loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Manyanya ataka NEC kuzuia mambo ya ovyo

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetakiwa kuchukua hatua inapoona faulo za wazi hasa wakati huu ambapo mchakato wa uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwemo ule wa kutolewa fomu za uteuzi kwa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kwani tayari kuna mambo mengi ya ovyo yanaendelea.

Kwa mujibu wa NEC, fomu za uteuzi kwa wagombea wa ubunge na udiwani zitaanza kutolewa leo.

Akizungumza hivi karibuni kwenye banda la NEC wakati wa maonesho ya Wakulima yaliyomalizika katika viwanja vya Nzuguni jijini hapa, Naibu Waziri wa Viwanda, Stella Manyanya (pichani) alisema kazi kubwa inayofanywa na Tume imekuwa ikionekana hasa katika mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.

“Kazi iliyo mbele ni ngumu kwani kuna watu wanagombea kwa kufuata taratibu lakini wengine sivyo, kuna maneno ya ovyo ovyo, kuchafuana hata kabla ya kuchukua fomu za uteuzi, mambo mengi yanaonekana, mkiona faulo za waziwazi mchukue hatua, hata vyombo vya sheria vichukue hatua ili uchaguzi uwe wa haki,”alisema.

Alisema pia kuna haja ya kuhakikisha elimu wanazotoa zinawafikia wananchi waliopo vijijini na kuweka mazingira ya kupata elimu kwa makundi mbalimbali ikiwemo wajasiriamali na makundi maalumu ikiwemo walemavu.

“Taifa linakwenda kufanya maamuzi magumu ya nchi yetu sio maamuzi ya mtu, ni maamuzi ya hatma ya taifa, tukachague kiongozi mwenye mapenzi mema na nchi yetu atakayelifanya taifa lizidi kusonga mbele,” alisema.

Alisema kila mmoja anatakiwa kuzingatia kanuni na taratibu na wananchi wasikubali kutumika na kikundi chochote kwa kufanya mambo yanayohatarisha amani. Alivitaka vyama vya siasa kuheshimu sheria za nchi ili uchaguzi ufanyike kwa haki na amani.

Pia alisema baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwe na tume huru ya uchaguzi na kufafanua “Tume iliyopo ni huru, twende kwenye uchaguzi sasa”. Kwa upande wake, Ofisa Elimu Idara ya Habari na Elimu kwa Mpigakura, Johari Mutani alisema wanawafikia wananchi kwa kutoa elimu kwa njia mbalimbali, ikiwemo matangazo, vipindi vya redio, blogu na kuweza kukutana moja kwa moja na wapiga kura.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na NEC, uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani utafanyika Oktoba 28, mwaka huu. Fomu za uteuzi kwa wagombea wa kiti ya Rais na Makamu wa Rais zimeanza kutolewa Agosti mosi hadi Agosti, 25 mwaka huu katika ofisi za NEC Njedengwa Jijini Dodoma.

Pia fomu za uteuzi kwa wagombea ubunge zitaanza kutolewa leo hadi Agosti 25 mwaka huu katika ofisi za halmashauri husika. Fomu za uteuzi kwa wagombea udiwani zitaanza kutolewa leo hadi Agosti 25 katika ofisi za kata husika.

Aidha uteuzi wa wagombea kiti cha rais, makamu wa rais, ubunge na udiwani utafanyika Agosti 25, mwaka huu. Kampeni za uchaguzi zitaanza Agosti 26 na hadi Oktoba 27, mwaka huu na Oktoba 28, mwaka huu itakuwa siku ya Uchaguzi Mkuu.

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi