loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wagoma kutoa michango mpaka wasomewe mapato

WAKAZI wa mtaa wa Gezaulole wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wamegoma kutoa michango hadi watakaposomewa taarifa ya mapato na matumizi ya michango ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ya Shule ya Msingi Gezaulole.

Walisema hayo baada ya kupokea msaada wa mifuko 20 ya saruji kutoka kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai ole Sabaya, kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Akiwasilisha msaada huo kwa niaba ya Sabaya, Ofisa Tarafa Masama, Nsajigwa Ndagile alisema serikali imetoa mifuko hiyo na Shule ya Msingi Uhuru ilitoa mifuko 20 kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo ambao ulianzishwa mwaka 2017 na aliyekuwa Mkuu wa wilaya hiyo kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Glasius Byakanwa.

Alisema lengo la kuanza ujenzi huo ni kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani lakini kutokana na mradi huo kukwama kwa muda mrefu serikali imeona itoe mifuko hiyo ya saruji halafu wananchi waunge mkono kwa kuchangia.

Hata hivyo wakazi hao walianza kulalamika na kupiga kelele wakidai wasomewe taarifa ya mapato na matumizi ya fedha walizochanga kwa ajili ya ujenzi huo.

Mkazi wa Kijiji hicho, Eliasifiwe Lema alisema wakati wanaanza ujenzi huo wananchi walikuwa wanachangia Sh 25,000 na fedha zilikusanywa nyumba kwa nyumba.

Pia wadau mbalimbali walichanga hadi ujenzi ukafikia hatua ya kuezekwa kwa madarasa matatu. Naye Kanshabee Tegemea alisema ili waendelee kuchanga, wanaomba kamati ya ujenzi iitwe itoe taarifa ya mapato na matumizi na ikiwezekana Mkuu wa Wilaya, Sabaya afike hapo ili asikie na kuona mambo yaliyosababisha ujenzi kukwama kwa muda mrefu.

Awali Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Veronica Kitosio alisema shule hiyo ina upungufu wa vyumba vya madarasa kwa muda mrefu, jambo lililosababisha msongamano wa wanafunzi darasani na ufundishaji kuwa mgumu.

Alisema tayari chumba kimoja kimekamilika, vimebaki vyumba viwili kuwekewa sakafu, madirisha, milango, plasta, rangi na ili ujenzi ukalimilike unatarajiwa kugharimu Sh milioni 39.

JAMII imehadharishwa dhidi ya tabia ya ...

foto
Mwandishi: Flora Mwakasala, Hai

1 Comments

  • avatar
    Lucas Shayo
    12/08/2020

    Safi kwa maamuzi yao

Post your comments

Habari Nyingine