loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Pwani yapokea bilioni 33.6/- za elimu bure

MKOA wa Pwani umepokea Sh bilioni 33.6 kupitia mpango wa elimu bure kwa kwa kipindi cha miaka minne. Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, alipokuwa akizungumza na viongozi, wataalamu na uongozi wa Shule ya Sekondari Bagamoyo, wakati wa ziara yake ya kutembelea mkoa huo kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo.

Mkuu huyo wa mkoa aliwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kuhakikisha ifikapo Septemba mosi, mwaka huu, madawati 30,000 kwa ajili ya shule za msingi na viti na meza 22,000 kwa ajili ya shule za sekondari yanapatikana na kusiwe na mwanafunzi anayekaa chini.

Alisema serikali imekuwa ikiweka mkazo mkubwa kwenye sekta ya elimu ili kumaliza changamoto zinazokwaza sekta hiyo.

“Tunaishukuru serikali kwa kuweka mpango huu wa elimu bure ambapo wananchi wameondolewa kero ya michango mbalimbali na umewezesha wanafunzi kupata elimu bila malipo.”

“Haiwezekani wanafunzi wakae chini wakati mkoa una maeneo ya misitu kama Rufiji ambako kuna miti ya mbao pamoja na magogo ambayo yanaweza kutengenezwa madawati, viti na meza,” alisema.

Aidha, Ndikilo alisema shule kongwe tano za mkoa wa Pwani zimepewa fedha na serikali kwa ajili ya ukarabati, ambazo ni Bagamoyo, Kibiti, Kibaha, Ruvu na Minaki na kuwataka walimu kuongeza ufaulu ili iwe shukrani kwa Rais John Magufuli kwa kutoa fedha hizo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Bagamoyo, Khalfan Milongo, alisema serikali imeipatia shule hiyo Sh milioni 935 kwa ajili ya ukarabati wa mabweni, ofisi, nyumba za walimu, vyoo na usambazaji wa maji safi na majitaka.

Alisema wakati wa ukarabati huo walikumbana na changamoto kadhaa, ikiwamo kuadimika kwa bidhaa za ujenzi kama saruji na wanahitaji fedha kwa ajili ya kukamilisha sehemu ya jiko katika shule hiyo yenye wanafunzi 691 iliyoanzishwa mwaka 1973.

foto
Mwandishi: John Gagarini, Bagamoyo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi