loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkapa alilenga kujenga Ujamaa katika mazingira mapya - 3

Hii ni sehemu ya tatu na ya mwisho ya ushuhuda wa Mzee Ferdinand Kamuntu Ruhinda juu ya rafiki yake wa zaidi ya miaka 50, Benjamin William Mkapa, Rais wa Tatu wa Tanzania, aliyefariki dunia Julai 23 na kuzikwa Julai 29, mwaka huu kijijini kwao Lupaso mkoani Mtwara.

Mzee Ruhinda ni Mwandishi wa Habari, Mshauri na Mwanastratejia wa Siasa, Mhariri na aliyepata kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Canada na Jamhuri ya Watu wa China.

Endelea kusoma… Benjamin William Mkapa alikuwa muumini wa dhati wa mambo makubwa kadhaa ambayo ndiyo yalikuwa falsafa kuu na misingi mikuu ya urais wake na uongozi wa Tanzania kwa miaka 10, na hata kabla ya kuingia madarakani.

Kwanza, alikuwa mwanafunzi na mfuasi mwaminifu wa Mwalimu Nyerere. Pili, alikuwa muumini wa Sera ya Uwazi na Ukweli. Tatu, aliamini katika ujenzi wa uchumi wa kisasa, kama njia ya uhakika na kisayansi kuwatoa watu katika umasikini. Nne, alichukia unyonyaji wa mtu kwa mtu. Tano, aliamini katika uongozi wa pamoja na alichukia mno tashihisi, yaani tabia ya kuabudiwa (personality cult). Sita, aliamini kuwa nchi haiwezi kujengwa kwa misingi ya kusadikika na kufikirika (utopia).

Hivyo ndivyo Balozi Ferdinand Kamuntu Ruhinda, rafiki wa karibu wa kimaisha, kifamilia na kisiasa wa Benjamin Mkapa kwa zaidi ya miaka 50, anavyoeleza, kwa ufupi tu, misingi mikuu iliyomwongoza Mkapa katika uongozi wake.

“Benjamin Mkapa alikuwa muumini na mwanafunzi wa Mwalimu Nyerere, kama tulivyokuwa Watanzania wote. Lakini hakuwa mwanafunzi wake wa darasani (si kweli kuwa Mwalimu alimfundisha Mkapa pale Pugu).

Mkapa aliingia Pugu wakati Mwalimu anajiuzulu ama amejiuzulu kazi ya ualimu. Hivyo, uanafunzi wa Ben kwa Mwalimu ni wa siasa, tabia na uongozi.” “Kubwa hapa ni kwamba, Benjamin Mkapa alikutana na Mwalimu mapema sana katika maisha yake, mara tu baada ya masomo yake, na akafanya kazi naye kwa miaka mingi, na akawa muumini wa kiongozi huyo, ambaye aliamini katika Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, “anasema Mzee Ruhinda na kuongeza: “Na kama tunavyojua, Mwalimu alilenga kujenga Ujamaa wenye misingi ya Utamaduni wa Kiafrika.

Hii ilikuwa tofauti na baadhi ya watu walioamini kuwa Ujamaa lazima ujengwe kwa kupambanisha matabaka ndani ya jamii. Sasa nyie mnajua kuwa binafsi nimeishi na kutembelea baadhi nchi za nje ambazo nyingine zilijenga ama zinajaribu kujenga ujamaa – China, Sweden, Korea Kaskazini, Cuba na pia nilikaa Canada.

Moja ya mambo niliyojifunza ni kwamba katika nchi zote, hakuna kiwango kilicho sawa (standard) cha ujenzi wa Ujamaa.” “Korea Kaskazini kule sijui hata wanajenga Ujamaa wa namna gani. Cuba wao wako katika mapambano yao ya miaka mingi na Marekani.

Sweden ni sehemu ya nchi za Scandinavia ambazo zina mfumo wa dola la ustawi (welfare state). China wao wanajenga Ujamaa wenye sifa za Kichina (socialism with Chinese characteristics)… Sasa utaona kuwa hakuna standard moja ya ujenzi wa Ujamaa duniani.” Anafafanua Balozi Ruhinda:

“Bwana Mkapa naye, kama nilivyosema, alikuwa muumini na mwanafunzi wa Mwalimu, na kama alivyokuwa Mwalimu, Ben alichukia unyonyaji wa mtu kwa mtu, hata kama alijua kuwa binadamu lazima wawe tofauti. Lakini tofauti zile zisitokane na kundi moja lenye uwezo kuwanyonya wasiokuwa nacho.

Aliamini katika jamii sawa, na alilenga kujenga usawa miongoni mwa Watanzania.” “Kwa maneno mengine, Ben alijitwisha mzigo wa kujenga Ujamaa lakini katika mazingira mapya ya Tanzania na kwa kupitia hali halisi ya nchi yetu.

Hii ni sawa zilivyofanywa ama zinavyofanya nchi nyingine nilizozitaja hapo juu katika kujenga Ujamaa, kila nchi katika mazingira na hali halisi yake.” “Ben, kama ilivyo siasa yetu ya Ujamaa, alipinga sana unyonyaji na alilenga kujenga usawa mongoni mwa watu.

Falsafa yake na hatua zake zote zililenga kufanikisha hayo mawili – kufuta umasikini na kujenga usawa katika nchi yetu. Huu ndiyo msingi wa kuundwa kwa taasisi kama TASAF, na kubuniwa kwa programu kama vile Dira ya Maendeleo ya 2025 na kuwekwa kwa misingi ya uchumi wa kisasa,” anafafanua Mzee Ruhinda.

Anaelezea kuwa katika kufanikisha lengo la kuwatoa watu katika umaskini, ambalo pia ndiyo lilikuwa lengo kuu la Siasa ya Ujamaa, Mkapa alibuni mbinu mbalimbali za utekelezaji wa azma hiyo kwa sababu alijua fika kuwa ilikuwa vigumu sana kujenga Ujamaa kwa fikra tu, kwa utopia (njozi) ama kwa njia ya kufikirika na kusadikika.

Moja ya mbinu hizo za kutimiza lengo la kuondoa umaskini, anaeleza Mzee Ruhinda, ilikuwa ni kujenga misingi ya uchumi wa kisasa ambao faida zake zingesambaa haraka kwa watu wengi zaidi. Anasema Balozi: “Rais Magufuli amelizungumzia vizuri sana hili….alitoa hotuba nzuri sana pale uwanjani, na Rais Kikwete ameyarudia yale yale vizuri sana pia katika hotuba yake kule Lupaso wakati wa maziko ya Ben.”

“Wote wamezungumza kwa kina jitihada za Ben kuweka misingi ya ujenzi wa uchumi wa kisasa. Lakini katika ujenzi wa misingi ya uchumi huo wa kisasa, ilibidi achukue hatua nyingine, hata kama hatua hizo zilizua maneno mengi, kama kubuni na kutekeleza Sera ya Ubinafsishaji.”

“Zipo hatua nzuri nyingi ambazo Mwalimu Nyerere alizichukua, lakini utekelezaji ukawa unashindikana, kwa sababu ya hali halisi ya Tanzania, kama vile kutaifisha mashamba na viwanda, na kuunda mashirika ya umma lukuki, yote yakibebwa na kodi ya wananchi.” Anasema: “Sasa wapo watu waliomlaumu sana Mkapa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IFM).

Ushirikiano na mashirika hayo hauwezi kuzuia ujenzi wa Ujamaa, na jamii ya usawa na haki. Leo ukienda China ama Urusi huwezi kusema nchi hizo hazijengi Ujamaa kwa sababu nazo zinashirikiana na mashirika hayo makubwa ya kimataifa ya fedha na uchumi.” “Kama ambavyo Ujamaa usingeweza kujengwa kwa kufikirika (utopia), vile vile uwekaji wa misingi ya uchumi wa kisasa.

Ili kufanikisha mageuzi hayo ya kiuchumi, Ben alilazimika kuangalia mazingira ya nchi na kufanya mabadiliko ya msingi, ili kujenga msingi wa mageuzi yenyewe. Kama nilivyosema hapo mapema, Mkapa alijitishwa mzigo wa kuendeleza fikra za Ujamaa katika mazingira mapya ya Tanzania.” Balozi Ruhinda anageukia suala lingine la msingi katika utawala wa Rais Mkapa na kusema: “Kweli, Mkapa aliweka misingi ya uchumi wa kisasa, lakini hakuwa peke yake katika kuifanya kazi hiyo.

Ilikuwa ni Mkapa akifanya kazi na watu wengine – alikuwa na mawaziri wake na Baraza lake la Mawaziri, alikuwa na chama chake, alikuwa na Benki Kuu ya Tanzania na watu wengine wengi. Dira ile ya Maendeleo ya 2025, sijui sasa imefikia wapi, aliibuni na watu wengine. Kwa hiyo, mafanikio yote haya hakuyaleta Mkapa pekee yake.

Yeye mwenyewe aliamini fika katika uongozi wa pamoja.” “Tuna tatizo kubwa sana la tashihisi (personification) ya mambo, na tabia ya kujenga abudu kwa viongozi (personality cult). Utaratibu huu wa personalization unaendelea sasa lakini ni hatari kujenga abudu katika mambo ya uongozi. Ni kweli, tunahitaji awepo kiongozi, lakini kiongozi si kila kitu.”

“Kwa mfano, tunajisifu sana kuhusu nchi kuingia uchumi wa kati. Mimi sijasoma popote, lakini nasikia Benki ya Dunia ndiyo imetangaza kuwa tumeingia uchumi wa kati. Lakini tukumbuke kuwa huo ni mwanzo tu. Ndiyo kwanza tumefungua milango ya uchumi huo wa kati. Tusijisifu sana kupita kiasi. Safari ya kukamilisha hili na kuwatoa Watanzania katika umaskini bado ndefu.

” Balozi Ruhinda pia anazungumzia nafasi ya Mkapa kama mwandishi wa habari na mhariri wa magazeti na kusema: “Wakati najiunga na The Nationalist, na ninyi wenyewe mmefanya kazi katika vyombo vya habari na mnajua utaratibu huu, tulikuwa tunafanya mikutano ya tathmini ya magazeti kila siku asubuhi.” “Yeye ndiye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo.

Tulijadiliana kwa uwazi, kwa urafiki na uhuru kamili kama wanataaluma. Tulikubaliana na tulihitilafiana. Lakini hatimaye, yeye kama Mhariri ndiye alitoa msimamo wa mwisho.

Na kwa kweli hiyo ndiyo kazi ya Mhariri kutoa msimamo na mwelekeo wa gazeti. Kwa maana hiyo, Mhariri yeyote ni Mdhibiti wa gazeti lake.” Anaongeza Balozi Ruhinda: “Lakini kwa maana ya kwamba yeye Mkapa aliwazuia waandishi kuandika walivyotaka kulingana na sera ya gazeti, ama alizima mawazo yao, hapana, na wakati ule gazeti lile lilikuwa na waandishi kutoka Ghana, kutoka Biafra. Isipokuwa, ni kweli kuwa uamuzi wa mwisho ulikuwa wa kwake, akiwa Mhariri, kama walivyo wahariri wengine wowote duniani.

” Balozi Ruhinda pia anasema kuwa si kweli kuwa Mkapa aliletwa kuongoza gazeti bila kuandaliwa ama kusomea na kupata uzoefu wa kazi na taaluma ya uandishi wa habari.

“Mkapa vile vile alipata mafunzo ya uandishi wa habari,” anasema Mzee Ruhinda na kufafanua: “ Kabla ya kujiunga na vyombo vya habari, Ben alipelekwa kwenye Gazeti la (Daily) Mirror, gazeti kubwa na maarufu la Uingereza, na kufanya kazi kule kwa muda, akipata mafunzo kama mwandishi wa habari na kuandaliwa kuwa Mhariri.” Lakini hata kabla ya kupelekwa Gazeti la Mirror, Ben alikuwa na uwezo mkubwa wa kuandika na hata kuhariri.

“Kwa maoni yangu, Ben alikuwa mwandishi wa habari na Mhariri mzuri.” “Nimalizie, kama nilivyoanza mahojiano haya, kwa kusema: Nilimpenda Ben kwa sababu ya utu na ubinadamu wake. Kama nilivyoeleza, Ben alikuwa na sifa zote nzuri ambazo binadamu anastahili kuwa nazo.

Ni binadamu aliyeongozwa na fikra na nia njema wakati wote katika maisha yake. Buriani Benjamin William Mkapa, rafiki yangu, ndugu yangu.” Waandishi wa makala haya ni waandishi waandamizi nchini.

Kwa sasa, Salva na Nguba wanaongoza Kampuni ya Mawasiliano ya Pioneer Communications, na Tido ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Habari ya Azam Media.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Salva Rweyemamu, Saidi Nguba na Tido Mhando

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi