loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bodi ya Mikopo na elimu kwa wanufaika

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), hivi karibuni imefungua ‘dirisha la maombi’ ya mikopo kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/2021.

Hii ni fursa kwa wanafunzi waliohitimu masomo ya kidato cha sita na ngazi ya stashahada kutoka katika vyuo mbalimbali nchini kutuma maombi ya mikopo ya elimu ya juu ili kuwezeshwa na serikali kugharamia ada, chakula na malazi wanapokuwa masomoni.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi, Abdul-Razaq Badru, katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali imetenga Sh bilioni 464 zinazotarajiwa kuwanufaisha wanafunzi 145,000, wakiwemo wanafunzi 54,000 wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 91,000 wanaoendelea na masomo.

Anasema kiasi hicho cha Sh bilioni 464 kimeongezeka kutoka Sh bilioni 450 za mwaka uliopita (2019/2020) ambazo zilizowanufaisha wanafunzi 132,119. Anasema ongezeko hilo la bajeti linatokana na azma ya serikali ya kupanua wigo wa elimu ya juu, hususani kwa wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi.

Katika kuhakikisha Watanzania wenye sifa stahiki wananufaika na mikopo hiyo, Bodi imetoa mwongozo wa uombaji wa mikopo unaoainisha hatua zinazopaswa kuzingatiwa na waombaji. Mwongozo wa aina hii hutolewa kila mwaka.

Uchunguzi wa Bodi unaonesha kuwa, wanafunzi wengi wamekuwa wakijikuta wanakosa mikopo kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu kutokana na kufanya makosa wakati wa kujaza fomu za maombi ya mikopo kama inavyoelekezwa katika mwongozo wa mwaka husika.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, kuanzia mwaka wa masomo 2019/2020 Bodi imekuwa ikiendesha programu ya mafunzo ya elimu kwa umma kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo ya elimu ya juu kupitia kampeni ya ‘WeweNdoFuture’, kwa kutembelea mikoa mbalimbali ili kutoa ufafanuzi na hatua mbalimbali zinazopaswa kuzingatiwa katika kujaza fomu za maombi ya mikopo ya elimu ya juu.

Hivi karibuni Bodi iliendesha mafunzo ya programu ya elimu kwa umma katika mikoa 14 nchini yakilenga kujibu hoja na kutoa ufafanuzi wa maswali mbalimbali kutoka kwa wadau wa elimu nchini wakiwemo wanafunzi, watendaji wa serikali na watoa huduma za mtandao katika ngazi ya mamlaka za serikali za mitaa nchini.

Mikoa hiyo ni pamoja na Rukwa, Mbeya, Katavi, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Geita, Kigoma pamoja na Zanzibar (mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja Kaskazini, Unguja Kusini, Pemba Kaskazini na Pemba Kusini).

Huko, maofisa mikopo wa Bodi walitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu changamoto wanazokumbana nazo wanafunzi wakati wa uombaji wa mikopo kwa njia ya mtandao.

Katika mikoa ya Geita na Kigoma, maofisa wa Bodi walifanya mikutano saba katika halmashauri za wilaya za Geita, Chato, Bukombe na Mbogwe huku mkoani Kigoma wakizifikia wilaya za Kasulu, Kibondo na Manispaa ya Kigoma-Ujiji.

Maofisa walijibu hoja na kutoa ufafanuzi wa maswali 159 kutoka kwa wanafunzi 3,500 waliohitimu kidato cha sita na masomo ya stashahada katika mikoa hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo mkoani Geita, Meneja Mikopo wa Kanda ya Ziwa, Usama Choka, anasema pamoja na nia njema iliyowekwa na Serikali kuhakikisha wanafunzi wanaotoka katika familia maskini wananufaika na mikopo hiyo, bado miongoni mwao wamejikuta wakikosa fursa hiyo kutokana na kufanya makosa mbalimbali wakati wa kujaza fomu za maombi.

“Wanafunzi wengi wanaotoka katika kaya maskini hususani waliopo katika mikoa ya pembezoni, wamekuwa wakishindwa kukamilisha baadhi ya maelekezo yanayotolewa wakati wa kujaza fomu za maombi ya mikopo ya elimu ya juu kupitia mtandao, hivyo Bodi tumeamua kuanzisha programu hii ya elimu ya mafunzo ya jinsi ya kujaza fomu hizo ili kuongeza wigo wa wanufaika wa mikopo hii,” anasema Choka.

Anasema baadhi ya makosa ni pamoja na waombaji kusahau kupiga mihuri fomu, uwekaji wa saini ya mwombaji pamoja na mdhamini au kuacha kuweka vithibitisho ikiwemo cheti cha kuzaliwa, hivyo kufanya maombi kutofanyiwa kazi.

Choka anasema pamoja na kuendesha kampeni ya elimu kwa umma kuhusu utaratibu wa kujaza fomu za maombi, Bodi ya Mikopo pia imefungua ofisi za kanda katika mikoa sita nchini; Arusha, Mbeya, Dodoma, Mwanza, Mtwara pamoja na Zanzibar ambako Watanzania wanaweza kupata maelekezo muhimu kuhusu mikopo na namna ya kurejesha mikipo kwa wale waliokwishahitimu masomo.

“Tumefungua ofisi kwa malengo mahsusi ya kusaidia waombaji wa mikopo hii ambao idadi yao imekuwa ikiongezeka siku hadi siku,’’ anasema.

Akifafanua zaidi, Choka anasema Bodi pamoja na kutoa mwongozo kwa waombaji wa mikopo katika mwaka huu wa masomo, pia imetoa mwongozo kwa watoa huduma za mtandao (internet) unaoainisha hatua mbalimbali muhimu zinazopaswa kuzingatiwa na watoa huduma za mtandao kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanaotuma maombi ya mikopo ya elimu ya juu.

Ofisa Mikopo wa Bodi, Jonathan Nkwabi, anawataka wanafunzi wanaotuma maombi ya mikopo kwa mwaka 2020/2021 kujihadhari na matapeli ambao mara kadhaa wamekuwa wakiwadanganya kuwa ni mawakala waliotumwa na Bodi na hivyo kudai fedha ili kuwasaidia wakati wa kutuma maombi yao.

“Uzoefu unaonesha katika kipindi hiki huwa kunaibuka wimbi la matapeli wanaoanzisha makundi ya mitandao ikiwemo whatsapp na kuchangisha pesa eti ili wawasaidie waombaji wa mikopo kujaza fomu.”

“Ukweli ni kuwa Bodi haina wakala yeyote. Hao ni matapeli. Tunawashauri wanufaika watarajiwa kusoma vyema mwongozo wetu na iwapo kutatokea changamoto zozote wapige simu zetu zilizotolewa katika mwongozo wa maombi,’’ anasema Nkwabi.

Anasisitiza kuwa, hakuna upendeleo wowote unaotumika wakati wa upangaji mikopo kwa wanufaika wanaokidhi vigezo, alimradi wahitaji wamejaza fomu kwa usahihi na kuambatanisha nyaraka zote muhimu ikiwemo vyeti vya vifo iwapo mwombaji amepoteza mzazi/wazazi.

Akichangia hoja wakati wa mafunzo hayo, Grace Selestine ambaye ni mhitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Udzungwa iliyopo Mkoani Iringa, anaipongeza serikali kupitia Bodi kwa kutoa mikopo ambayo imekuwa faraja kubwa kwa wanafunzi wanaotoka katika kaya maskini.

Anasema utaratibu wa utoaji mikopo ni mzuri kwa kuwa unaongeza fursa na wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu kwa usawa kwani bila hivyo elimu ya juu ingebaki kuwa ya matajiri.

“Tunaipongeza Bodi kwa kuweka utaratibu wa mafunzo elekezi kuhusu namna ya kujaza fomu za maombi ya mikopo. Tunaomba utaratibu huu uwe endelevu,’’ anasema Grace.

Naye Erick Bukuru, mhitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Ilboru ilioko Arusha anasema mafunzo ya mwongozo wa uombaji mikopo yamewasaidia kujua vyema vigezo na sifa zinazotumika katika upangaji wa kiwango cha mikopo baina ya mwombaji mmoja na mwingine kwani awali suala hilo lilikuwa likiwachanganya wanafunzi wengi.

Bukuru anaipongeza Bodi kwa kutoa mwongozo wa uombaji mikopo kila mwaka wa masomo, kwani unawawezesha waombaji wengi kufahamu kipaumbele kinachopangwa na Serikali katika uhitaji wa mikopo ya elimu ya juu na utofauti uliopo baina ya mwombaji mmoja na mwingine na kutokana na sifa na vigezo vinavyoainishwa.

Kwa upande wake, Jeremiah Deus, mhitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Umbwe iliyopo mkoani Kilimanjaro anasema mikopo ya elimu ya juu imekuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi yaliyofikiwa na Tanzania ikiwemo kuifikisha nchi kwenye kipato cha kati kabla ya muda wa malengo yaliyowekwa katika dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025.

“Elimu ndio mhimili wa maendeleo ya nchi, kupitia mikopo ya elimu inayotolewa na Bodi ya Mikopo imesaidia kuzalisha wataalamu wa kada mbalimbali na kuwa chachu ya kufikia nchi ya kipato cha kati.”

“Nashauri kila mwaka Serikali iendelee kuongeza bajeti ili wanafunzi wengi hususani wanaotoka katika familia maskini waweze kunufaika,’’ anasema Jeremiah. Mwandishi wa makala haya ni ofisa wa habari wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB).

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Ismail Ngayonga

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi