loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waliochukua fomu urais wafikia 16

MGOMBEA urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itamteua agombee nafasi hiyo na akishinda, ataimarisha uchumi na usawa na kuhakikisha fedha zinapatikana mikononi mwa watu.

 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage alimkabidhi Profesa Lipumba fomu za uteuzi katika jengo la makao makuu ya NEC, Njedengwa jijini Dodoma. 

Lipumba alisema akishinda pia atahakikisha nchi inakuwa na Katiba mpya. 

"Mpango wetu ni kuhakikisha kwamba tunapata Katiba Mpya iliyoandikwa kwa kuzingatia malengo ya taifa," alisema Profesa Lipumba.

Alisema kuwa ataendeleza uchumi na kwamba mkakati wake unaenda sambamba na mkakati wa dunia wa kutokomeza umasikini ifikapo 2030.

 Alisema kuwa sera yake ni kuhakikisha kwamba anakuza uchumi nchini na kuongeza mzunguko wa fedha katika soko la ndani nchini. 

 Profesa Lipumba alisema biashara zinaanguka na uwekezeji hauendelei, hivyo nchi inahitaji mabadiliko kwa ajili ya kuhakikisha serikali inatoa huduma bora za jamii zikiwemo za elimu na afya. 

 Lipumba alikwenda kuchukua fomu akiwa ameongozana na Mgombea Mwenza, Hamida Abdullah Huweishi.

 Hii ni mara ya tano kwa profesa huyo wa uchumi kugombea urais. Aligombea kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa 1995 na miaka yote anasimama kwa tiketi ya CUF. Aliendelea kusimama kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi wa 2000, 2005 na 2010 isipokuwa uchaguzi wa mwaka 2015.

 Wakati huo huo, mgombea wa Chama cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele alifika ofisi za NEC  jana kuchukua fomu za uteuzi kuwania urais wa Tanzania. Alikwenda hapo akiwa  na Mgombea Mwenza, Ali Said Issa.

 Mwaijojele alisema kuwa mpango wake ni kuhakikisha anafanya kampeni za kistaarabu na kwamba chama chake kinalenga kufanya mabadiliko kwa kuboresha maisha ya wakulima nchini.

 Katika tukio lingine, Mgombea wa NCCR-Mageuzi, Yeremia Kulwa Maganja alifika katika ofisi za NEC jana kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi ya urais nchini. 

Maganja alifika ofisini hapo na Mgombea Mwenza, Haji Ambar Khamis.

 Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Maganja alisema kuwa chama chake kimejiandaa vizuri kushiriki uchaguzi na kushinda. Aliomba tume kuhakikisha inamtangaza mshindi wa kweli. 

 Alisema kuwa NCCR-Mageuzi inataka kufanya mabadiliko ya nchi kwa kuendeleza uchumi wa nchi. Aliahidi kuboresha Bunge, kuimarisha utawala wa sheria na kusaidia wakulima nchini.

 Maganja ambaye ni mfanyabiashara wa Dar es Salaam, alisema anajua changamoto zinazokabili jamii ya wafanyabiashara nchini. Alisema kuwa serikali atakayounda itazingatia na kutilia mkazo uzalishaji, badala ya kutegemea zaidi kodi. 

 "Najua hata wafanyakazi wa serikali hawajapata haki zao kama nyongeza ya mishahara na kupandishwa vyeo na madaraja, hivyo serikali yangu inatashughulikia changamoto hizo za wafanyakazi serikalini mapema," alisema.

Jana jioni mgombea wa chama cha ADA Tadea, John Shibuda alifika ofisi za NEC kuchukua fomu za uteuzi. Uchukuaji wa fomu hizo ulianza Agosti 5 mwaka huu jijini Dodoma.

Mgombea wa kwanza kuchukua fomu hizo alikuwa Seif Maalim Seif kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), akiwa amefuatana na Mgombea Mwenza, Rashid  Rai na wanachama wachache wa chama hicho. 

Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli tayari amechukua fomu ya kuwania tena urais. Alishinda kwa kura nyingi katika uchaguzi mkuu uliopita. 

Wagombea wa vyama vingine waliochukua fomu mpaka sasa ni wa: Chama cha Democratic Party (DP), National Reconstruction Alliance (NRA), United Democratic Party (UPDP), ACT-Wazalendo, Alliance For Democratic Party (ADC), Sauti ya Umma (SAU),  Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Chama Cha Demokrasia Makini.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi