loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Sekta ya kilimo inahitaji uwepo wa amani, utulivu’

MAKAMU wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi amesema ustawi wa sekta ya kilimo unahitaji uwepo wa amani na utulivu ndani ya taifa ili wananchi wanaotegemea sekta hiyo wapate maendeleo yatakayochangia pato la taifa.

Alisema bila ya amani na utulivu hakuna mwananchi yeyote atakayethubutu kwenda shambani au baharini kutafuta riziki na hatimaye atashindwa kupata mahitaji muhimu ya kila siku, ikiwemo chakula pamoja na matibabu.

Balozi Iddi alisema hayo wakati akiyafunga Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu Nanenane yaliyofanyika Chamanangwe Mkoa wa kaskazini Pemba ambayo ni mara ya tatu kuadhimishwa katika kisiwa cha Pemba.

Alifahamisha huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu ambapo harakati nyingi za kisiasa zitakuwa zikipamba moto na kuwashirikisha makundi mbalimbali ambapo uvumilivu wa kisiasa unahitajika kuepuka jazba za kisiasa.

“Huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu ambapo harakati za kisiasa zitapamba moto, ikiwemo mikutano ya kampeni lakini kitu kikubwa kwa wananchi kujenga tabia ya uvumilivu wa kisiasa na kuepuka kauli za chuki na jazba,”alisema.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imejipanga kuhakikisha sekta ya kilimo na uvuvi inapata msukumo mkubwa kwa ajili ya kutumia eneo la bahari kuu kukuza uchumi na uwekezaji.

Tayari juhudi hizo zimeanza kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kununua meli mpya ya uvuvi Mv Sehewa III ambayo itakuwa ikivua katika maeneo ya bahari kuu.

‘’Tumejipanga kulitumia eneo la bahari kuu kwa ajili ya uwekezaji wa sekta ya uvuvi na kuona vijana wanapata ajira na kuinua hali zao za kiuchumi, tayari meli ya Mv Sehewa III imeanza kuvua katika ukanda huo,” alisema.

Aidha, Balozi Iddi aliwapongeza watendaji wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa kazi kubwa ya kusimamia na kuyaendeleza maonesho ya kilimo kwa muda wa miaka mitatu sasa kwa mafanikio.

Mapema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Dk Omar Ali Amir alisema maonesho hayo yamehudhuriwa na zaidi ya taasisi za 180, ikiwemo wajasiriamali ambao wameonesha ujuzi na ubunifu wa kutengeneza bidhaa mbalimbali za asilia.

“Maonesho haya ni endelevu kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wetu kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya kuonesha bidhaa zao wanazozizalisha na kuingia katika ushindani wa soko,” alisema

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi