loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Abbasi: Tanzania ipo vizuri kidiplomasia

MSEMAJI Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbasi amepinga mtazamo kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi nyingine, umepungua kutokana na hatua zilizochukuliwa kupambana na janga la corona.

Hatua hizo ni pamoja na kuruhusu wananchi waendelee na shughuli zao wakati nchi nyingi watu wanazuiwa kutoka majumbani.

Alisema jana kuwa uamuzi wa serikali kupambana na janga hilo ulikuwa wa dharura, kwa kadri ilivyoona inafaa na hata nchi nchi nyingine zilikabili virusi vya corona kivyao.

Aliyasema hayo wakati anahojiwa kwenye kipindi cha Front Page kinachorushwa na Kituo cha Redio Global jijini Dar es Salaam.

“Watu wasichanganye nchi moja kuchukua hatua inazoamini zitawasaidia kupambana na corona halafu ukasema hiyo nchi inazuia nchi nyingine ushirikiano wake, hapana. Corona ilikuwa ni surprise, mataifa yenyewe makubwa yamepigwa kuliko hata sisi kwa hiyo kila mmoja ali-panic kwa namna yake” alisema. 

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kila nchi ilifanya ilichoamini ili kudhibiti virusi vya corona na kwamba Tanzania ipo vizuri na mataifa mengine.

“Kwa hiyo nchi ikifunga mpaka huwezi kusema kakufungia mpaka, hamna undugu, sio kweli. Sisi na Kenya tupo vizuri, kuna wakati wao waliamini wakifunga mpaka wata- control (watadhibiti) corona, wamefunga corona bado ipo…Zambia nae aliona hiyo ni approach akifunga mpaka corona itakuwa hamna, sijui anaendeleaje”alisema.

Dk Abbasi alisema kuwa Tanzania inatumia Kanuni za Diplomasia katika kushirikiana na mataifa mengine na alitoa mfano ushirikiano na Kenya kwamba hakuna ugomvi, lakini mambo yanaenda kwa kuzingatia Kanuni hiyo.

“Ukisema ndege zako hazitakuja kwangu, mimi nakuja kwako kufanya nini, kwa hiyo wala sio ugomvi, ni Kanuni ya Diplomasia…walisema katika ndege zinazoruhusiwa kwenda kwao sisi hatumo, ina maana zile ni nchi zinafanya assessment (tathmini) zaidi labla siku fulani angeturuhusu, siku fulani angeturuhusu…

“Lakini sisi tukasema kama ambavyo diplomasia inaruhusu, na kwa kuheshimu kwa kweli maoni ya jirani yetu mzuri huyu ambaye tuna ushirikiano naye tu wa damu na wa kindugu, basi kama sisi hatumo kwenda, basi kwa kipindi hiki pia na wao wapumzike”alisema.

Kanuni za maudhui kwenye redio, televisheni

Dk Abbasi alsema kuwa serikali imeweka Kanuni Mpya za Maudhui kwenye Redio na Televisheni ili kuilinda nchi katika masuala kadhaa yakiwemo maadili, faragha za watu na taifa, kudhibiti kashfa na kulinda usalama wa taifa.

Alisema kuwa redio na televisheni nyingi za kimataifa, hazina mitambo nchini hivyo kulikuwa na pengo katika kudhibiti mambo hayo ya muhimu.

“Wewe unatoka huko unapotoka unatugongea tu maudhui yale, unatugongea tu, brothers and sisters lazima nchi tuilinde”alisema Dk Abbasi. 

Alisema si kweli kuwa Kanuni mpya, zitazuia kukua kwa lugha ya Kiswahili na hakuna uhusiano wa kanuni hizo na maendeleo ya lugha hiyo.

“Uhusiano ni kwamba maadili ya taaluma ya habari lazima yaenziwe na yazingatiwe bila kujali double standards. Kwa hiyo hiyo Kanuni imekuja kuweka mawanda hayo ya taratibu kwenye hilo eneo,”alisema.

Dk Abbasi pia alisema kuwa kutafuta pande zote zinazohusishwa kwenye taarifa husika si jambo la hiyari, na kwamba suala linalohusu sekta fulani, lazima atafutwe mhusika wa sekta husika zikiwemo wizara.

“Wasipopatikana sema hawajapatikana, kwa sababu na sisi serikalini tunaambiana na hatuna cha kuficha. Tumechapa kazi, changamoto zipo kama ambavyo nchi yoyote duniani ina changamoto”alisema na kubainisha kuwa mtendaji akishindwa kutoa taarifa, yeye (Dk Abbasi) apewe jina la mhusika.

“Kwa hiyo dhana ya kusema ni tuhuma sija-balance, tuonyeshe umefanya hiyo jitihada ya kwanza na sio uzandiki tu. Umepiga tu listori mtu katoka, atuhumu tu nchi yetu, hapana”alisema.

Taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeeleza kuwa serikali kupitia wizara yenye dhamana ya Habari na Utangazaji, imetoa Kanuni Mpya za Maudhui ya Redio na Televisheni.

Kanuni hizo zinalenga kuboresha huduma za maudhui ya redio na televisheni na usimamizi wake, kutokana na uzoefu uliopatikana kwa kipindi cha miaka miwili tangu kanuni za zamani zilizoanza kutumika mwaka 2018.

Kwa mujibu wa TCRA, miongoni mwa maboresho yaliyopo kwenye Kanuni Mpya ya mwaka 2020 ni: Mwenye leseni hataruhusiwa kujiunga na mtoa huduma za maudhui mwingine, kwa kurusha matangazo ya nyumbani au ya kigeni bila kibali kutoka katika ofisi za mamlaka.

Pia, baada ya kupata kibali cha kujiunga na mtoa huduma mwingine wa maudhui. mwenye leseni atawajibika kwa maudhui yoyote yasiyozingatia sheria na kanuni hizi.

Aidha, mwenye leseni ya maudhui haruhusiwi kutembelea au kufanya biashara na raia wa kigeni inayohusu urushaji wa maudhui bila kuambatana na ofisa wa serikali au mfanyakazi kutoka mamlaka.

Chadema kuongeza maneno Wimbo wa Taifa

Dk Abbasi alisema suala la Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuingiza maneno yao kwenye wimbo wa Taifa, limeachwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuwa ndiyo mamlaka sahihi ya kushughulikia jambo hilo.

Alionya kuwa si sahihi kudhani kwamba kwa kuwa kuna uchaguzi, basi unaweza ukaachwa uvunje sheria na pia dhana ya uvumilivu wa kisiasa haina nafasi kwenye utekelezaji wa sheria.

“Sio kwamba serikali itawavumilia wanaovunja sheria kipindi hiki, yaani nasema tena hapana, na wala hataogopwa mtu” alisema.

Alisema Msajili amewaonya Chadema, pengine kwa sababu sheria inamtaka afanye hivyo kwanza na hafahamu chama hicho kimeieleza nini mamlaka hiyo ya serikali.

“Wakati wa uchaguzi sheria hazisimami kutekelezwa. Kwa hiyo usije ukaweka tafsiri yake kwamba sasa hivi bwana kuna hiyo unayosema political tolerance (uvumilivu wa kisiasa), lakini sivyo hali ilivyo… sheria mbalimbali za nchi zipo na zinaendelea kutumika isipokuwa yapo mambo serikali inachagua, priorities (vipaumbele)”alisema.

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amewaonya Chadema wasithubutu kuongeza aya katika Wimbo wa Taifa, kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

"Jambo la kuchukua Wimbo wa Taifa na kuongeza aya ya tatu si jema. Sikutegemea chama cha siasa kikongwe namna ile kifanye uvunjifu wa sheria kwa makusudi tukae kimya"alisema Jaji Mutungi hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi