, kumekuwa na maandamano ya wananchi ya kuipinga serikali yao. Diab alisema kuwa serikali imejiuzulu ili kuwaunga mkono wananchi wa Lebanon wanaotaka kuwepo kwa mabadiliko ya kweli.

Mlipuko huo umesababisha vifo vya watu 158 na kujeruhi wengine 6,000 na kusababisha maandamano ya wananchi wanaotaka kufumuliwa kwa mfumo mzima wa kisiasa.

Wananchi wanawalalamikia watawala kwa uzembe na kutojali kwa kuhifadhi kiasi kikubwa cha ammonium nitrate katika bandari hiyo na kusababisha mlipuko mkubwa.

Hata hivyo, Diaba alikataa kuwajibishwa kwa vitendo vya rushwa vilivyofanywa na serikali zilizopita.

“Wiki chache baada ya kuundwa kwa serikali yetu, baadhi ya vyama vya siasa vilijaribu kutuwajibisha kwa rushwa, deni la umma na kuanguka kwa uchumi, tuko makini kuhusu nchi hii, mustakabali wake na mustakabali wa watoto wetu, hatuna maslahi binafsi bali tunachotaka ni ustawi wa nchi hii, lakini tumegoma kuburutwa kwa hoja zisizo na maana,”alisema Diab.

Uchunguzi wa milipuko hiyo bado unaendelea. Maofisa waandamizi watatu na watumishi wengine 16 wa bandari hiyo, walikamatwa mwishoni mwa wiki kwa uchunguzi wa mkasa huo.

Wananchi wa Lebanon wameapa kuendelea na maandamano mpaka hapo Bunge nalo litakapojiuzulu na kuitishwa kwa uchaguzi wa haraka wa Bunge.

Diab aliteuliwa Desemba mwaka jana baada ya kutokea kwa maandamano nchi nzima, yaliyosababisha kujiuzulu kwa serikali ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Saada Hariri.

JUMUIYA ya Nchi za Afrika, Carribean na Pacifi c (OACPS) ...

foto
Mwandishi: BEIRUT, Lebanon

Post your comments

Habari Nyingine