loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

RC aunda kamati kuchunguza umiliki soko la Ndugai

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge ameunda kamati maalumu inayoshirikisha wataalamu kutoka ofi sini kwake na Jiji kuchunguza waliojimilikisha vibanda viwili au zaidi katika soko la Ndugai.

Akizungumza na wafanyabiashara katika soko kuu la Job Ndugai jijini hapa, Dk Mahenge alisema kamati hiyo itafanya kazi kwa siku saba, itatakiwa kutoa ripoti kamili ya soko hilo.

Dk Mahenge alisema walengwa wa soko hilo walikuwa wale waliohamishwa kutoka eneo la Jamatini, Sarafina, Stendi ya Mabasi Mjini na maeneo mengine kuhamishiwa kwa muda Nanenane.

Kamati hiyo itakuwa chini ya Ofisa Masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna na viongozi wa wenye magari, mama na babalishe, machinga, bajaji na bodaboda na watendaji wengine kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa.

Pamoja na kuchunguza watu waliojimilikisha vibanda viwili au zaidi, pia itachunguza maeneo ya kufanyia biashara baba na mamalishe, matumizi ya vizimba na uwezekano wa kujenga vibanda kwa kutumia michoro ya jiji.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya baadhi ya wafanyabiashara wakiwemo machinga na wajasiriamali kukosa nafasi katika soko hilo, na kumlalamikia mkuu huyo wa mkoa.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema amesikia maagizo ya Mkuu wa Mkoa na ndani ya siku tano atakuwa amekaa na wataalamu wake kuangalia uwezekano wa kusaidia baba na mamalishe na kuboresha mazingira ya soko hilo kwa ujumla.

Alisema pia ataandaa orodha ya wafanyabiashara wote ambao walihamishiwa Nanenane kwa muda ambao wamekosa maeneo katika soko la Ndugai ili kupewa maeneo katika soko hilo.

Kunambi alisema wafanyabiashara waliohamishiwa Nanenane kutoka maeneo ya mjini waliambiwa watakaa kwa muda na litakapojengwa soko la Ndugai watahamishiwa hapo.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi