loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maaskofu, mashehe wapinga siasa misikitini, makanisani

VIONGOZI wa dini kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), wamekutana kujadili amani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, huku wakionesha kukerwa na rushwa sambamba na viongozi wanaochanganya dini na siasa.

Aidha, Katibu wa Baraza la Ulamaa Kitaifa, Shehe Hassan Chizenga alisema kuwa ipo haja Watanzania watenge siku tatu kwa ajili ya kufanya maombi maalumu kwa Mungu ili awavushe salama katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kama walivyoomba na Mungu akawavusha dhidi ya janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid- 19).

Walikutana jana kwenye mkutano wa kitaifa wa viongozi wa dini Tanzania, uliofanyika Kurasini, Dar es Salaam kwa lengo la kujadili haki, wajibu wa kijamii na ushiriki wa wanachi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Oktoba 28, 2020.

Katika mkutano huo, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini alionesha kukerwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa dini kuwa wakereketwa wa vyama vya siasa.

“Viongozi wa dini wanaweza kuhamasisha vizuri watu juu ya demokrasia na uchaguzi, lakini ili wafanikiwe katika hilo inabidi kiongozi wa dini asiwe mwanasiasa mkereketwa… akitaka kuwa mwanasiasa wa chama kwanza avue joho la uongozi wa dini na aingie siasa” alisema Kilaini.

Katibu Mkuu wa TEC, Padri Dk Charles Kitima na Shehe wa Mkoa wa Kagera, Haruna Kichwabuta waliilaumu tabia ya baadhi ya wanasiasa, kutaka kununua uongozi kupitia rushwa.

“Ili amani iliyopo iendelee kudumu, tusikubali wapigakura kuuza haki, wala wagombea kununua haki ya kuchaguliwa kupitia rushwa maana wenye uwezo kipesa wanaweza kumiliki haki ya kuchaguliwa na wasio na uwezo huo wakabaki kunung’unika na hivyo, kuwa sababu ya uwezekano wa kutoweka kwa amani,”alisema Shehe Kichwabuta. 

Mwenyekiti wa Wanawake wa Kiislamu Tanzania katika Bakwata, Shamim Khan alimpongeza Rais John Magufuli kwa kuanzisha utaratibu unaodhibiti rushwa katika uchaguzi kwa kufanya uchaguzi kuwa wazi na huru zaidi.

Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema ili kulinda amani katika uchaguzi, wagombea watakaoshindwa, lazima wakubali matokeo na mamlaka zisimamie haki na amani kwa wote.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Makamu wa Kwanza wa Rais wa CCT, Askofu Fredrick Shoo alisema kuwa ili kuwe na amani, kabla wakati na baada ya uchaguzi, wagombea wazingatie sheria na kutoa sera badala ya matusi, kashfa na kejeli kwa wagombea, vyama na serikali.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Shehe Hassan Mataka alisema kuwa ili kuwe na amani endelevu, kila kiongozi wa chama, mgombea, mpigakura na wananchi kwa jumla, watimize wajibu wa kulinda na kuheshimu haki za wengine.

Katika mada isemayo Amani ni Matokeo ya Haki, Shehe  Issa Othmani Issa kutoka Bakwata alisema endapo viongozi wa dini, watashindwa kuwajengea waumini wao amani ya ndani, uchaguzi mkuu unaweza kuwa na mushkeli.

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi