loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wasiosikia washirikishwe Uchaguzi Mkuu mwaka huu

WALEMAVU ni moja ya makundi ambayo yanahitaji kushirikishwa vema katika harakati mbalimbali zifanyikazo nchini, ikiwa ni hatua mojawapo ya kuzingatia demokrasia kwa wote.

Kwa kufanya hivyo, makundi hayo kulingana na ulemavu walionao, watakuwa wameondoa dhana ya kubaguliwa ama kutengwa kwa namna moja au nyingine.

Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika nchini Oktoba 28, baadhi ya walemavu wasiosikia wametoa kilio chao kuwa, kutokana na ukubwa wa tatizo linalowakabili imekuwa vigumu kufuatilia na kuzielewa sera za wagombea na kujikuta wakichagua sura ya mtu siku ya kupiga kura.

Jambo hilo si la kunyamaziwa hata kidogo na mamlaka husika wakiwemo wagombea wa ngazi zote, kwani suala la msingi ni kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika uchaguzi huo kwa kuelewa kile kinachokwenda kufanywa na mgombea wa nafasi husika endapo akichaguliwa.

Kundi la walemavu wasiosikia limekuwa likieleza changamoto zao mara kwa mara kuwa ni kukosekana kwa wakalimani katika nyanja mbalimbali za maisha, ikiwamo wakati wa mchakato wa uchaguzi, kutangaza sera hadi upigaji kura, hivyo wakijikuta wakibahatisha juu ya kile kinachoendelea.

Wapo pia walioshindwa kwenda kwenye nyumba za ibada kulingana na imani zao kutokana na tatizo hilo kutokana na kutoelewa kile kinachozungumzwa na kubaki kuwa watazamaji.

Makamu Mwenyekiti wa Sauti ya Wanawake Wenye Ulemavu Tanzania (Swauta), Tatu Kondo, anasema kutokana na walemavu wasiosikia kukosa wakalimani wa lugha ya alama, hujikuta wakipiga kura kwa mtindo wa kufumba macho na kuimba ‘ana ana ana dooo’ na kumchagua ambaye wimbo huo umeishia kwake.

Anasema wakati wa kupiga kura, wasiosikia wanaangalia sura za watu badala ya sera na maelezo ya mgombea ambayo yanaeleza atafanya nini au atawasaidiaje akichaguliwa.

Kutokana na maneno ya kiongozi huyo ni wazi kuwa, kundi hilo linatamani kusikia yanayosemwa na wagombea, lakini hujikuta wakiishia patupu.

Hivyo, ni vema kuelekea uchaguzi mkuu wakaandaliwa wakalimani watakaotumika wakati wa kampeni kwa wagombea wote na vyombo vya habari vya televisheni waweze kujua kinachozungumzwa ili kuwapa fursa wenye ulemavu wa kutosikia ya kuwa na uwanda mpana wa kuwachagua viongozi wanaowafaa.

Inawezekana kwa upande mwingine kundi hilo hubaki kuelezwa sera za mgombea katika familia, jambo ambalo ni hatari kwa kuwa sio wote wanaweza kuwa wapenzi wa mgombea fulani ama chama fulani, hivyo wakapotoshwa.

Ikumbukwe kuwa, kwa mujibu wa Katiba, kila mtu ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa katika wadhifa fulani, hivyo kwa kundi hilo ili lisijione kuikosa haki hiyo linapaswa kuwekewa utaratibu mzuri wa kujua yanayoendelea wakati wote wa kampeni na uchaguzi wenyewe.

Kwa mantiki hiyo, kuelekea uchaguzi mkuu, ni muhimu basi kwa wagombea kuanzia kwenye kampeni kuwa na wakalimani watakaotafsiri wanachozungumza wakiwa majukwaani.

Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ione ni kwa namna gani kundi hilo litashiriki kikamilifu katika uchaguzi.

KAMPENI za uchaguzi kwa ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi